Makala

UFUGAJI: Mbuzi wa maziwa

July 23rd, 2019 3 min read

Na SAMMY WAWERU

WATAALAMU wa masuala ya afya wanasema unywaji wa maziwa ya mbuzi ni jambo wanalotilia maanani kwa wagonjwa kwa sababu ya manufaa yake kisiha.

Kando na kusheheni Protini, maziwa ya mbuzi yanasemekana kuwa rahisi kusagwa kwenye viungo vya mwili yanaponywewa.

Leah Gitahi, muuguzi na mtaalamu wa afya Naivasha anasema maziwa haya yana Calcium ambayo ni muhimu kwa mwili wa binadamu.

“Maziwa ya mbuzi husaidia kupunguza kiwango cha lehemu (Cholesterol) mwilini. Yanasaidia katika ukuaji wa ngozi hasa kwa watoto na kuilainisha,” anafafanua Bi Gitahi.

Cholesterol ni chembechembe inayopatikana kwenye damu, na yenye mafuta.

Kiwango chake kikizidi kinachohitajika, kwa mujibu wa matabibu husababisha ugonjwa wa moyo. Aidha, mafuta mengi huziba mishipa ya kueneza damu.

Mtaalamu Leah Gitahi anaendelea kueleza kuwa kiwango cha Cholesterol katika maziwa ya mbuzi ni cha chini kikilinganishwa na ya ng’ombe, hivyo basi ni bora kwa wenye shida ya msukumo wa damu (BP).

“Kiwango chake cha sukari ni cha chini, wenye matatizo ya ugonjwa wa Kisukari wanahimizwa kuyatumia,” anasema.

Ni muhimu kutaja kuwa maziwa haya yamesheheni Vitamini B1, ambayo husaidia kukabiliana na mzongo wa mawazo na shida za kusokotwa na tumbo.

Licha ya manufaa yake chungu nzima kiafya, wataalamu wanasema yameadimika kwa ajili ya wakulima wachache wanaofuga mbuzi.

“Mahitaji yake ni mengi lakini inaonekana wafugaji wa wale wa maziwa ni wachache,” anaeleza Leah Gitahi, kauli inayotiliwa mkazo na James Mwangi ambaye ni mtaalamu na muuguzi mjini Murang’a.

Bw Joseph Mathenge ni mfugaji wa mbuzi wa maziwa na anasema yeye ni miongoni mwa wakulima wachache wanaofuga wanyama hawa.

Kulingana na mfugaji huyu ni kwamba ufugaji wa mbuzi ni rahisi mno ukilinganishwa na ng’ombe.

Ni shughuli anayoifanyia eneo la mjini, mtaani Mwihoko, Kaunti ya Kiambu, katika ploti yake yenye ukubwa wa nusu ekari na ambayo amejenga jumba la kuishi.

Zizi la mifugo hii ina urefu wa futi 30, upana futi nane na futi 13.7 kuenda juu.

Aidha, kimeinuliwa futi 3 kutoka ardhini ili kuzuia viroboto na wadudu hatari kuingia.

Katika kipimo cha kuenda juu, ametenga nafasi ya futi 4 ambapo ameunda stoo ya kuhifadhi lishe.

Pembezoni, ana kingine ambacho ni cha wanambuzi.

“Maeneo ya mjini, kuna upungufu wa ardhi na muundo huo utamuwezesha mwenye ari ya mbuzi wa maziwa kuwafuga bila mahangaiko,” anasema Bw Mathenge.

Kwa sasa ana jumla ya mbuzi 17, saba wakizalisha maziwa.

Lita moja ya maziwa ya mbuzi inagharimu Sh200, wateja wa mfugaji huyu wakiwa vituo vya afya eneo la Mwihoko, Ruiru na Juja.

“Wengi wa wateja wangu ni wenye watoto na vituo vya afya, hununua kwa kipimo cha robo lita ninachouzwa Sh50,” anadokeza Mathenge.

Mfugaji huyu anakiri kwamba kuna upungufu wa maziwa ya mbuzi nchini kwa sababu ya oda nyingi anazopokea. Anasema imekuwa vigumu kuafikia mahitaji ya wateja wote kikamilifu, ikizingatiwa kuwa sehemu anayowafugia ni haba.

Alianza ufugaji huu 2011.

“Tangu nianze, nimeuza zaidi ya mbuzi 200 kwa ajili ya upungufu wa shamba,” anafichua.

Hufuga mbuzi aina ya Alphine, wenye asili ya Ujerumani na Afrika.

La kutia moyo katika ufugaji wa mbuzi hao ni kwamba huwahudumia muda wa saa mbili pekee.

Bw Mathenge anasema anaporauka asubuhi, hung’arisha kwa kufagia makazi yao, vifaa vya chakula na maji.

Huwatilia mlo kisha anawakama, ambapo mmoja huzalisha kati ya lita 3 hadi 4 kwa siku.

Ufugaji usio na kikwazo

Huwapa nyasi zilizokauka maarufu kama hay, Boma Rhodes, Lucerne na chakula maalum cha mifugo.

“Chakula chake kiwe kamilifu, na kishamiri Protini pamoja na kunyweshwa maji kwa wingi,” anashauri Bw Simon Wagura,

Ufugaji wa mbuzi hauna kikwazo kwani si lazima mkulima awe na kibali kutoka kwa halmashauri ya kitaifa ya mazingira, Nema. Wanaoishi kaunti ya Nairobi hata hivyo wanahimizwa kuhusisha Nema ili kutathminiwa eneo wanalopania kuwafuga.

Bw Joseph Mathenge anasema uhaba wa maziwa ya mbuzi nchini utatatuliwa iwapo wakulima watakumbatia mkondo wa ufugaji wa mijini. Mbali na manufaa kiafya, maziwa yake yanaletea mfugaji mapato. Mbuzi pia huchinjwa, ambapo nyama yake ina ladha tamu.