Michezo

Ugaidi wafanya vijiji Lamu visalie mahame

September 19th, 2020 2 min read

Na KALUME KAZUNGU

MAGAIDI wa Al-Shabaab wamevuruga maisha ya wakazi kwenye vijiji kadha vya Lamu ambavyo miaka iliyopita vilishuhudia mashambulizi ya kila mara.

Baadhi ya vijiji vimeachwa mahame ilhali vingine vikisalia na idadi ndogo ya watu.

Miongoni mwa vijiji ambavyo viliathirika na mashambulizi ya Al-Shabaab kaunti ya Lamu ni Maleli, Nyongoro, Kaisari, Mavuno, Poromoko na Mararani.

Utafiti uliofanywa na Taifa Leo ulibaini kuwa kijiji kama vile Kaisari, kimeachwa ganjo baada ya wakazi kuhamia maeneo salama, ikiwemo Kibaoni na Mpeketoni, karibu kilomita 60 kutoka kijiji hicho.

Mnamo Julai, 2014, wiki chache baada ya Al-Shabaab kuvamia mji wa Mpeketoni na kuua wanaume 60, kuteketeza mali ya mamilioni, magaidi hao hao walivamia kijiji cha Kaisari ambapo waliwatoa watu kwa nyumba zao na kuwachinja wanaume 16.

Januari, 2016, magaidi wa Al-Shabaab walivamia kijiji hicho cha Kaisari kwa mara ya pili ambapo waliwachinja wanaume watatu na kuteketeza nyumba.

Hali hiyo ilifanya wakazi kuhama kutoka kijiji hicho ambacho kilionekana kuwa cha laana kufuatia masaibu yaliyokuwa yakiwakumba.

Katika kijiji cha Mararani kilichoko ndani ya msitu wa Boni, hali ya upweke inazidi kuandama kijiji hicho baada ya idadi kubwa ya wakazi kutoroka kijijini humo.

Kulingana na mzee wa kijiji cha Mararani, Bw Hassan Mahadhi, ni familia tano pekee kati ya 80 zilizosalia kijijini humo.

Bw Mahadhi alisema kijiji hicho kimevamiwa karibu mara tano na Al-Shabaab kati ya 2014 na 2015.

“Hali ya upweke imetanda hapa Mararani. Kabla mashambulizi ya kila mara ya Al-Shabaab kutekelezwa, zaidi ya familia 80 zilikuwa zikiishi hapa. Tumesalia familia tano pekee. Yote hayo yameletwa na hofu ya Al-Shabaab,” akasema Bw Mahadhi.

Katika kijiji cha Maleli, asilimia 60 ya wakazi waliokuwa wakiishi kijijini humo walihama na kuapa kutordi tena eneo hilo.

Mnamo Agosti, 2017, kijiji cha Maleli kiligonga vichwa vya habari magaidi wa Al-Shabaab walipovamia kijiji hicho na kuua watu wanne.

Kwa sasa wakazi wengi wa kijiji cha Maleli wamehamia eneo la Katsaka Kairu ambako wamepiga kambi huko tangu 2017.

Katika vijiji vya Mavuno na Poromoko vilivyoko Wadi ya Mkunumbi, Kaunti ya Lamu, wakazi wamevigeuza vijiji hivyo kuwa mashamba yao, ambapo wamekuwa wakifika kulima na kulisha mifugo na kurudi Mpeketoni na Kibaoni.

“Hatuwezi kuishi vijijini humo tena. Tunaenda tu kulima na kurudi Mpeketoni. Vijiji vyetu hivyo vilikuwa vikitumiwa kama njia za Al-Shabaab na hilo limetutia woga,” akasema Bi Mary Kamau.

Hata hivyo, Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Bw Irungu Macharia, alisema usalama umeimarishwa vilivyo kote Lamu na akawataka wakazi wasiwe na wasiwasi.