Habari

Uganda yaimarisha mikakati ya kukabili Ebola

June 14th, 2019 1 min read

Na DAILY MONITOR

SERIKALI ya Uganda Ijumaa imepiga marufuku mikutano ya hadhara katika wilaya ya Kasese Magharibi mwa nchi hiyo huku maafisa wakijaribu kuzuia kusambaa kwa ugonjwa wa Ebola.

Ugonjwa huo hatari tayari umesababisha vifo vya watu si chini ya wawili katika nchi hiyo siku chache baada ya virusi vya ugonjwa huo kusambaa kutoka nchi jirani ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo (DRC).

Msemaji wa Wizara ya Afya Emmanuel Ainebyona, amethibitisha hatua hiyo saa chache baada ya maafisa kutangaza kwamba mwanamke mmoja raia wa DRC mwenye umri wa miaka 50 ni mgonjwa wa pili kufariki kutokana na ugonjwa huo nchini Uganda.

Mjukuu wake wa kiume wa umri wa miaka mitano alithibitishwa kufariki kutokana na ugonjwa wa Ebola nchini Uganda.

Kakake mvulana huyo mwenye umri wa miaka mitatu pia ameambukizwa ugonjwa huo na anaendelea kutibiwa.

Watu hao watatu ni sehemu ya kundi la familia iliyosafiri hadi Katoka, DRC kuzika jamaa yao mmoja ambaye pia alifariki kutokana na ugonjwa wa Ebola, kabla ya kurejea nchini Uganda.

Maambukizihayo ni ya kwanza kuthibitishwa nchini Uganda.

Ebola ilizuka katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri Mashariki nchini DRC katika miezi 10 iliyopita.

Kufikia sasa imesababisha vifo vya zaidi ya watu 2,000 huku wagonjwa wengine 3,400 wakiendelea kutibiwa.

Hii ni kwa mujibu wa takwimu kutoka Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO).

Habari hii imetafsiriwa na CHARLES WASONGA