Makala

UFUGAJI KIBIASHARA: Amepiga hatua kuu maishani kwa ufugaji wa ng'ombe wa maziwa

August 22nd, 2019 3 min read

Na SAMUEL BAYA

KIJIJI cha Solai katika Kaunti ya Nakuru kiligusa vichwa vya habari mwaka 2018 wakati maji yalipasua kuta za bwawa la Patel na kuangamiza zaidi ya watu 40.

Hapo ilikuwa ni awali ila kwa sasa, na hasa baada ya mkasa huo, maisha ya wakazi yamekuwa yakiendelea polepole wakijaribu kusahau kilichotukia.

Baada ya dhiki ni faraja na kijiji hiki sasa kimeshuhudia miradi mbalimbali ya kilimo ambayo imeshika kasi huku wakazi wakiwa na lengo la kujikwamua kiuchumi.

Naam, hivyo ukipita mbele kidogo ya kituo hiki cha biashara ukielekea eneo la Kabazi, utakutana na Bw Edward Kiprotich. Yeye ni mfugaji wa ng’ombe wa maziwa, biashara ambayo inamsaidia kupambana na maisha.

“Nilikuja hapa mwaka wa 1997 ila nikaanza shughuli za ufugaji mwaka wa 2,000 wakati nilipoleta ng’ombe wa babangu mzazi nikiwa ninamchungia. Baadaye babangu aliuza ng’ombe wote kisha tukagawa, na leo hii ninafanya kazi hii kwa ng’ombe wangu wote,” akasema Bw Kiprotich.

Bw Kiprotich kwa sasa anamiliki ngombe sita katika kipande chake cha ekari moja na nusu cha ardhi katika kijiji hicho cha Solai.

Ingawa amepanda nyasi katika baadhi ya sehemu ya ardhi yake, bado nyasi hizo ni chache kulingana na wingi wa mifugo wake hivyo kulazimika kununua chakula cha mifugo ambacho alidai katik mahojiano kwamba ni ghali mno.

Tulipokutana naye, Bw Kiprotich alikuwa katika mkutano wa maendeleo kijijini lakini ari ya kutaka kutuelezea kuhusu biashara yake ilimfanya kuja pindi tu alipofahamishwa kwamba ukumbi wa ‘Akilimali’ ulikuwa umefika bomani mwake.

“Nina ng’ombe wanane, ndama sita na nzao mbili. Mimi huwa ninauza lita 30 kwa siku kwa sababu nyakati za asubuhi, huwa ninakamua lita 15 na jioni pia hukamua lita zengine 15,” akasema Bw Kiprotich.

Anasema kuwa lita moja inauzwa kwa Sh30 hivyo basi yeye kupata kipato cha Sh900 kwa siku. Hata hivyo mfugaji huyu alisema kuwa kiwango hicho cha bei ya maziwa bado kiko chini na hakimfaidi sana mkulima.

“Shida moja ni bei, au mahali ambapo tunauzia. Mara nyengine tunalazimika kuuza kwa reja reja kwa sababu ile gari ya KCC, huwa inakuja leo unasubiri hata siku mbili gari haifiki tena. Hiyo inamaana kwamba lazima sasa urudi tena kwa kijiji uuze kwa rejareja,” akasema Bw Kiprotich.

Aidha, aliongeza kwamba mara nyingi mojawapo ya changamoto kubwa ni bei ya chakula cha mifugo wake ambayo ni ghali sana.

“Huyu ng’ombe ninamlisha dairy meal kwa afya bora ili kuifanya iweze kutoa maziwa mengi,” akasema.

Kilo hamsini za dairy meal huuzwa kati ya Sh1,800 na Sh2,000 na mfugaji huyu alisema kuwa kila mwezi yeye hununua kilo 100 kwa mwezi. Alisema kuwa bei hiyo iko juu sana na ina gharama kuu kw mfugaji.

“Hii biashara ya ufugaji imenisaidia kusukuma maisha yangu. Imenisaidi kulipa karo za masomo kwa watoto wangu. Mara nyengine kukiwa na shida hata nyumbani, ninachukua mnyama mmoja na kuuza ili kujisaidia,” akasema Bw Kiprotich.

Kaunti yatakiwa isaidie

Anaomba serikali ya kaunti kuangalia hiyo sekta ya ufugaji na kuona ni kwa njia gani ambayo watafanya kuimarisha sekta hiyo wanaoitegemea kujikimu.

“Tunaomba serikali iweze kutoa mikopo kwa wakulima na wafugaji kama sisi. Vile vile tunaomba serikali itusaidie kwa kutupatia mbegu za ng’ombe kwa sababu kwa sasa kupandisha ng’ombe inagharimu kiasi cha Sh2,000 na hiyo ni ghali sana kwa mfugaji,” akasema Bw Kiprotich.

Anasema kuwa kitengo cha mifugo katika kaunti kinafaa pia kuweka pesa kunyunyizia dawa katika maegesho ya mifugo ili waweze kupeleka mifugo wao kuwaogesha kama njia ya kuwaepusha gharama za kuwatibu.

“Hili egesho letu la Solai halina dawa ya kuwezea kutibu maji nasi kupeleka mifugo yetu. Hiyo itatusaidia sisi kuepukana na gharama za kununua dawa za mifugo,” akasema mfugaji huyo.

Bw Kiprotich ambaye ni baba wa watoto sita anasema kuwa kwa siku yeye huuza maziwa kiasi cha Sh2,000 hivyo basi kwa mwezi, huwa anapata pesa kiasi cha Sh50,000.

“Tulikuwa na chama cha ushirika hapa Solai lakini huduma zake zimekuwa duni na mara kwa mara hakifanyi kazi kama tulivyokuwa tukitarajia. Ni kwa maana hiyo basi kuna haja ya kuhakikisha kwamba serikali inaboresha sekta hii ya maziwa ili tufaidi sisi kama wakulima na wafugaji,” akasema mfugaji huyo.