Uganda yarukia EU kwa kutaka iwekewe vikwazo

Uganda yarukia EU kwa kutaka iwekewe vikwazo

Na MASHIRIKA

KAMPALA, Uganda

UGANDA imeukashifu Umoja wa Ulaya (EU) kwa kuingilia masuala yake ya ndani baada ya bunge la umoja huo kupendekeza iwekewe vikwazo kwa kuwadhulumu na kuwakamata wanaopinga ushindi wa Rais Yoweri Museveni katika uchaguzi uliofanyika Januari.

Rais Museveni, 86, ambaye amekuwa mamlakani tangu 1986 alipata asilimia 59 ya kura katika uchaguzi huo uliofanyika Januari 14 lakini mpinzani wake wa karibu Robert Kyangulanyi, almaarufu Bobi Wine, amepinga matokeo hayo.

Mnamo Alhamisi, Bunge la EU lilipitisha uamuzi uliosema kuwa uchaguzi huo haukuendeshwa kwa njia ya kidemokrasia likiongeza kuwa polisi na wanajeshi walitumia nguvu kupita kiasi.

Bunge hilo liliitaka serikali ya Uganda kuwaachilia huru wanasiasa na raia waliokamatwa kipindi cha uchaguzi huo.

“Kuuliza Uganda kuwaachilia washukiwa ambao tayari wako mbele ya mahakama ni sawa kuingilia kazi halali ya idara ya mahakama,” msemaji wa serikali Ofwono Opondo aliaambia shirika la habari la Reuters.

“Tunachukulia uamuzi wa bunge la EU dhidi ya Uganda kama usiozingatia usawa na ukweli. Hatujabaini nia ya uamuzi huo,” akaeleza.

Bw Wine amewasilisha kesi ya katika Mahakama ya Juu kupinga matokeo ya uchaguzi huo.

Wakati wa kampeni za kuelekea uchaguzi huo, maafisa wa usalama walisambaratisha mikutano ya kampeni ya Wine kwa kutumia vitoa machozi, risasi na kuwapiga wafuasi wake.

Serikali ilisema mikutano hiyo ilitibuliwa kwa sababu ilipangwa kinyume na kanuni za kuzuia msambao wa virusi vya corona huku ikiisuta kambi ya Wine kwa “kuhatarisha maisha ya wananchi.”

Karibu watu 54 waliuawa katika makabiliano kati ya wafuasi wa upinzani na maafisa wa usalama huku watu wengine 600 walitiwa mbaroni.

“Uchaguzi huo haukuendeshwa kwa njia ya kidemokrasia na uwazi,” likasema bunge la EU katika uamuzi wake.

Umoja huo ulilaani maafisa wa usalama kuwa kutekeleza vitendo vya ukatili na kuingilia shughuli za kisiasa huku ukiilamu serikali ya Uganda kwa kutumia Covid-19 kama kisingizio cha kuendeleza udhalimu.

“Sharti vikwazo viwekwe dhidi ya watu na asasi zilizohusika na uvunjaji wa haki za kibinadamu nchini Uganda,” wabunge kutoka mataifa 27 wanachama wa EU wakasema katika uamuzi huo.

Rais Museveni, 76, amekuwa mwandani wa mataifa ya Magharibi ambayo yamekuwa wakiipa Uganda misaada ya kifedha huku ikituma wanajeshi wake katika mataifa yanayokumba na misukosuko ya Sudan Kusini na Somalia.

Hata hivyo, kusalia kwake mamlakani kwa miaka mingi na mienendo yake ya kuwadhulumu wapinzani wake, imekasirisha mataifa hayo fadhili.

You can share this post!

UDA yapigwa jeki uchaguzi Matungu

Manchester City wakomoa Spurs na kuendeleza ubabe wao...