Ugaidi watishia tena juhudi za kufufua utalii kisiwani Lamu

Ugaidi watishia tena juhudi za kufufua utalii kisiwani Lamu

KALUME KAZUNGU NA VALENTINE OBARA

MATUMAINI ya serikali ya Kaunti ya Lamu kuimarisha utalii eneo hilo yametiwa doa na mashambulio ya kigaidi yaliyochipuka upya wiki chache zilizopita.

Tangu mwaka 2022, serikali ya kaunti hiyo ilikuwa imerejelea maandalizi ya tamasha na hafla mbalimbali za kusisimua watalii.

Hata hivyo, baada ya utulivu wa muda mrefu, mashambulio yalianza kuibuka upya kwa njia ya kutisha baadaye Desemba na kuendelea hadi mapema mwezi huu wa Januari.

“Lengo letu ni kurejesha Lamu yenye amani na utulivu; Lamu ambayo imenawiri kitalii, kibiashara na kadhalika. Hii ndiyo sababu sisi kama kaunti tukaafikia kurejesha tamasha za kila mwaka eneo hili. Tayari tumejionea jinsi Lamu ilivyofufuka kiuchumi, na bado. Tutajikaza zaidi kuona kwamba sekta zetu za kiuchumi zinafanya vyema kwa hadi asilimia 100,” Gavana Issa Timamy, alisema kwenye mahojiano ya awali.

Baadhi ya tamasha ambazo huvutia watalii wa kimataifa ni kama vile tamasha ya utamaduni wa Lamu, yoga, Maulidi, mashindano ya kila mwaka ya uvuvi, tamasha la sanaa ya uchoraji na ubunifu, maonyesho ya vyakula vya kitamaduni, miongoni mwa mengine.

Kulingana na Chama cha Utalii Lamu (LTA), kati ya mwaka wa 2014 na 2018 wakati makundi ya kigaidi yalipokuwa yakivamia kila mara, utalii ulisambaratika hadi chini ya asilimia 10.

Baadaye kuanzia mwaka wa 2020, sekta hiyo ilipata pigo zaidi kwa sababu ya janga la virusi vya Covid-19 ambalo lilivuruga shughuli zote ulimwenguni.

Shambulio la hivi punde zaidi ni lile la Jumanne iliyopita, ambapo magaidi walivamia msafara wa magari ya ujenzi wa barabara ya Lamu-Ijara-Garissa katika eneo la Algis-Malhadhon, karibu kilomita 7 kutoka kituo cha polisi cha Bodhei.

Waliua mfanyakazi mmoja na kujeruhi watu sita, ikiwemo wanajeshi wawili (KDF) huku wakichoma magari.

Mnamo Desemba 28, 2022, magaidi waliovalia sare za kijeshi walivamia magari na kuua dereva wa lori na utingo wake eneo la Mambo Sasa, karibu na Witu.

Katika mahojiano yake ya kwanza ya ana kwa ana na wanahabari wa runinga nchini, Rais William Ruto alisema serikali ishatambua wafadhili wa makundi ya kigaidi yanayovamia maeneo ya Lamu kila mara.

Siku chache baadaye, Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI), ilichapisha majina ya washukiwa wanne waliodaiwa kuhusika katika mashambulio ambayo hutokea Lamu.

Mapema mwezi huu Januari wakati Waziri wa Usalama wa Ndani, Prof Kithure Kindiki alipozuru Lamu kutathmini hali ya usalama, aliagiza doria za polisi na KDF kuongezwa ili kudhibiti usalama wa watumiaji wa barabara, kurahisisha usafiri na pia kuhakikisha biashara ya uchukuzi haitatizwi.

Mbali na utalii ulio kitega uchumi kikubwa katika eneo hilo, serikali imewekeza mabilioni ya pesa kwa miradi mikubwa ya kimaendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara kuu na bandari, chini ya mradi wa Uchukuzi kati ya Bandari ya Lamu, Sudan Kusini na Ethiopia (LAPSSET).

Miradi ya LAPSSET, hasa ule wa Sh17.9 bilioni wa barabara kuu ya Lamu-Ijara-Garissa, imekuwa ikikwamishwa kwa sababu ya uvamizi unaolenga wanakandarasi na wafanyakazi.

Baadhi ya nchi za Magharibi na Ulaya bado zimeorodhesha Lamu kama eneo hatari la kutembelewa na raia wake kwa sababu za kiusalama.

  • Tags

You can share this post!

Kinaya wabunge wakitafuna minofu huku wakidai CDF

Wafuasi njiapanda Raila akikana Ruto

T L