Habari za Kitaifa

Ufunguzi wa shule waahirishwa kwa juma moja zaidi kutokana na mafuriko

April 29th, 2024 1 min read

NA TAIFA LEO RIPOTA

SERIKALI imeahirishwa kufunguliwa kwa shule kote nchini kutokana na mafuriko makubwa yanayoendelea kushuhudiwa katika sehemu nyingi za taifa.

Tarehe mpya ya kufunguliwa shule sasa ni Mei 6, 2024, ikimaanisha kwamba wanafunzi wana angalau juma moja zaidi la kukaa nyumbani.

Kupitia taarifa iliyotolewa na Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu, maafisa wa nyanjani badala yake wametakiwa kuwasilisha maelezo na data kutoka kwa shule zote za msingi na upili ili kuwezesha Serikali kutathmini utayarifu wa kuanza kwa Muhula wa Pili ambao ulikuwa uanze Aprili 29, 2024.

“Ripoti zilizotufikia, na ambazo zimethibitishwa na vitengo vingine vya serikali zinaonyesha kwamba shule mbali mbali zimeathiriwa vibaya na mafuriko,” ikasema taarifa hiyo.

Inaendelea kusema kwamba athari za mafuriko hayo ziko mbaya zaidi kiasi kwamba zitahatarisha pakubwa maisha ya wanafunzi na walimu kabla ya hatua madhubuti kuchukuliwa.

Ni kwa sababu hii, Serikali inasema, imelazimika kuahirisha ufunguzi wa shule kwa Muhula wa Pili.