Habari Mseto

Ugaidi: Familia yalia polisi imwache huru mwanao

December 15th, 2019 1 min read

Na FADHILI FREDRICK

Familia moja katika Kwale inawataka maafisa wa polisi kumweka huru kijana wao mwenye umri wa miaka 20 ambaye walimkamata kwa tuhuma za kuwa mwanachama wa kikundi cha kigaidi.

Bw Rashid Kombo, mwalimu wa madrassa katika kijiji cha Mulungunipa katika kauntindogo ya Msambweni, alikamatwa na polisi Alhamisi wiki iliyopita.

Kulingana na mama yake, Bi Mwanakmbo Abdulrahman, maafisa wa polisi walivamia nyumba yao na kudai kwamba waliiba Sh10,000.

“Walikuwa wanatafuta wanangu wawili lakini walifanikiwa kumkamata mmoja wakati alipokuwa akija nyumbani kwa baiskeli na kutumia nguvu kumtia mbaroni na kuondoka naye tusifahamu walikompeleka ” akasema.

Aliongeza kuwa walifanikiwa kupata kofia na viatu alivyokuwa amevaa siku hiyo ya purukushani.

Mama huyo alibubujikwa machozi kwa uchungu wakati akiongea na wanahabari katika mji wa Ukunda akiwa na familia na maafisa wa shirika la kutetea haki za binadamu la MUHURI.

Binamu yake Shamakame Rumba alisema serikali ndiyo inayojua vizuri kule walikompeleka kwa hivyo wanataka mtoto wao aliyechukuliwa na maafisa hao aachwe huru.

“Kama familia tunataka serikali imlete akiwa amekufa au hai kwa sababu tunasikitika na hatujui hatma yake,” akasema.

Kisa hicho kiliripotiwa katika Kituo cha Polisi cha Diani lakini familia hiyo imeshindwa kujua aliko licha ya kuwasiliana na maafisa wa polisi katika kituo hicho.

Afisa wa Muhuri, Bw Francis Ouma alishutumu maafisa wa polisi kwa kufanya kazi kwa udhalimu mkubwa licha ya sheria ya kulinda washukiwa.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti ndogo ya Msambweni Bw Nehemia Bitok alisema hana habari juu kutiwa mbaroni kwa kijana huyo lakini aliahidi kufuatilia swala hilo.