Michezo

UG yapiga Kenya na kupanda nafasi saba viwango vya raga

June 24th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

UGANDA imeruka juu nafasi saba kwenye viwango bora vya raga ya wachezaji 15 kila upande duniani baada ya kuzima Kenya kwa alama 16-13 katika Kombe la Elgon mjini Kisumu mnamo Juni 22, 2019.

Cranes, ambayo haikuwa imechapa Kenya nchini Kenya tangu ishinde 17-16 mwaka 2013, ilizoa ushindi huo muhimu kupitia alama za Adrian Kasito (mguso), Aaron Ofoyrwoth (penalti na goli la alama tatu) na Santos Senteza (mguso) na kurukia nafasi ya 35 kutoka 41.

Waganda wameruka Lithuania, Zimbabwe, Ukraine, Czech, Malta na Tunisia ambazo zimeteremka nafasi moja kila mmoja na kufuatana kutoka nafasi ya 35 hadi 41.

Katika viwanga bora vya Bara Afrika, mabingwa Namibia wanaongoza katika nafasi ya 23 na kufuatiwa na Simbas ya Kenya, ambayo inatetea taji la Elgon Cup, katika nafasi ya 32 duniani. Simbas imepoteza karibu alama mbili kwa kulimwa na Uganda na sasa ina jumla ya alama 51.05. Imekwamilia nafasi hiyo, ingawa sasa iko mbele ya nambari 33 Colombia kwa alama 0.29 pekee.

Uganda ni ya tatu (nafasi sita juu hadi nambari 35 duniani), Zimbabwe (nafasi moja chini hadi 37 duniani), Tunisia (imeteremka nafasi moja hadi 41 duniani) nazo Morocco, Madagascar na Senegal zimekwamilia nafasi za 47, 53 na 55 duniani mtawalia. Zambia na Nigeria zinafunga 10-bora barani Afrika katika nafasi 65 na 71 duniani, mtawalia.

Mabadiliko mengine katika viwango hivi vya mataifa 105 ni Uhispania kupaa nafasi mbili hadi nambari 17 duniani ikibadilishana nafasi ya 19 na Uruguay. Uhispania ilicharaza Uruguay 41-21 jijini Montevideo mnamo Juni 22.

Kenya itazuru jijini Kampala mnamo Julai 13 kwa mechi ya marudiano dhidi ya Uganda.

Aidha, Lionesses ya Kenya na She Cranes ya Uganda zimesalia katika nafasi za 31 na 41 kwenye viwango bora vya wanawake vinavyohusisha mataifa 53. Lionesses ilipepeta Waganda 42-13 mjini Kisumu mnamo Juni 22 katika mechi ya mkondo wa kwanza ya Elgon Cup. Afrika Kusini ndiyo ya kwanza barani Afrika katika nafasi ya 11 duniani ikifuatiwa na Kenya (31), Zimbabwe (37), Namibia (39) halafu Uganda na Botswana zinazoshikilia nafasi ya 41 duniani.