Makala

UFUGAJI: Ufugaji vipepeo ulivyowawezesha wanawake kutunza Arabuko Sokoke

March 12th, 2020 3 min read

BRIAN OKINDA na CHARLES WASONGA

BI Jamila Rashid, mama wa watoto watatu, anayeishi katika kijiji cha Mida, tarafa ya Gede, Kaunti ya Kilifi amekuwa akifanya biashara ya kuuza kuni na makaa katika msitu mkubwa wa Arabuko-Sokoke.

Mama huyo na wenzake kutoka kijiji hicho wamekuwa wakishinda kwa saa nyingi msituni wakisaka vipande vya kuni na kuchoma makaa, shughuli ambayo mara kadhaa iliwafanya kukosana na wahifadhi misitu na maafisa kutoka Shirika la Huduma ya Misitu (KWS).

“Sifahamu njia nyingine ya kupata pesa na ndio maana mimi hutegemea biashara ya makaa. Lakini mara nyingi kazi hii hutugonganisha na maafisa wa misitu na ndovu ambao huishi msituni,” anasema Rehema Hassan ambaye huishi karibu na msitu huo.

Lakini sasa biashara ya vipepeo imegeuka kuwa kitega uchumi muhimu kwa akina mama hawa.

Msitu wa Arabuko- Sokoke ni hifadhi ya takriban jamii 260 za vipepeo, kulingana na Afisa wa Shirika la Huduma za Misitu (KFS) Elvis Fondo, ambaye ni afisa msimamizi wa msitu huo.

Anaongeza kuwa takriban asilimia 30 ya aina ya vipepeo wanaopatikana nchini wanaishi katika msitu huu. “Ufugaji wa vipepeo ni njia mbadala ya uchumaji mapato kwa watu wanaoishi karibu na msitu kwani kazi hii haihitaji mtaji mkubwa. Pia vifaa hitajika ni vichache,” anasema Bw Fondo.

Ili kufuga vipepeo, kwanza wale wa kike hunaswa kwa kutumia mitego iliyowekewa chambo cha kutoa harufu ya kuwavutia. Vipepeo hungia ndani ya mtego, ambao huwa umetengenezwa kwa umbo la uteo, na hukaa mle hadi wanawake hao watakapokuja na kuwakusanya.

Nyakati zingine wanawake hawa huwakamata vipepeo hao kwa kutumia nyavu maalum, haswa wanapopaa.

Lakini mbinu hii huwa inachosha kwa sababu wao hulazimika kuwafukuza wadadu hao huku na kule katika jitihada za kuwanasa kwa nyavu hizo.

Bi Rehema, na wenzake, huwapeleka vipepeo hawa nyumbani ambako wamejenga vibanda maalum vya kuwafugia. “Ndani ya vibanda hivyo vya ukubwa mbalimbali, hutiwa majani ya mimea na matundu yenye harufu nzuri kama vile maembe mabivu,” anasema Bi Rehema.

Vipepeo hawa hula majani hayo ndani ya vibanda hivyo hadi watakapoanza kutaga mayai. Mayai haya huzalisha vipepeo wengine. Vibanda hivi kutengenezwa kwa mbao na nyavu zitakazohakikisha wadudu hao wanapata hewa safi na huku wakisalia mle ndani.

Kila mmoja wa wanawake hawa wafugaji vipepeo amejenga vibanda hivi maalum nyumbani; huku baadhi yao wakiwa na kati ya viwili na 10.

Baada ya vipepeo hao kutaga mayai, wanawake hawa hushauriwa kuwaachilia warejee msituni katika mazingira asili ili waendelee kuzaana.

Vipepeo wanaweza kutaga kati ya mayai 1,000 na 2,000 wawapo hai kwa kipindi kisichozidi wiki mbili, kwa mujibu wataalamu wa wadudu. Baada ya mayai kuanguliwa, vipepeo wadogo hupelekwa katika kituo cha mradi wa Kipepeo Butterfly Project Centre ambacho kinasimamiwa na Shirika la East Afrina Natural History Society na Makavazi ya Kitaifa (NMK).

Ni katika kituo hiki ambako akina mama hawa huuza vipepeo. Aidha, ni katika kituo hiki ambako vipepeo hawa huainishwa katika gredi mbalimbali kulingana na hitaji la soko ya kimataifa.

Gredi hizo hutegemea aina ya vipepeo, na iwapo wameathiriwa na magonjwa yanayojulikana kwa kimombo kama Ophryocystis, Elektroscirrha na Tachinid fly. Mambo kama haya na mengine huzingatiwa wakati wa ukadiriaji wa bei ya vipepeo hawa ambayo ni kati ya Sh25 hadi Sh70 kwa kila mmoja.

Baada ya kuwanunua vipepeo, wasimamizi wa Kipepeo Butterfly Project Centre huwauza katika mataifa ya Uropa, Amerika, Uturuki miongoni mwa mataifa mengine.

Nyakati nyingine vipepeo hawa wadogo huuzwa katika taasisi kama Makavazi ya Kitaifa, ambayo huendesha maonyesha ya vipepeo kila mara.

Charo Ngumbao, ambaye ni afisa mkuu wa Kipepeo Butterfly Project Centre anasema kuwa aina ya vipepeo ambao wanahitajika kwa wingi katika masoko ya kimataifa ni wale wanaojulikana kama Papilio Swallowtails na Charaxes.

Afisa huyu anasema kwamba kwa wastani wanawake wenye bidii wanaweza kutia kibindoni Sh10,000 kila wiki kutokana na wadudu wao.

Mmoja wao ni Mama Fatuma Hamisi, mkazi wa eneo hilo anasema kazi hiyo imemwezesha kugharimia mahitaji ya familia yake, haswa karo ya watoto.