Uganda yamruka Ruto kuhusu ziara yake iliyotibuka

Uganda yamruka Ruto kuhusu ziara yake iliyotibuka

Na LEONARD ONYANGO

SERIKALI ya Uganda imemruka Naibu wa Rais William Ruto kuhusu ziara yake iliyotibuka mapema wiki hii, ikisema haikumtarajia.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Uganda, Okello Oryem jana alisema hawakufahamishwa na ubalozi wa Kenya kwamba Dkt Ruto alistahili kuzuru taifa hilo mnamo Jumatatu.

Oryem pia alikanusha madai kwamba Rais Yoweri Museveni anaingilia siasa za Kenya kwa kuunga mkono Dkt Ruto.Mnamo Jumatatu, Dkt Ruto alizuiliwa kuelekea nchini Uganda kama alivyopanga.

Alilazimika kukaa katika uwanja wa ndege wa Wilson kwa muda wa saa tano, lakini mwishowe maafisa wa uhamiaji wakakataa kumruhusu kusafiri.

Lakini wabunge Oscar Sudi (Kapseret), Benjamin Tayari (Kinango) na Ndindi Nyoro (Kiharu) pamoja na wafanyabiashara wandani wake waliruhusiwa kusafiri hadi Uganda.

Dkt Ruto alisisitiza kuwa ziara yake ilikuwa ya kibinafsi, hivyo hakuhitajika kupata idhini kutoka kwa mtu yeyote.

“Hatukupokea ombi lolote kutoka kwa ubalozi wa Kenya la kututaka kutoa huduma za mapokezi kwa Dkt Ruto,” Bw Oryem aliambia gazeti la New Vision la Uganda.Bw Oryem alisema sera ya Uganda hairuhusu taifa hilo kuingilia siasa au masuala ya ndani ya nchi nyingine.

“Kenya inaongozwa na kiongozi aliyechaguliwa, Rais Uhuru Kenyatta na anafanya kazi nzuri na hakuna sababu yoyote ya Uganda kuingilia siasa za majirani wetu. Hatuna mamlaka ya kuingilia masuala ya Kenya na wao ndio wanajua kwa nini walimzuia Ruto kuja Uganda,” akasema.

Jana alipokuwa akihutubia wanahabari baada ya kukutana na wabunge wanaomuunga mkono, Dkt Ruto alikataa kuzungumzia ziara yake nchini Uganda.Mnamo Jumatano alisema kwamba Rais Museveni ni rafiki yake.

“Ni kweli kwamba Museveni ni rafiki yangu. Nimewahi kumfanyia kampeni. Na viongozi wote wa Nasa pia wamewahi kumfanyia kampeni. Sasa ikiwa yeye ni rafiki wa wote, mbona kuna shida kubwa ikiwa nitamtembelea kiongozi huyo?” akauliza.

Wandani wa Dkt Ruto wamefichua kuwa analenga kujumuisha washauri wa siasa wa Rais Museveni katika kikosi chake cha kampeni anapojiandaa kuwania urais 2022.

Bw Sudi aliambia Taifa Leo kuwa walienda Uganda kujifunza kutoka kwa chama tawala cha Uganda, Nation Resistance Movement (NRM) ambacho kimekuwa mamlakani kwa miaka 35 chini ya Rais Museveni.

Ufichuzi huo umezua mjadala mkali nchini, huku wanasiasa wa ODM wakidai kuwa Dkt Ruto anapanga kutumia NRM kusababisha machafuko nchini endapo atapoteza katika uchaguzi wa urais 2022.

You can share this post!

Mtangazaji wa zamani wa KBC Gladys Erude afariki

Ni kisasi, vita vya ubabe kati ya Faith na Hassan fainali...