Habari

Ufufuzi wa kesi za 2007 wazua maswali

November 24th, 2020 3 min read

WANDERI KAMAU na VALENTINE OBARA

IDARA ya Upelelezi wa Jinai (DCI) imetangaza kufufua upya kesi za ghasia zilizotokea baada ya uchaguzi tata wa 2007, kwenye hatua ambayo imeibua msururu wa maswali kutoka kwa washirika wa Naibu Rais William Ruto.

Mkurugenzi Mkuu wa DCI, Bw George Kinoti, alisema polisi walichukua hatua hiyo baada ya kupokea malalamishi kutoka kwa baadhi ya waathiriwa wa ghasia hizo kwamba wameanza kupokea vitisho vipya kuhama maeneo wanamoishi.

Kulingana na Bw Kinoti, watu 118 walijitokeza jana kuandikisha taarifa kuhusu visa vya mauaji na kuhamishwa kwa lazima vilivyotokea kati ya 2007 na 2008.

“Tutatumia taarifa zote mlizoandikisha hapa kuunda ushahidi wetu. Tutainua Biblia mbele ya mahakama na kusema huyu ndiye aliua, huyu ndiye alichoma na huyu ndiye alimpokonya mwenzake shamba,” akasema.

Hatua hiyo imetokea wiki chache baada ya wakili Paul Gicheru kujisalimisha katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kwa mashtaka ya kushawishi mashahidi wajiondoe katika kesi iliyomwandama Naibu Rais William Ruto.

Akizungumza katika kikao cha wanahabari Jumatatu katika makao makuu ya DCI Nairobi, Bw Kinoti alisema uamuzi wa kufungua upya kesi hizo unalenga kuzuia matukio mengine kama yale yaliyoshuhudiwa 2007.

Katika ghasia hizo zilizozuka baada ya utatanishi kuhusu matokeo ya kura za urais za aliyekuwa rais Mwai Kibaki na kiongozi wa ODM Raila Odinga, watu zaidi ya 1,000 waliuliwa kinyama na maelfu wengine wakaachwa bila makao maeneo mbalimbali ya nchi.

“Tuliambiwa kuna watu wameanza kuita wenzao majina fulani tukawa na wasiwasi. Jukumu la polisi ni kuzuia uhalifu kabla utendeke. Serikali imetuagiza tusiwahi tena kurudi kukusanya miili kwa malori wala kuzika watu kwa makaburi ya halaiki,” akasema Bw Kinoti.

Kesi za Wakenya sita, wakiwemo Rais Uhuru Kenyatta na Dkt Ruto katika ICC zilisitishwa kutokana na ukosefu wa ushahidi wa kutosha.

Licha ya kusitishwa, mahakama ilisema upande wa mashtaka unaoongozwa na Bi Fatou Bensouda uko huru kuzifufua katika mahakama hiyo au humu nchini ikiwa ushahidi mpya utapatikana baadaye.

Bi Bensouda alidai ushahidi wake ulivurugwa kwa sababu ya njama iliyotekelezwa na watu waliohonga mashahidi, kuwatishia au kuwaua.

Hata hivyo, Bw Kinoti alisema Jumatatu ushahidi utakaokusanywa na polisi hautapelekwa katika mahakama yoyote ya nje bali kesi zitafunguliwa na kukamilishwa humu nchini.

“Mahakama zetu zina uwezo, na asasi zetu zote za utendaji haki zina uwezo wa kutosha kuanzia kwa upelelezi, uendeshaji mashtaka hadi maamuzi kortini,” akasema.

Kufuatia hatua hiyo, baadhi ya viongozi walikosoa vikali taarifa ya Bw Kinoti, wakiitaja kama njama ya kuzichochea jamii, hasa zinazoishi katika eneo la Bonde la Ufa.

Kupitia ujumbe alioweka kwenye katika Twitter, Seneta Kipchumba Murkomen wa Elgeyo Marakwet, aliwaomba wenyeji wa eneo hilo kutofanya lolote ambalo huenda likaibua chuki miongoni mwao na jamii nyingine.

“Taarifa ya DCI ni njama mpya ya serikali kumkabili kisiasa Naibu Rais William Ruto baada ya kushindwa na mbinu za awali. Wanataka kuzichochea jamiii, hasa katika Bonde la Ufa ili kusambaratisha uungwaji mkono wa Dkt Ruto katika eneo la Mlima Kenya. Tulisema na kuapa kutojihusisha tena kwenye vita,” akasema.

Seneta Susan Kihika wa Nakuru pia alitoa kauli kama hiyo, akidai serikali inaitumia DCI kimakusudi kuzua hali ya taharuki miongoni mwa wenyeji wa Bonde la Ufa.

Naye Seneta Ledama Ole Kina wa Narok alieleza: “Kwa hivyo hakukuwa na ushahidi wa kutosha mnamo 2007/2008? Lazima tutahadhari sana kuhusu mwelekeo tunaofuata kisiasa.”

Akasema Seneta Mutula Kilonzo Junior wa Makueni: “Lazima hatua ya kufunguliwa upya kwa kesi za baada ya uchaguzi tata wa 2007 itathminiwe upya. Wakati ilipofaa, Serikali ilibuni jopokazi ambalo halikupata ushahidi wa kumshtaki yeyote kuhusiana na ghasia hizo. Je, imebainika sasa kwamba hilo lilikuwa kosa?”

Mbunge wa Kikuyu, Kimani Ichungwa, ambaye ni mshirika wa karibu wa Dkt Ruto pia aliikosoa vikali hatua hiyo akitaka DCI isikubali kutumiwa kisiasa.

Mnamo Septemba, mbunge Ngunjiri Wambugu wa Nyeri Mjini aliandika barua kwa DCI akilalamika kuna baadhi ya watu waliokuwa wakitishia baadhi ya jamii katika eneo la Bonde la Ufa kwa misingi ya miegemeo yao kisiasa.