Ufugaji wa kuku riziki tosha kwake

Ufugaji wa kuku riziki tosha kwake

NA WACHIRA ELISHAPHAN

VIJANA wengi wanapomaliza masomo yao, hujiingiza katika anasa na matumizi ya mihadarati ambayo hatimaye huwadhuru wanapokosa njia za kujikimu kimaisha,ila kijana Ibrahim Raphael hakubaki kujikunyata nyumbani kwa sababu ya kukosa kazi.

Alijitosa katika biashara ya kuwalea na kuwauza ndege mbalimbali ambao mara nyingi wanatumika nyumbani kama zana za kurembesha nyumba.

Alipomaliza masomo yake katika chuo cha mafunzo ya ndege cha aviation alipokuwa akisomea stashahada ya utalii wa kimataifa(International Tourism), aliamua kujitoa mhanga kumsaidia babake ambaye tayari alikuwa ameanza kujihusisha katika biashara ya kuwafuga na kuwalisha ndege mbalimbali na tangu hapo akafanikiwa kuiendeleza biashara hii. Anasema kwamba ujio wa gonjwa hatari la Covid-19 ulimsaidia sana kujimudu kwani ndipo alianza biashara hii adhimu.

“Nilipomaliza chuo cha mafunzo ya ndege cha Aviation,jijini Nairobi nilionelea vyema kuwafuga ndege ambao tayari niliwapenda. Lakini mara tu nilipofuzu katika chuo cha Aviation kwa masomo ya Utalii mwaka wa 2019 mwezi Disemba,nilianza kuwafuga ndege tofauti kwa sababu sikuwa nimepata kazi . lakini ujio wa gonjwa la Korona ukafifisha kabisa tamaa yangu ya kupata kazi. Wakati mwingine ilkuwa vigumu kuwakimu kabisa ndipo nilianza na ndege wa sampuli moja,kuku aina ya Silky kisha nikaongeza wengine,” anasema

Licha ya kuwa na masomo ya stashahada,Ibrahim alishindwa kujizuia kufanya alichokipenda akaamua kujihusisha katika biashara hii adhimu. Anasema kwamba biashara hii imemsaidia pakubwa kujiinua kiuchumi kwani imempa uwezo wa kukimu mahitaji yake ya kimsingi pamoja na yale ya familia yao. Anasema kwamba alianza kuonyesha kuwapenda Wanyama tangu alipokuwa mtoto mdogo akiwa shule ya msingi,alipokuwa akiwafuga Wanyama wa nyumbani kama vile sungura na kuku.

“Kazi hii ninaifanya kwa sababu ni uraibu wangu,napenda kuwafuga Wanyama. Hata nilipokuwa nasoma shule ya msingi,nilipenda kuwafuga sungura na kuku ambao niliwapenda sana,” anaeleza. PICHA/ WACHIRA ELISHAPAN

Tofauti na wakazi wengine katika Kijiji cha Samar(Mariiki), eneobunge la Maragua katika Kaunti ya Murang’a ambao wanazamia katika biashara ya kuwafuga ng’ombe,mbuzi na kondoo , Ibrahim anasema kwamba badala yake aliamua kilimo cha ndege wa aina mbalimbali wa mwituni kama kanga na njiwa ambao hawapatikani kwingi ili kuonyesha upekee wake katika Sanaa ya urembo. Anasema kwamba kuwafuga ndege kama hawa wa mwitu humpa raha kwani huwa na urembo wa ajabu. Kati ya ndege anaofuga ni bata,kuku aina ya Silky, kanga na njiwa

“ Sitaki kuwa kama wafugaji wengine hapa Samar wanaofuga ng’ombe na mbuzi,nataka ufugaji wangu uwe wa kipekee. Nataka niwape hifadhi ndege hawa wa mwituni kwa sababu hawapatikani kwingi. Kila mara ninapoamka kuwahudumia huona raha sana,” anasema.

Ibrahim anasema kwamba amekuwa akiwauza kuku wake kwa watu binafsi ambao wameonyesha haja ya kumuunga mkono katika anachofanya. Kufikia muda wa Akilimali kumtembelea kwake nyumbani, anasema kwamba tayari alikuwa amewauza kuku 30 kwa kipindi cha wiki moja kwa bei ya shillingi 1200 kila mmoja. Akilinganisha jinsi alivyonunua kifaranga mmoja kwa shillingi 150 kwa kila mmoja,Ibrahim anasema kwamba kazi imemletea faida kubwa.

“Nimekuwa nikiwauza ndege wangu kwa wakazi wa huku kwetu, lakini mara kwa mara nimepata wageni kutoka mbali kidogo kama Kenol na Murang’a. Kama wiki moja iliyopita nimeuza njiwa kadhaa na kuku 30, na bado nimebaki na kuku kama 25 hivi na kanga 15,” anasema Ibrahim.

” Homa hii ni hatari sana,lakini wakulima kama Ibrahim wasitie shaka. Watilie maanani chanjo inayotolewa kila mwaka kwa ndege na watafaulu, lakini pia wasimwone daktari ovyo wa mifugo, watafute wataalamu,” anasema Dkt.Gichuru.

Ibrahim amewajengea kuku na kanga wake vibanda vilivyokandikwa udongo na kuezekwa mbati,lakini vikawekewa nguzo za vikingi vya saruji. Imani yake imebaki kwamba jasho lake lazima lilindwe ifaavyo kwa kuwajengea vizuri. Njiwa nao kama ndege wanaopaa, amewajengea vibanda alivyoviinua juu vyenye matundu ili kuwapa nafasi kuishi kama mwituni.

Kwa kuwa amekuwa mkulima mzuri, anadokeza kwamba chakula anachowapa ndege hao anakichanganya vizuri kwa kutumia fomyula maalum inayowapa madini na virutubisho vizuri kwa afya njema. Anasema kwamba hatua ya kwanza anapoamka ni kusafisha mahali wanapoishi ndege hawa ili kuwalinda kutokana na magonjwa hatari yanayoweza kumpoka jasho lake.

“Nina fomyula maalum ya kuchanganya chakula,sitaki kuwapa chakula kingi lakini pia sitaki kuwanyima. Ninachothamini hapa ni afya ya ndege wangu,na kila ninapoamka asubuhi,lazima niyaoshe mabanda vizuri ili wasiadhirike na magonjwa,” anadokeza.

Hata hivyo,Ibrahim anasema kwamba kwa kazi yake hii kuna changamoto kadhaa,akitaja magonjwa ya kuambukiza kama homa ya nyuni kama adui mkubwa kwa kuku na bata. Anasema kwamba yeye huwapa kinga ya chanjo ( vaccine) ndege wake mara anapogundua kwamba kuna ugonjwa unaoambukiza ndege.

Kwa mujibu wa Dkt Gichuru ambaye ni mtaalamu wa afya kwa mifugo na ndege, ugonjwa wa homa kwa nyuni (Avian influenza) ni hatari na unaweza hata kusababisha vifo vya maelfu ya nyuni. Dkt Gichuru anatoa ushauri kwa wafugaji kuvaa mavazi ya kujikinga kwani homa hii pia huadhiri binadamu wanapotagusana kwa njia ya moja kwa moja na nyuni hao.

Hata hivyo,anadokeza kwamba njia rahisi ya kuepuka homa hii ni kuwapa chanjo nyuni angalau mara moja kwa mwaka.

Na licha ya kuwa biashara hii imemkuza kifedha, anasema kwamba changamoto ya kununuliwa kwa ndege wake kwa bei ya chini hufifisha matumaini yake ya kuongezea idadi ya ndege wake.

“Biashara imekuwa nzuri sana wakati hakuna magonjwa,lakini mambo huwa magumu sana wakati badhi ya wanunuzi wananunua kwa bei ya chini(brokers). Msimu wa sherehe nyingi kama za krismasi huwa wa mavuno,” anasema

Katika kuwauza ndege wake, Ibrahim anadokeza kwamba mtandao wa facebook umekuwa wa manufaa sana kwake kwani yeye hupachika picha humo na hatimaye akapata wateja. Japo huwa hashughuliki na kulisha mifugo kama ng’ombe, Ibrahim anasema kwamba hajutii chaguo lake na yuko tayari kupanua biashara yake.

You can share this post!

Fahamu muda sahihi unaopaswa kula matunda

Wakenya waendelea kuishinikiza IMF kukoma kuikopesha Kenya