Makala

UFUGAJI: Chumvi na madini faafu kwa mifugo ni muhimu kwa uzalishaji maziwa

September 29th, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

ALIPOANZA ufugaji wa ng’ombe wa maziwa zaidi ya miaka saba iliyopita, Gitau Kinuthia alikuwa mateka wa chumvi na madini ya hadhi ya chini ya mifugo.

Bw Kinuthia ambaye ni mfugaji eneo la Githunguri, Kaunti ya Kiambu, alijinasua kutoka kwenye minyororo hiyo kupitia utafiti wa kina na kugundua soko limesheheni bidhaa bandia za mifugo.

Ni mmoja miongoni mwa wengi waliokadiria hasara na wengine kufikia sasa wangali mateka wa chumvi na madini bandia.

Licha ya kuwekeza maelfu ya pesa kutunza ng’ombe wake, maziwa waliyozalisha hayakugharamia mahitaji ya kuendesha shughuli hiyo.

“Nina ng’ombe 30 wa maziwa na kila mmoja alinipa lita 10 pekee kwa siku. Kumbuka mmoja anahitaji chakula kila siku, chumvi, maji na matibabu. Ilikuwa hasara tupu,” Kinuthia asema.

Isitoshe, ng’ombe alipojifungua ilikuwa vigumu kutoa utumbo unaositiri ndama kabla kuzaa.

“Chumvi na madini unayolisha ng’ombe husaidia kutoa utumbo. Bidhaa za hadhi ya chini nilizotumia hazikufanikisha hilo,” adokeza.

Kufuatia utafiti wa mfugaji huyo uliohusisha wataalamu, ulimnusuru. Kwa muda wa miaka minne mfululizo, amekuwa akitumia bidhaa halisi na zilizoidhinishwa na taasisi husika katika sekta ya kilimo na ufugaji.

“Kwa jumla sasa ninapata zaidi ya lita 700,” afichua Bw Kinuthia, akihimiza wafugaji wenza kuzingatia wanacholisha mifugo.

Ni kufuatia suala la kuwepo kwa bidhaa bandia za mifugo ambapo baadhi ya kampuni zinaonekana kuimarisha utendakazi wake.

Wiki iliyopita kampuni ya kutengeneza chumvi na madini ya mifugo cha Cooper K – Brands Ltd, CKL, ilizindua kiwanda kipya.

Ni katika hafla hiyo ambapo wakulima walishauriwa kuwa waangalifu wanaponunua bidhaa za mifugo endapo wanataka kuimarisha shughuli za ufugaji hususan mifugo wa nyama na maziwa.

Mkurugenzi mkuu wa CKL Bw Mucai Kunyiha alisema kuwepo kwa bidhaa bandia sokoni ni miongoni mwa viini vya mazao duni. Alisema changamoto hiyo itaangaziwa iwapo wakulima watakuwa makini wanaponunua madini na kushirikiana na asasi husika katika vita dhidi ya bidhaa bandia.

“Ninawashauri wawe waangalifu kwa sababu soko limesheheni bidhaa bandia hasa madini ya kuimarisha afya ya mifugo. La sivyo wataendelea kulalamikia mazao duni na ya hadhi ya chini,” akasema wakati wa uzinduzi wa kiwanda hicho eneo la Ruiru kaunti ya Kiambu.

Cooper K – Brands Ltd ni tajika nchini katika utengenezaji wa chumvi na madini ya kuimarisha mifugo wa maziwa na nyama kama Maclik Super, Maclik beef, Maclik dry cow, Maclik XP na Maclik mineral brick. Pia hutengeneza na kusambaza dawa kama triatix, grenade, nilzan, kupakula, nefluk, romectin na nyinginezo.

Kampuni hiyo pia ilizindua upakiaji na sura mpya ya bidhaa zake, katika kile kinaonekana kuzuia matapeli kuuza madini bandia kwa jina la kampuni hiyo.

Kulingana na Gitau Kinuthia, hatua hiyo itasaidia pakubwa kunusuru wakulima na ambao wamegubikwa na suala la bidhaa bandia.

Mkulima huyu anasema kila kiwanda cha kuunda bidhaa za mifugo kikiiga mkondo Cooper K – Brands Ltd, huenda kero la chumvi na madini bandia likakabidiliwa vilvyo.

“Matapeli wanaghushi bidhaa zinawiana na zile halali. Atajua baada ya kukadiria hasara. Kampuni ziweke mikakati kabambe kutambua bidhaa zake upesi na kuzifanya ngumu kughushiwa,” aelezea Bw Kinuthia.

Kulingana na Mwae Malibet, ambaye pia mfugaji wa ng’ombe wa maziwa, serikali inapaswa kuimarisha vita dhidi ya bidhaa bandia. Anasema operesheni isiwe ya muda mfupi tu kisha inasahaulika.

“Wakulima ndio wanaathirika zaidi na bidhaa bandia. Ng’ombe ukimpa chumvi au madini bandia, bila shaka mazao yatakuwa duni,” asema Bw Malibet. Yote tisa, la kumi kitendawili hiki kitateguliwa wakulima wakishirikiana kwa karibu na asasi husika.