Makala

UFUGAJI: Mboga za kijani ni muhimu katika kuwapa kuku madini ya Vitamini

October 4th, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

UKIZURU yumkini katika kila boma, hasa mashambani kuna mifugo na ndege wa nyumbani ambao hutakosa kuwaona. Nao ni ng’ombe, mbuzi, kondoo na kuku.

Wanafugwa kwa minajili ya nyama na mayai – kuku, pamoja na kuimarisha kiwango cha mapato.

Kwa kuwa ni rahisi kufuga, kuku ndio wanaongoza kwa idadi ya wanaowafuga. Nyuni hawa wa nyumbani wanaorodheshwa miongoni mwa nyama nyeupe na zisizo na mafuta hatari aina ya Cholesterol.

Mbali na kusheheni mashambani, baadhi ya wanaoishi mijini pia wamekumbatia ufugaji wake.

Ili kufanikisha ufugaji wa kuku masuala kadha wa kadha yanapaswa kuzingatiwa. Lishe bora na kamilifu, inaongoza katika vigezo faafu ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa maji safi.

Fauka ya hayo, mazingira yanapaswa kuwa salama na la mno kuhakikisha ndege hao wanapata matibabu ulegevu unapobainika.

Katika suala la chakula, ili kuimarisha siha ya kuku mfugaji anapaswa kuzingatia mlo kamilifu. Okuta Ngura, mtaalamu wa masuala ya mifugo na aliyebobea katika ufugaji wa kuku anasema cha muhimu kwa ndege hao wa nyumbani ni mkusanyiko wa vyakula mbalimbali, hususan vyenye virutubisho au virutubishi vinavyotakikana.

Kuku wanafugwa kwa minajili ya nyama na mayai – mazao yaliyosheheni Protini, na wataalamu wanahimiza chakulq chake kiwe na zaidi ya asilimia 18 ya Protini.

“Madini ya Protini ni muhimu katika uundaji wa nyama na mayai, hivyo basi kuku alishwe chakula chenye Protini kwa wingi,” asema Bw Ngura.

Katika orodha hiyo, Wanga, ni muhimu sana katika kuupa mwili nguvu. Ngura anasema kuku hapaswi kuikosa kwa kuwa humuwezesha kula bila matatizo, kucheza pamoja na kumpa nguvu za kutaga.

Sawa na binadamu, kuku wanahitaji Vitamini ili kuwaepushia maradhi ibuka. Hesbon Asava ambaye ni mfugaji wa kuku wa kienyeji kaunti ya Vihiga anasema hupiga jeki ndege wake kwa Vitamini kupitia mboga.

Katika shamba la mkulima huyo ametenga sehemu kukuza sukuma wiki na spinachi. “Huwakatakatia mboga ninazolima mwenyewe,” asema Bw Asava.

Kuyasaga mahindi

Asava hujiundia chakula cha kuku ambapo husaga mahindi anayokuza katika shamba lake na kuyachanganya na punje aina ya pellets.

Bw Okuta Ngura anahimiza wakulima kukumbatia mkondo wa kupanda mboga ili kuimarisha afya ya kuku kwa Vitamini.

“Vitamini inatoka kwa matunda, mboga na majani,” asema mtaalamu huyo.

Kigezo kingine muhimu katika lishe ni Mafuta, ambayo huupa mwili wa kuku joto hususan wakati wa kuatamia na kuangua mayai.

Ili kukwepa kero la kuwepo kwa chakula bandia na cha hadhi ya chini cha mifugo, Bw Ngura anahimiza wakulima kujiundia lishe. “Kingi cha chakula masokoni hakijaafikia vigezo faafu na ili kuepuka kero lake, wakulima wajiundia chao ikiwa wana malighafi,” ashauri.

Yote tisa, la kumi kuku wanyweshwe maji safi kwa wingi. Mazingira wanayoishi yawe safi na yanayoruhusu Oxijeni kuingia.

Mfugaji anashauriwa kuhakikisha kuku wanapata matibabu na chanjo. Baadhi ya wakulima wanaothamini mfumo asilia, huwapa maji yaliyochanganywa na mmea aina ya aloe vera na pilipili ili kudhibiti ueneaji wa maradhi.