Makala

UFUGAJI WA FAIDA: Mbuzi kwake kimbilio akitaja bei nzuri ya maziwa, gharama nafuu

October 24th, 2019 3 min read

Na RICHARD MAOSI

KAUNTI ndogo ya Rongai inayopatikana viungani mwa mji wa Nakuru, ni eneo linalopokea mvua kidogo kila mwaka, jambo linalowapatia wakulima wengi changamoto wakati wa kutafutia mifugo yao chakula na maji.

Wakulima wengi hapa ni wafugaji wa ng’ombe na pia hukuza mimea kama vile mahindi, maharagwe, parachichi na matikiti maji, ila miaka ya hivi karibuni mabadiliko ya hali ya anga yamefanya wao kutalii nyanja nyingine ya ukulima.

Mmoja wao ni Patrick Ndung’u Chege anayewafuga mbuzi wa maziwa badala ya ng’ombe wa kawaida, akisema kuwa gharama yake ni nafuu, na ni kilimo kinachoweza kumpatia mkulima tija.

Tulimkuta katika kipande chake cha ardhi akiendelea kuwakama mbuzi wake, kabla ya kusafirisha maziwa yake sokoni ambayo anasema yanawaniwa na wanunuzi kutoka maeneo yanayozunguka Nakuru.

Aidha anasema kilichomsukuma kuanzisha mradi huu ni hitaji la kujiongezea kipato, mbali na kushirikiana na wakulima wengine wenye nia ya kujiinua kimapato kutoka Rongai.

Patrick anasema kwa siku moja anaweza kupata lita nane ya maziwa kutoka kwa mbuzi watatu, ambapo lita moja sokoni huuzwa kwa 125, mara tatu bei ya maziwa kutoka kwa ng’ombe.

Hii inamaanisha kuwa kwa wiki moja anaweza kutengeneza baina ya 7,000-8,000 kutoka kwa mbuzi watatu, ambapo humtengenezea zaidi ya 30,000 kwa mwezi ikizingatiwa kuwa yeye pia ni mkulima wa mahindi.

Kipato hiki kimemsaidia kuwasomesha watoto na kujinunulia kipande cha ardhi, na malengo yake ni kupanua uwanda wa ufugaji kwa sababu baada ya muda mfupi amekubali mbuzi ni bora kuliko ng’ombe.

“Haja yangu kubwa kuanzisha mradi huu ni kupatia familia yangu maziwa ya hali ya juu, lakini sasa mradi wenyewe umekuwa ni kitega uchumi,” Patrick akasema.

Kwa mtaji kidogo alianza na mbuzi mmoja, kisha wakazaana na sasa anafuga spishi mbalimbali ambazo ni Saanen na Alpine ambao huvumilia hali ngumu ya mazingira na pia wamezoea kula kiwango kidogo cha majani yanayoweza kupatikana.

Hata hivyo, Patrick anasema kuna baadhi ya mambo ambayo mkulima anapaswa kuzingatia wakati wa kufuga mbuzi wake. Kwanza ahakikishe kuwa kibanda cha mbuzi kimeinuliwa kidogo kutoka ardhini mita mbili hivi ili kuhakikisha kuwa viroboto na kupe hawayashambulii makazi yao.

Anasema hii itapunguza gharama ya kuwatibu kwa kupulizia dawa mara kwa mara, jambo ambalo linaweza kuzuilika kutokana na ufugaji sahihi.

Patrick huwakamua mbuzi watatu kila siku, na anaweza kupata lita nane au zaidi, jambo linalomfanya kuungama kuwa amejitengenezea nafasi ya ajira badala ya kutegemea vibarua huko nje visivyoweza kutabirika.

Anawashauri wakulima kujikita katika kilimo biashara ili waweze kupata soko kwa bidhaa zao wanazozalisha kwa wanunuzi. Anasema katika mataifa yaliyoendelea ufugaji wa mbuzi umeleta viwanda vingi vinavyojihusisha na maziwa ya mbuzi.

“Hiki ni kilimo kinachoweza kuendeshwa na watu wanaomiliki mashamba na wale wasiokuwa na mashamba mijini, muradi waelewe kanuni zinazohitajika kustawisha mradi wenyewe,” akasema.

Mbuzi anahitaji nafasi ndogo wakati wa kumfuga ambayo ni mita nne mraba na wala hakuna mtu yeyote ambaye anaweza kulalamika kuwa hawezi kupata nafasi kama hiyo, kuendeshea mradi wake.

Miongoni mwa mbuzi wake kuna wale wanaokamuliwa, wengine ni wajawazito na kuna mbuzi wadogo waliozaliwa hivi karibuni ili kuendeleza kizazi cha mifugo hiyo.

Aidha, mbuzi wanaweza kutumia majani ya kawaida kama vile magugu na miche na pia wao hunywa kiwango kidogo cha maji.

Wao pia hawahitaji matibabu ya kila wakati kwa sababu ni nadra sana kutatizwa na magonjwa.

“Katika maeneo ambayo maziwa ya mbuzi yamekuwa yakitegemewa wengi wanaoyahitaji huyatumia kwa sababu za kiafya na bei yake huwa kati ya 100-200 kwa lita,” akasema Patrick.

Ambapo kimatibabu watoto wanaokuwa na udhaifu wa kimwili na matatizo ya kusimama au kutembea wanashauriwa kuyatumia maziwa haya, ambayo huwa na virutubishi muhimu vya calcium, magnesium na patassium.

Vilevile maziwa ya mbuzi husaidia watoto kukua haraka na kuwapatia uwezo wa kukomaa ubongo mapema ili wasipate changamoto wakati wa kuzungumza.

Patrick anasema amefaidika na ufugaji wa mbuzi kwa sababu anapatikana karibu na mji wa Nakuru na Eldoret, anasema wakulima wengi huanzisha mradi wenyewe bila kufahamu soko lake.