Makala

UGAIDI: Al Shabaab walazimisha wakazi kukosa huduma muhimu

September 5th, 2018 3 min read

Na KALUME KAZUNGU

MASHAMBULIZI ya mara kwa mara ya Al-Shabaab ambayo yamekuwa yakishuhudiwa kwenye baadhi ya maeneo ya Kaunti ya Lamu yamewanyima wakazi wa maeneo husika huduma muhimu za serikali.

Baadhi ya maeneo ambayo yameathiriwa zaidi na mashambulizi ya Al-Shabaab ni Basuba, Milimani, Mangai, Mararani na Kiangwe.

Vijiji vilivyoko mpakani mwa Lamu na Somalia, ikiwemo Kiunga na Ishakani pia ni miongoni mwa maeneo ambayo yanakosa kufikiwa na huduma muhimu za serikali kufuatia hali duni ya usalama inayochangiwa na Al-Shabaab.

Elimu, afya, barabara na mawasiliano ni miongoni mwa sekta ambazo zimeathiriwa pakubwa hasa tangu Al-Shabaab walipoanza kushambulia maeneo husika kati ya 2014 hadi sasa.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo juma hili ulibaini kuwa shule zote tano za wadi ya Basuba hazikufunguliwa tena kwa muhula wa tatu, ikiwa ni takriban mwaka wa nne mfululizo sasa tangu shule hizo zilipofungwa kutokana na hatari za kiusalama.

Shule za Basuba, Milimani, Mangai, Mararani na Kiangwe zilifungwa mnamo 2015 baada ya walimu waliokuwa wakihudumu kwenye maeneo husika kutoroka kwa kuhofia usalama wao.

Ilibainika kuwa nyingi ya shule hizo kwa sasa zimemea magugu na kugeuka kuwa mahame tangu wanafunzi na walimu walipositisha shughuli zao za masomo kwenye shule hizo.

Baadhi ya wazazi waliozungumza nasi walieleza masikitiko yao kuhusiana na jinsi watoto wao wanavyoendelea kukaa nyumbani bila masomo tangu shule zao zilipofungwa.

Licha ya serikali ya Kaunti ya Lamu kujitahidi na kuhamisha takriban wanafunzi 260 wa darasa la nne hadi nane hadi shule ya Mokowe Arid Zone ambayo iko kwenye eneo salama, imebainika kuwa idadi kubwa ya wanafunzi kutoka maeneo yanayokaribiana na msitu wa Boni bado wamesalia majumbani bila elimu.

“Tuko na watoto wadogo ambao wanastahili kusoma wakiwa chini ya uangalizi wa wazazi wao. Hawawezi kuhamishwa kusomea sehemu za mbali kama wengine kutokana na umri wao mdogo. Ombi letu ni shule zifunguliwe na watoto wetu wasome wakiwa karibu na wazazi wao,” akasema Bw Yusuf Abdi.

Changamoto nyingine inayokabili wakazi ni ukosefu wa huduma za afya.

Taifa Leo ilibaini kuwa wanawake wajawazito na watoto ndio wanaoteseka hata zaidi kwa kukosa huduma za kliniki kwenye vijiji husika.

Hospitali zote kwenye wadi ya Basuba na maeneo yanayopakana na msitu wa Boni pia zilifungwa miaka minne iliyopita baada ya Al-Shabaab kuendeleza mashambulizi ya kila mara.

Madaktari waliokuwa wakihudumu kwenye maeneo husika pia walitoroka kwa kuhofia kulengwa na Al-Shabaab.

“Sisi mara nyingine hulazimika kutafuta waganga wa kienyeji ili kutibiwa. Wakunga pia wamekuwa wakitusaidia kuzaa. Hakuna huduma za kliniki hapa kwani hata hospitali yenyewe hakuna,” akasema Bi Khadija Gurba ambaye ni mkazi wa Mangai.

Ukosefu wa mawasiliano pia ni changamoto nyingine inayokabili wakazi wa vijiji vinavyopakana na msitu wa Boni na nchi jirani ya Somalia.

Licha ya serikali kushirikiana na kampuni za mawasiliano na kuweka milingoti ya mawasiliano kwenye baadhi ya vijiji, idadi kubwa ya milingoti hiyo haifanyi kazi hasa baada ya magaidi wa Al-Shabaab kuilenga na kuilipua.

Mwakilishi wa Wadi ya Basuba, Deko Barissa anasema wamelazimika kupanda juu ya miti kila wakati wanapofanya mawasiliano.

“Serfikali iangazie suala hili la mawasiliano hapa Basuba. Tunapanda juu ya miti kutafuta mawimbi kila tunapohitaji kuwasiliana na wengine nchini. Milingoti mingi hapa haifanyi kazi tangu ilipoharibiwa na Al-Shabaab,” akasema Bw Deko.

Wakazi pia waliitaka serikali kutekeleza ujenzi wa barabara kuu ya Kiunga hadi Hindi ili kupunguza visa ambavyo vimekuwa vikishuhudiwa vya mashambulizi na mauaji yanayotekelezwa na Al-Shabaab.

Ni hivi majuzi ambapo wanajeshi zaidi ya 10 wa Kenya (KDF) waliuawa kwenye mashambulizi mawili tofauti kwenye eneo la Sankuri na Bodhei kwenye barabara hiyo ya Kiunga kuelekea Hindi.

Mashambulizi hayo ya vilipuzi vya kujitengenezea yanashukiwa kutekelezwa na Al-Shabaab.

Wakazi wanaamini iwapo barabara hiyo itakarabatiwa itasuluhisha suala tata la usalama eneo hilo.

Mnamo Septemba, 2015, serikali ya kitaifa ilizindua operesheni ya Linda Boni, Kaunti ya Lamu, dhamira kuu ikiwa ni kuwasaka na kuwamaliza magaidi wa Al-Shabaab wanaoaminika kujificha ndani yam situ wa Boni.

Operesheni hiyo inaendelea hadi sasa.