Ugaidi Lamu ulipungua 2020

Ugaidi Lamu ulipungua 2020

Na KALUME KAZUNGU

WAKAZI wa kaunti ya Lamu wana matumaini makubwa kwamba vita dhidi ya magaidi wa Al-Shabaab vitamalizwa eneo hilo ifikapo mwaka 2021.

Wakazi wanaimiminia sifa serikali kwa jinsi ambavyo imesaidia pakubwa kupunguza visa vya magaidi hao kushambulia na kuua raia na walinda usalama katika mwaka 2020.

Kinyume na ilivyokuwa katika miaka ya awali, ambapo Lamu ingeshuhudia visa vingi vya mashambulizi kutoka kwa Al-Shabaab, mwaka wa 2020 ndio ulioshuhudia visa vichache zaidi vya wanamgambo hao kushambulia na kuua wananchi na walinda usalama.

Mnamo Januari 2 mwaka huu, magaidi wa Al-Shabaab walivamia mojawapo ya mabasi ya usafiri wa umma katika eneo la Nyongoro, kwenye barabara kuu ya Lamu kuelekea Mombasa, ambapo waliua abiria watatu na kujeruhi wengine watatu.

Masaaa machache baadaye, maafisa wa usalama wa;litekeleza msako mkali dhidi ya wahalifu hao, ambapo walifaulu kuua wanne na kumkamata mwingine akiwa hai.

Januari 5 mwaka huu, kundi la magaidi wa Al-Shabaab waliokuwa wamejihami kwa silaha hatari walivamia kambi ya jeshi la Kenya na lile la Marekani eneo la Manda, kaunti ya Lamu.

Wakati wa uvamizi huo wa alfajiri, wanajeshi walifaulu kuwaua wanamgambo watano wa Al-Shabaab huku mmoja akikamatwa akiwa hai.

Desemba 20 mwaka huu, walinda usalama walitibua jaribio la Al-Shabaab kuvamia na kuliteka nyara gari la polisi wa kushika doria mipakani (BPU) katika eneo la Nyongoro kwenye barabara ya Lamu kuelekea Mombasa.

Kisa cha hivi punde zaidi kushuhudiwa Lamu ni kile cha Desemba 27, ambapo wanajeshi wa Kenya (KDF) walivamia maficho ya Al-Shabaab kwenye eneo la Bodhai, msituni Boni ambapo waliua wanamgambo kadhaa wa kundi hilo na kujeruhi wengine wengi.

Wakati wa uvamizi huo, mmoja wa wanamgambo wa Al-Shabaab alikamatwa akiwa hai ilhali zana mbalimbali za kivita zinazotumiwa na magaidi hao zikinaswa.

Katika mahojiano na Taifa Leo juma hili, wakazi waliimiminia sifa kochokocho serikali hasa kwa kuanzisha operesheni ya usalama ya Linda Boni inayoendelezwa ndani ya msitu wa Boni.

Operesheni hiyo ilizinduliwa Septemba, 2015, dhamira kuu ikiwa ni kuwamaliza magaidi wa Al-Shabaab wanaojificha ndani yam situ wa Boni.

Bw Hemed Abdi alisema matarajio yake ni kwamba mwaka wa 2021 uwe wa amani na ambao hautashuhudia tukio lolote la kigaidi.

“Nafurahi kwamba mwaka 2020 umekuwa mwaka mwema uliokosa visanga vingi vya Al-Shabaab kinyume na miaka iliyopita. Ni matarajio yangu kwamba vita dhidi ya Al-Shabaab vitamalizwa kabisa ili mwaka wa 2021 uwe wa amani na utulivu,” akasema Bw Abdi.

Ali Salim alisema anatarajia kwamba safari za usiku ambazo zilikatizwa kwenye barabara kuu ya Lamu kuelekea Mombasa kutokana na kero la Al-Shabaab zitarejelewa ifikapo 2021.

Alisema watumiaji wengi wa barabara ya Lamu kuelekea Mombasa kwa sasa wamebadili misimamo yao, ambapo baadhi yao husafiri kwa ndege ili kuepuka kuvamiwa na Al-Sahabaab.

“Ombi letu ni kwamba vita vya Al-Shabaab vizikwe katika kaburi la sahau ili tukiingia mwaka 2021 uwe wa amani n ahata hizi safari za usiku barabarani zirejelewe. Kusafiri kwa ndege ni ghali mno na wengi wamelazimika kufanya hivyo ili kuepuka kuvamiwa barabarani na Al-Shabaab,” akasema Bw Salim.

Kwa upande wake aidha, Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Irungu Macharia, aliwahakikishia wakazi usalama wao msimu huu wa sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya.

Alisema kila mahali, ikiwemo barabarani, angani, baharini n ahata kwenye msitu kunalindwa vilivyo.

“Tumeongeza doria za KDF na polisi kila mahali. Hakuna sababu ya wananchi kuhofia kwani tumedhibiti vilivyo usalama wao,” akasema Bw Macharia.

You can share this post!

Corona yanusuru Sh290 milioni bungeni

MARY WANGARI: Tuwe na matumaini 2021 itakuwa yenye heri...