Habari MsetoSiasa

UFISADI: Uhuru na Raila wasema sheria ifuatwe

April 4th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa upinzani Raila Odinga ameunga mkono kauli ya Rais Uhuru Kenyatta kwamba sheria inapasa kuzingatiwa katika vita dhidi ya ufisadi.

Hata hivyo, Bw Odinga ambaye ni kiongozi wa ODM alitaka asasi husika kuharakisha kesi za ufisadi ili kuhakikisha kuwa washukiwa na Wakenya kwa jumla wanapata haki.

“Ninaunga mkono usemi wa Rais Uhuru Kenyatta kwenye hotuba yake kwamba vita dhidi ya ufisadi vinapasa kuendeshwa kwa misingi ya sheria. Uchunguzi wa kina lazima ufanyika na ushahidi thabiti kuwasilishwa mahakama kuweza kufanikisha kesi,” akasema.

“Lakini Wakenya wanavunjwa moyo kutokana na hali kwamba kesi hizo huchunguzwa kwa muda mrefu mno. Hali hiyo hiyo hufanyika baada ya kesi kuwasilishwa mahakamani. Ndipo napendekeza kwamba asasi kama vile DCI, DPP na EACC ziharakishe kesi hizo ili pande zote husika zipate haki haraka,” akaongeza Bw Odinga.

Kiongozi huyo ambaye pia ni Balozi wa Umoja wa Afrika (AU) kuhusu Miundo Msingi, alisema kuwa kesi hizo zikiharakishwa ili kuwazima kabisa waporaji wa mali ya umma. “Sharti uchunguzi na mashtaka ya kesi za ufisadi zifikie kikomo,” Bw Odinga akasisitiza.

Kiongozi huyo ambaye ni Waziri Mkuu wa zamani alisema hayo Alhamisi alipoongea na wanahabari katika majengo ya Bunge, Nairobi baada ya Rais Kenyatta kukamilisha hotuba yake kwa kikao cha pamoja cha wabunge na maseneta.

Katika hotuba yake Rais Kenyatta alisema kuwa vita dhidi ya ufisadi sharti viendeshwa kwa sheria ili pande zote husika zipate haki.

“Sharti niseme kwamba nimekuwa nikishinikizwa kuwafuta watu fulani. Lakini sharti nionye kwamba vita dhidi ya ufisadi vitaendeshwa tu kwa misingi ya sheria. Hakuna mtu atakayetuhumiwa kabla ya kusikizwa,” akasema Rais Kenyatta.

Akaongeza: “Nguzo kuu ya demokrasia yetu ni utawala wa sheria sawa na misingi ya kufuata utaratibu ufaao.”

Rais Kenyatta alisema kuwa sharti taifa hili lihakikishe kuwa haifuati haki katika nyanja fulani kupitia ukiukaji wa haki katika nyanja nyingine.

“Nina imani kuwa asasi zetu za kuchunguza kesi za ufisadi na zile za kuendesha mashtaka zitaweza kuhakikisha haki imepatikana kwa misingi ya ushahidi uliopo na uzingativu wa sheria,” akasema.

Hata hivyo, Rais alionya kwamba maafisa wanaochunguzwa kuhusiana na sakata mbalimbali za ufisadi wataondolewa kutoka nyadhifa zao iwapo kesi dhidi yao zitafikishwa kortini.

“Jinsi ambavyo nimewahi kufanya hapo awali, nitachukua hatua na kuwaondoa serikali wale ambao watapatikana kuwa na kesi ya kujibu mahakamani,” akasema huku akishangiliwa na wabunge na maseneta waliohudhuria kikao hicho maalum.

Huku akielezea imani yake kwa utendakazi wa asasi za kupambana na uovu huo, Rais Kenyatta alizitaka kupamba na uhalifu wa kiuchumi kwa kuegemea ushahidi na ukweli.