Ugali moto wa GMO wamchoma Ruto

Ugali moto wa GMO wamchoma Ruto

WANDERI KAMAU na TITUS OMINDE

UAMUZI wa serikali kuagiza magunia milioni 10 ya mahindi yaliyofanyiwa ukarabati wa kisayansi (GMO) umeendelea kuzua joto la kisiasa nchini na kupingwa vikali na baadhi ya wandani wa Rais William Ruto.

Wandani hao wamejitokeza kupinga hatua hiyo, wakisema kuwa inahatarisha afya na maisha ya mamilioni ya Wakenya wanaotumia mahindi kama chakula chao cha kawaida.

Ijapokuwa serikali imefafanua kwa nini ilichukua hatua hiyo -kupunguza njaa na kuongeza kiwango cha chakula nchini- uamuzi huo umekosolewa vikali na wanasiasa, wataalamu na wakulima wa mahindi.

Hapo jana Jumapili, kiongozi wa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya, Bw Raila Odinga, aliwahimiza Wakenya kukataa vyakula vya GMO, akimlaumu Rais Ruto kwa “kuwasaliti” raia kutokana na hatua ya kuruhusu uagizaji wake.

Kinara wa ODM, Raila Odinga (kati) akiandamana na Kiongozi wa Wachache bungeni Opiyo Wandayi (kushoto) na Mbunge wa Suna Mashariki, Junet Mohamed azungumza na wanahabari katika wakfu wa Jaramogi Oginga Odinga, Nairobi, Novemba 20, 2022. Raila alipinga mpango wa serikali wa kuagizia mahindi ya GMO. PICHA|LUCY WANJIRU

Kwenye kikao na wanahabari jana, Bw Odinga alisema kuwa uamuzi wa kuagiza vyakula hivyo ulifanywa bila kuushirikisha umma na wadau muhimu.

Bw Odinga alimlaumu Rais Ruto kwa kuwa “kikaragosi” cha mataifa ya kigeni, akiongeza kuwa hatua hiyo itaiathiri sana sekta ya kilimo nchini.

Alisema serikali inafaa kusitisha utekelezaji wa hatua hiyo na kubuni mashauriano mapya na wadau wa husika.

“Tunachukulia hatua ya kuondoa marufuku ya uagizaji wa vyakula vya GMO nchini kama usaliti kwa nchi yetu. Kwa hili, utawala wa Ruto hauwatumikii Wakenya. Yeye ni kikaragosi anayefanyia kazi mataifa ya kigeni na mashirika yao, kinyume na matakwa yetu kama nchi. Anabuni nafasi ya mashirika yanayotengeneza vyakula vya kisayansi ughaibuni,” akasema Bw Odinga.

Kigogo huyo wa siasa pia alimtaka Waziri wa Biashara, Viwanda na Uwekezaji, Moses Kuria, kuwaomba Wakenya msamaha kwa matamshi yake “mabaya”, akiyataja kukosa msingi wa kisayansi.

“Kama chama, tunaamini suala la uagizaji wa vyakula vya GMO nchini ni lenye uzito sana kuingizwa mzaha. Tunamwomba Bw Kuria na utawala wa UDA kuwaomba Wakenya msamaha,” akasema.

Waziri Kuria alinukuliwa akisema, “Almradi wewe ni Mkenya, kifo kinaweza kukupata wakati wowote. Na kwa kuwa kuna vitu vitu vingi nchini vinavyoweza kukua, hakuna shida tukiongeza GMO kwenye orodha hiyo.”

Pia, hatua hiyo imekosolewa vikali na Seneta Samson Cherargei wa Kaunti ya Nandi.

Kwenye kikao na wanahabari mjini Eldoret jana Jumapili, Bw Cherargei alimwambia Bw Kuria kusimamisha hatua hiyo hadi Februari, ili kuruhusu wakulima kuvuna mahindi yao msimu huu.

Bw Cherargei alisema wakulima kutoka maeneo yanayokuza mahindi katika Bonde la Ufa wanatarajia kupata mavuno mengi, kwani mahindi hayo yatafurika katika masoko ya humu nchini na kuwasababishia hasara wakulima ambao wamekuwa wakihangaika kupata soko.

“Kwa wakulima kutoka Kusini mwa Bonde la Ufa na katika sehemu nyingi za Kenya ambapo tunapanda mahindi, huu ni msimu wa mavuno na tuliona ni jambo la busara Wizara ya Biashara kusitisha uagizaji wa mahindi hayo hadi tuvune mahindi yetu na NCPB ifungue maghala ili wakulima wawasilishe mazao yao,” akasema.

Licha ya kutangaza kuiunga mkono serikali ya Rais Ruto, wakili mbishi Miguna Miguna pia alikashifu vikali hatua hiyo.

Kwenye ujumbe alioweka katika mtandao wa Twitter, Dkt Miguna alitaja hatua hiyo kuwa “mzaha”.

“Ninasema ‘La’ kwa haraka iliyopo katika kuagiza mahindi ya GMO na vyakula vingine nchini. Ninaamini kuwa hii ni hali ya kutojali kwa upande wa serikali ya Kenya Kwanza. Kunafaa kuwa na mashauriano mapana kuhusu masuala kama hayo yanayoathiri sera ya kitaifa,” akasema Dkt Miguna.

Mashirika kadhaa ya kutetea kilimo kama Greenpeace Africa na Biodiversity, pia yamejitokeza vikali kupinga vikali hatua hiyo.

Wadadisi wanasema hisia hizo zinafaa kuifungua macho serikali, kwani huenda ikaanza kuipotezea umaarufu wake licha ya hatua hiyo kuwa mkakati wa kukabili njaa nchini.

  • Tags

You can share this post!

WANTO WARUI: Wanafunzi wa Gredi ya Saba ni wa shule za...

Mtahiniwa azuiliwa kwa njama ya kuchoma bweni

T L