UFISADI: Wazito sasa wafinywa

UFISADI: Wazito sasa wafinywa

JOSEPH WANGUI na RICHARD MUNGUTI

VITA dhidi ya ufisadi vimeanza kuzaa matunda kwa mara ya kwanza katika historia ya Kenya huku watu mashuhuri walioshtakiwa kwa kuhusika katika sakata mbalimbali wakipatikana na hatia na kuadhibiwa vikali.

Katika miezi michache iliyopita, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), amevalia njuga kesi za ufisadi ambapo waliokuwa watumishi wa umma na wafanyabiashara watajika wamehukumiwa baada ya kupatikana na hatia kwa kushiriki ufisadi.

Baadhi ya walioshikilia nyadhifa kuu serikalini waliopatikana na hatia ya kushiriki ufisadi ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Michezo Hassan Wario, aliyekuwa afisa mkuu Kamati ya Olimpiki (NOC-K) Stephen Soi, Mbunge wa Sirisia, Bw John Waluke na aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kitaifa ya Utafiti wa Kimatibabu (Kemri), Dkt Davy Koech.

Wafanyabiashara wenye ushawishi mkubwa; Bw Mukuria Ngamau na Bi Grace Wakhungu; pia wameadhibiwa kwa kupatikana na hatia ya kuhusika na ufisadi.

Mnamo Alhamisi, Bw Ngamau alitozwa faini ya Sh900 milioni ama atumikie kifungo cha miaka 27 gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kuiba pesa za Hazina ya Kustawisha Vijana Kibiashara (YEDF). Wiki mbili zilizopita, Bw Soi aliyeongoza kikosi cha Kenya kuhudhuria michezo ya Olimpiki 2016, alitozwa faini ya Sh115 milioni au atumikie kifungo cha miaka 17 gerezani.

Bw Soi ambaye alistaafu akiwa na cheo cha juu katika idara ya polisi alihukumiwa na Hakimu Mkuu, Bi Elizabeth Juma aliyempata na hatia ya kutumia vibaya mamlaka ya ofisi, kufuja pesa za umma na kukiuka kanuni na mwongozo wa kusimamia mali ya umma.

Katika kesi hiyo, Bi Juma pia alimtoza Bw Wario faini ya Sh3.6 milioni ama atumikie kifungo cha miaka sita gerezani.

Akipitisha hukumu, Bi Juma alisema wawili hao walisababisha walipa-kodi kupoteza mamilioni ya pesa kutokana na usimamizi mbaya wa fedha.

Alisema wawili hao walitarajiwa kutoa mwongozo mzuri walipoongoza kikosi cha wanamichezo walioshiriki katika Michezo ya Olimpik iliyofanyika mjini Rio De Jeneiro, Brazil 2016.

Ijumaa wiki iliyopita waziri msaidizi, Bw Chris Obure aliwekwa kizimbani kujitetea kwa ufisadi wa Sh1.3 bilioni katika sakata ya Anglo-Leasing.

Kashfa hii ilipokumba serikali ya marehemu Daniel arap Moi, Bw Obure alikuwa waziri wa Fedha.

Mahakama iliamua Bw Obure pamoja na aliyekuwa katibu mkuu wizara ya Uchukuzi, Bw Sammy Kyungu na Bw Samwel Chamobo Bundotich ambaye alikuwa katibu mkuu katika wizara ya Fedha, wana kesi ya kujibu kwa ufujaji pesa za umma.

Mshtakiwa mwenzao Francis Mellops Chahonyo, aliyekuwa mkuu wa shirika la Posta Kenya (PCK) alifariki kesi ikiendelea. Hakimu mwandamizi Anne Mwangi alisema ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka ulithibitisha kuwa washtakiwa walihusika katika kashfa hiyo iliyopelekea umma kupoteza mabilioni ya pesa.

Dkt Koech alitozwa faini ya Sh19.6 milioni ama atumikie kifungo cha miaka sita gerezani kwa ubadhirifu wa pesa za umma.

Dkt Koech alihukumiwa na Hakimu Mwandamizi Bw Victor Wakumile kwa kujifaidi na pesa za umma.

Alishtakiwa kuiba Sh800,000 mnamo Agosti 17, 2006 alipokuwa mkurugenzi mkuu wa Kemri.

Aidha, alishtakiwa kuiba Sh6 milioni na pia kuiba Sh12.5 milioni kutoka kwa shirika hilo la utafiti wa matibabu.

Mnamo Juni 2020, Bw Waluke na mshirika wake wa kibiashara Bi Grace Wakhungu walipewa kifungo cha miaka 67 na 69 mtawalia kwa kuilaghai Bodi ya Nafaka na Mazao (NCPB) Sh297milioni katika kashfa ya Mahindi. Bi Juma alimtoza Waluke faini ya Sh727 milioni na Bi Wakhungu Sh707milioni kama faini.

Bw Waluke aliachiliwa kwa dhamana baada ya kukata rufaa.

Bw Soi kupitia kwa wakili wake Kimutai Bosek amewasilisha arifa ya kukata rufaa kupinga adhabu aliyopewa.

You can share this post!

Itumbi alia korti kumzuia kuhusisha mlalamishi na UDA

Kiangazi: Serikali yaahidi kununua mifugo