Ufugaji wa nguruwe unavyompa mkulima kipato Mwatate

Ufugaji wa nguruwe unavyompa mkulima kipato Mwatate

NA PETER CHANGTOEK

MARTIN Msafari, amekuwa akishirikiana na ndugu yake na mama yake katika shughuli ya ufugaji wa nguruwe.

Mbali na kuwauza wanyama hao kwa wateja kutoka sehemu tofauti tofauti nchini, amekuwa akiwachinja baadhi ya nguruwe wake na kuwauzia wateja wake. Katika kitongoji cha Jombo, Mwatate, Kaunti ya Taita Taveta, mkulima huyo analimiliki shamba linalojulikana kwa jina Zosans Farm.

Yeye hushirikiana na mama yake anayejulikana kama Christine Mwakio na ndugu yake anayefahamika kama Harris Malambo. Msafari anadokeza kuwa, walijitosa katika shughuli hiyo ya ufugaji wa nguruwe mnamo mwaka 2013, wakiwa wameshirikiana pamoja.

Wakati huo huo, shughuli hiyo ilikuwa chini ya usimamizi wa wazazi wake. Lakini kwa sasa, yeye ndiye msimamizi. “Mradi huo ulikuwa umeanzisha mnamo mwaka 1995,” asema mkulima huyo, ambaye ni baba wa wasichana watatu.

Kwa sababu ya changamoto za hapa na pale, Msafari anasema kuwa shughuli hiyo ilikuwa imesitishwa, na ikaanzishwa tena upya baadaye. Wakati shughuli hiyo ilipoanzishwa upya, waliutumia Sh30,000, pesa taslimu, zilizotumika kuwanunua nguruwe watano.

Christine katika shamba lao la Zosans Farm…Picha/PETER CHANGTOEK

“Tuliwanunua nguruwe 6 kutoka Kaunti ya Kiambu, kwa Sh5,000 kila mmoja,” afichua Msafari. Anaongeza kuwa, wazazi wake ndio waliomfundisha jinsi ya kuwafuga wanyama hao. “Wazazi wetu walikuwa wakipata pesa za kutuelimisha kutoka kwa ufugaji wa nguruwe, tulipokuwa katika shule za upili,” adokeza mkulima huyo, aliyesomea taaluma ya uhasibu katika taasisi ya NYS.

Shamba wanalolitumia kuendeleza shughuli hiyo ni ekari moja, lakini wameitenga sehemu fulani ambayo huitumia kwa kilimo-biashara hicho. Msafari anadokeza kwamba, vibanda ambavyo wao huvitumia kuwafuga nguruwe wao, vina ukubwa wa futi 20 kwa futi 10.

Anafichua kuwa, ni jambo muhimu kutunza rekodi za shughuli zinazofanyika katika shamba linalotumika kuwafuga nguruwe. Hilo ni mojawapo la majukumu muhimu katika shughuli za ufugaji. Mkulima huyo hujitengenezea lishe anazozitumia kuwalisha nguruwe wake.

Yeye huchanganya aina ainati za mazao ya shambani kama vile mahindi, na malighafi nyinginezo ili kupata lishe. Msafari anaeleza kuwa, kuna wakati ambapo walikuwa wamefikisha nguruwe 120 katika shamba lao, lakini wakawauza na kuwachinja kadhaa.

Kuna baadhi ya changamoto zinazochangia kupunguzwa kwa idadi ya nguruwe shambani. Mojawapo ya changamoto hizo ni bei za juu za lishe. Aidha, magonjwa huwafanya wakulima wengi kupunguza idadi ya nguruwe wanaowafuga, kwa sababu kuna magonjwa kadha wa kadha yanayowaangamiza nguruwe kwa wingi, endapo mkulima hatachukua tahadhari kabla ya hatari.

Hata hivyo, mkulima huyo anasema kuwa, hawajawahi kukabiliwa na magonjwa yanayowaathiri nguruwe. Kwa wakati huu, Msafari ana nguruwe 20 katika shamba lao. “Tuna nguruwe sita wa kike, wawili wa kiume na wadogo, ambao ni kumi na wawili,” afichua Msafari, ambaye huwafuga nguruwe aina ya Landrace na Large white.

Mkulima huyo anasema kwamba, wana uwezo wa kutia kibindoni Sh500,000 kwa mwaka mmoja kutokana na ufugaji wa nguruwe na uuzaji wa nyama. Anawashauri wale ambao wana nia ya kujitosa katika shughuli ya ufugaji wa nguruwe kufanya hivyo, maadamu ni kilimo-biashara kilicho na tija, muradi tu ufanywe kwa njia iliyo mwafaka.

Anapania kununua mashine za kusaga lishe za nguruwe katika siku za usoni. Pia, anasema kuwa anaazimia kufungua bucha la kuuzia nyama za nguruwe. Yeye huwauza nguruwe wake kwa bei tofauti tofauti, kwa kutegemea mambo mbalimbali.

Huwauza kwa bei kuanzia Sh3,500-Sh40,000. Anasema kwamba, huwachinja nguruwe wawili kwa mwezi mmoja. Hata hivyo, anasisitiza kuwa, idadi huongezeka kwa kutegemea oda za wateja. “Mimi huwachinja siku za Jumamosi, kwa sababu watu wote huwa nyumbani ili wanisaidie kusambaza nyama,” aongeza mkulima huyo, ambaye huuza nyama ya nguruwe kilo moja kwa Sh400.

Ili kuwapata wateja, mkulima huyo anasema kwamba, huenda nyumba kwa nyumba, akitafuta oda kutoka kwa wateja.

You can share this post!

Kijana mwenye vipaji vingi, anayevitumia kuwafaa wenzake

Shahidi wa kesi dhidi ya Gicheru ICC ‘atoweka’

T L