Makala

UFUGAJI: Kipimo cha ratio, virutubisho na madini ni vigezo muhimu kuzingatiwa kufanikisha ufugaji ng’ombe wa maziwa

October 9th, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

ALIPOAMUA shughuli ya ufugaji wa ng’ombe hasa wa maziwa 2018, Mhandisi Joseph Oloo alihangaishwa na suala la lishe.

Mkulima huyu anayeendeshea gange hiyo kaunti ya Homa Bay, alilazimika kuendea chakula cha mifugo Kitale, eneo lililoko kaunti ya Trans Nzoia.

“Gharama ya kununua na kusafirisha ilikuwa ghali, na nilikuwa nikikadiria hasara tu,” asema Bw Oloo. Alikuwa akiendea matawi na majani ya mahindi, kwani Trans Nzoia inafahamika katika uzalishaji wa mahindi.

Isitoshe, mfugaji huyu pia alikuwa akinunulia ng’ombe wake chakula maalumu cha mifugo, almaarufu ‘dairy feeds’. Hata hivyo, anasema nyingi ya chakula hicho huwa hakijaafikia vigezo ya madini yafaayo kwa mifugo.

Oloo anasema kiwango cha maziwa alichopata ni chini ya lita saba kwa siku kutoka kwa ng’ombe mmoja. Mradi wake huo na ambao ni wa kipekee Homa Bay ulimgharimu mamilioni ya pesa kuwekeza.

“Nilijipata nikigharamia takriban kila kitu kilichohitajika badala ya ng’ombe wenye kujikimu na kunipa faida,” aeleza. Mfugaji huyu hakuwa na budi ila kutafuta njia mbadala kupunguza gharama ya chakula, na ambayo kwa wengi imekuwa kikwazo kikuu kwa sababu ya ongezeko la gharama.

Alichukua hatua ya busara kufanya utafiti katika mitandao pamoja na kuzuru wafugaji waliobobea, madhumuni yakiwa kutibu kidonda kilichouguza na kumsababishia hasara bin hasara. Aidha, aliafikia ili kupunguza gharama ni heri kujiundia chakula na ambacho ana uhakika wa uhalisia wake.

Kwa kuwa amejaaliwa na shamba kubwa, Oloo anasema alianza kujikuzia nyasi za mifugo kama vile boma rhodes, brachiria na napier. Vilevile hupanda mahindi.

“Nyasi hizo na mahindi, ndizo hutumia kutengeneza silage na hay,” asema.

Ni kutokana na hatua hiyo, ng’ombe wa mkulima huyo sasa wanazalisha zaidi ya lita 14, mmoja kwa siku. Kwa kuwa Homa Bay ni eneo linalojishughulisha na uvuvi, maziwa humo ni mithili ya dhahabu. Kwa mujibu wa Bw Oloo lita moja haipungui Sh60.

Kulingana na wataalamu, fanaka katika ufugaji wa ng’ombe wa maziwa inategemea hadhi ya chakula; virutubisho na madini yaliyomo.

Bw John Momanyi, kutoka Sigma Feeds – kampuni inayotengeneza chakula cha mifugo, anaiambia Taifa Leo kuwa cha muhimu zaidi ni lishe inavyochanganywa na madini. “Kipimo (ratio), unavyochanganya chakula maalumu – dairy meal, silage, hay na molasses, ni suala muhimu sana katika kufanikisha ufugaji wa mifugo wa maziwa na nyama,” Momanyi asisitiza.

Madini yafaayo

Anaongeza kusema kwamba chakula maalumu kinapaswa kuwa chenye virutubisho vya kutosha na madini yafaayo.

Anahimiza molasses isikose kwenye mlo kwa sababu huwapa ng’ombe motisha kunywa maji mengi, ambayo ni kiungo muhimu katika uundaji wa maziwa.

Ni muhimu kukumbusha mfugaji kuwa madini na chumvi hupewa ng’ombe kulingana na umri. Katika siku za kwanza, ndama anapaswa kunyweshwa maziwa kati ya lita 4 – 6 kwa siku.

Akiwa na umri mdogo, maziwa husaidia katika utengenezaji wa tumbo nne. Anapaswa kupewa chumvi, hasa Maclik Plus, baada ya kuhitimu kilo 350.

Ng’ombe, wakati wa ujauzito hasa miezi miwili kabla ya kujifungua, apewe Maclik dry cow. Akijifungua, yaani anayekamwa, hupewa Maclik Super.