UFUGAJI: Ufugaji wa ndege aina ainati unavyompa kipato

UFUGAJI: Ufugaji wa ndege aina ainati unavyompa kipato

NA PETER CHANGTOEK

AMEKUWA akiwafuga ndege aina mbalimbali kwa muda wa miaka mitano.

Vincent Muli, 30, anasema kuwa, ufugaji huo umemfaidi na umekuwa kitegea-uchumi kwake.

Amekuwa akiendeleza shughuli hiyo ya ufugaji katika eneo la Kaani, takribani kilomita 10 kutoka mjini Machakos, karibu na barabara ya Machakos-Kitui, Kaunti ya Machakos.Mfugaji huyo amekuwa akiwafuga ndege kama vile mabatabukini, mabatamzinga, kanga, miongoni mwa spishi nyinginezo.

“Nina kanga 45 kwa jumla; lavender 6, royal purple 4, white chested 6, back dotted 4 na wengine wa rangi nyeupe, mabatabukini karibu 10, mabatamzinga 8, American fantails 8, capuchin 2, silky bantam 6, polished bantam 4. Wale wengine ni njiwa wa kawaida ambao ni 6. Nina kuku wa Kenbro ambao ni 20 na kienyeji 15, ambao huwatumia kutotoa mayai,” aeleza Muli.

Anasema kuwa mayai ya kanga na mabatamzinga yanaweza kuanguliwa na kuku kwa sababu yakiwekwa kwa kitotozi ni machache tu ambayo yataanguliwa.Anaongeza kuwa hupata mayai 15 kwa siku, ambapo kwa wiki hupata 105.

“Kwa kitotozi nina mayai 210 na ninataka niweke 500. Ifikapo Januari, nitakuwa na vifaranga wasiopungua 300 wa kanga. Nimetotoa 20 ya silky, kanga walioanguliwa ni 25, na kuku wameatamia mayai 40,” aongeza mfugaji huyo.

Anaongeza kwamba, mwaka uliopita, alikuwa ametotoa mayai 200, na akawauza vifaranga wote na akalazimika kuwanunua wengine kutoka kwa rafiki yake ili awauzie wateja wake.

“Nimewauzia watu wengi sana Meru, Embu, Kisumu, Bungoma, Mombasa, Kilifi,” asema Muli, akiongeza kuwa, hupata wateja wengi sana kutoka Nairobi.

Aidha, anadokeza kuwa, mwaka huu 2022, aliwanunua kadhaa kutoka kwa rafiki yake ambaye alikuwa akimwuzia kwa Sh1,200 kwa wale waliokomaa na Sh800 kwa wale ambao hawajakomaa.

Vincent Muli akionyesha baadhi ya ndege anaowafuga katika eneo la Kaani, Kaunti ya Machakos. PICHA | PETER CHANGTOEK

Wale aliokuwa amewanunua kwa Sh800 alikuwa akiwauza kwa Sh1,500 na wale aliowanunua kwa Sh1,200 alikuwa akiwauza kwa Sh2,000.

“Nauza kanga wenye umri wa mwezi mmoja kwa Sh800, batabukini mwenye umri wa mwezi mmoja kwa Sh1,000, batamzinga mwenye umri wa mwezi mmoja ni Sh900. Waliokomaa ni Sh2,000, wale weupe kabisa ni Sh3,000, lavender Sh3,000, batabukini ni Sh3,500, batamzinga ni Sh3,500. Wakati mwingine ukinunua wa kiume na wa kike kwa wakati mmoja, hupunguza bei kwa Sh500,” asema.

Alijitosa kwa ufugaji huo kwa kuwanunua vifaranga na wakaja kuongezeka. Alianza kwa kuwafuga kanga pekee, ambapo kwa wakati huo, vifaranga walikuwa wakiuzwa kwa Sh400.

“Nikachukua 10 na waliokomaa walikuwa wakiuzwa Sh1,500. Niliwanunua 8 waliokomaa,” asema, akiongeza kuwa, aliwanunua kutoka kwa rafiki yake.

Hutumia lishe anazozinunua madukani kuwalisha ndege wake na huwalisha mara mbili kwa wiki. Pia, huwaruhusu watoke ndani wajitafutie lishe za ziada.Hata hivyo, anasema kuwa, kuna changamoto kadhaa ambazo amekumbana nazo, kama vile bei za juu za lishe, na baadhi ya magonjwa, ambapo baadhi hutibiwa na mengine ni sugu.

Muli pia huyauza mayai ya ndege aina ya ‘silk’ na ‘polish’ kwa Sh200 kila moja. Pia, huliuza yai la batamzinga kwa Sh150, la batabukini kwa Sh200 na la kanga kwa Sh150.

“Mayai ya kanga huchukua muda wa siku 28 kuanguliwa, ya kuku ni siku 21, ya ‘silk’ ni siku 19-20, ya batabukini ni siku 28 na batamzinga siku 28,” afichua mkulima huyo, ambaye huwauza kuku wa Kenbro kwa Sh750 na wa kienyeji kwa Sh650.

Anawashauri wakulima kujaribu shughuli hii kwa sababu ina faida.

“Ili kufanikiwa, wanafaa wawe na vifaranga wengi ili wawauze na kupata faida kubwa. Kuwafuga tu wale waliokomaa hakuleti faida kwa sababu utapata tu pesa kidogo zaidi ya zile ulizotumia kuwanunua. Mipango yangu ni kuhakikisha kuwa nina spishi zote na kuwa na shamba la kutoa mafunzo, ambapo watu watakuwa wakinitembelea na kufunzwa ili waende na waanzishe ufugaji,” asema.

Mfugaji huyo anadokeza kuwa, wateja wakimpa oda ya nyama za ndege hao, huwachinjia.

“Mwaka uliopita niliwachinjia mabatamzinga Waitaliano kule Westland,” asema, akiongeza kuwa, wengi hupenda nyama ya mabatamzinga.

Hupata wateja kutoka mitandaoni, ambapo amejiunga na vikundi mbalimbali vinavyojihusisha na ufugaji wa ndege mbalimbali. Aidha, anasema hupata wateja kwa jukwaa la Jiji.co.ke na wale wanaoelekezwa kwake.

  • Tags

You can share this post!

ZARAA: Mwalimu anayejituma ili kufufua kilimo cha kahawa

Vita baridi ndani ya Kenya Kwanza

T L