MakalaSiasa

UGATUZI: Hatari ya shughuli za kaunti kukwama

June 23rd, 2019 3 min read

Na CHARLES WASONGA

HUENDA shughuli katika serikali 47 za kaunti zikakwama kuanzia mwezi Julai ikiwa suluhu la mvutano kuhusu ugavi wa fedha kwazo halitapatikana Jumatatu.

Naibu Rais William Ruto anatarajiwa kuingilia kati suala hilo kwa kuongoza mkutano utakaowaleta pamoja wakuu wa bunge, Baraza la Magavana (CoG) na Tume ya Ugavi wa Mapato (CRA) afisini mwaka mtaani Karen, kusaka muafaka kuhusu suala hilo.

Bajeti ya kitaifa iliwasilishwa bungeni na Waziri wa Fedha Henry Rotich mnamo Juni 13 kabla ya kupitishwa kwa Mswada wa Ugavi wa Mapato (DORB) baada ya wabunge na maseneta kukosa kukubaliana kuhusu kiwango cha fedha zinapasa kutengewa serikali za kaunti katika mwaka wa kifedha wa 2019/2020.

Hii ni baada ya Kamati ya upatanisho ya wanachama wanane iliyobuniwa na Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi na mwenzake wa Seneti Kenneth Lusaka kuhitiliafia pale wabunge walipopendekeza kaunti zipewe Sh316 bilioni nao maseneta wakitaka Sh327 bilioni.

Hata hivyo, kwenye makadirio ya bajeti yaliyowasilishwa na Bw Rotich bungeni, Serikali za kaunti zimetengewa Sh310 bilioni, kiasi ambacho bunge la kitaifa na Hazina Kuu zilikuwa zimekubaliana kabla ya maseneta kuibua mapema mwezi Mei kabla ya maseneta kupinga kwa kupendekeza Sh335 bilioni.

Hii ndio maana mnamo Jumanne, alipoongoza kikao cha Baraza Shirikishi kuhusu Bajeti na Masuala ya Uchumi (Intergovernmental Budget na Economic Council-IBEC) afisini mwake mtaani Karen, Dkt Ruto aliahidi kufanya mazungumzo na uongozi wa bunge ili kukwamua mvutano huo kuhusu ugavi wa mapato.

Mkutano ulihudhuriwa na Waziri Rotich, wanachama wa CoG wakiongozwa na mwenyekiti wao Wycliffe Oparanya na mwenyekiti wa CRA Jane Karingai miongoni mwa wakuu wengine wa asasi husika za serikali.

“Huu mvutano kati ya wabunge na maseneta kuhusu kiasi cha pesa ambazo zinapasa kutengewa serikali za kaunti haupasi kuendelea kwani utaathiri shughuli za kaunti. Binafsi nitafanya mazungumzo na uongozi wa mabunge yote mawili kwa lengo la kupata suluhu la haraka kuhusu suala hili,” Dkt Ruto.

Mzozo huo umekwamisha shughuli za utayarishaji wa bajeti katika serikali zote 47 za kaunti na ikiwa hautatanzuliwa kufikia Juni 30, 2019, serikali hizo hazitapokea mgao wa fedha kutoka Hazina ya Kitaifa. Ina maana kuwa hazitaweza kuwalipa wafanyakazi kando na kutekeleza miradi kadhaa za maendeleo iliyoratibiwa kwenye mipango yao ya maendeleo.

Ndipo mwenyekiti wa CoG Bw Oparanya akaelezea haja ya mzozo huo kutatuliwa kwa haraka ili “kuokoa” serikali za kaunti dhidi ya kutumbukia katika mzozo wa kifedha.

Akihojiwa kwenye runinga ya NTV mnamo Alhamisi Gavana huyo wa Kakamega alionekana kutokuwa na imani kwamba Naibu Rais Dkt Ruto atafaulu kutatua mvutano huo kesho alipomwomba Rais Uhuru Kenyatta kuingilia kati mzozo huo.

“Tuna matumaini kwamba Rais Kenyatta akiingilia kati kutatua vita vya ubabe kati ya bunge la kitaifa na seneti kuhusu ugavi wa fedha kwa serikali za kaunti,” akasema.

Lakini kulingana na Bw Oparanya mageuzi ya Katiba kupitia kura ya maamuzi ndio yatatoa suluhu ya kudumu kwa suala hilo la mgao wa fedha kwa serikali badala ya kutegemea uamuzi wa wabunge na maseneta.

“Tunahitaji referenda kuamua jinsi fedha zitakuwa zikitengwa baina ya ngazi za Serikali ya Kitaifa na zile za Kaunti. Hatutaki kuwekwa mateka na wabunge ambao ni wazi kuwa wamekuwa wakishirikia na maafisa fulani wa serikali ya kitaifa kuhujumu ugatuzi,” anasema.

Lakini katika mahojiano na “Taifa Jumapili” kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa aliondoa hofu kuwa kutopitishwa kwa mswada wa ugavi wa rasimali kutazinyima serikali za kaunti pesa za kuendesha shughuli zao.

“Ningependa kuwahakikishia magavana kwamba wasiwe na hofu. Katiba na Sheria kuhusu Usimamizi wa Fedha (PFM Act) zinampa Waziri wa Fedha mamlaka ya kuzipa serikali za kaunti advansi ya angalua asilimia 50 ya mgao wao hata kabla ya kupitishwa kwa mswada wa ugavi wa rasimali. Pesa hizi il kugharamia mahitaji yao ya dharura kama vile ulipaji mishahara,” anasema Bw Duale ambaye ni Mbunge wa Garissa Mjini.

Hata hivyo, Bw Duale anasahau kuwa kisheria, serikali za kaunti zinapasa kutumia asilimia 70 ya fedha zinazopokea kutoka Hazina ya Kitaifa kwa shughuli za kila siku na asilimia 30 kwa miradi ya maendeleo.

Kwa hivyo, kimsingi hata ikiwa kaunti zitapewa advansi ya kima cha asilimia 50 pesa hizo hazitatosha kugharamia operesheni za kila siku huku miradi ya maendeleo ikikwama kabisa.

“Kauli ya Bw Duale haina msingi wowote. Anajaribu kuhalalisha mvutano kati wabunge kuhusu kiwango cha fedha ambazo zinapasa kupelekwa kwa kaunti, kitendo ambacho kinahujumu ugatuzi,” anasema mtaalamu wa utawala Barasa Nyukuri.

Kulingana na Bw Nyukuri, ambaye pia ni mchanganuzi wa masuala ya kisiasa anawaonya wabunge na maafisa wa serikali ya kitaifa kuhujumu ugatuzi kwa kupunguza mgao wa fedha kwa serikali za kaunti.

“Hii ni sawa na kuwanyima wananchi huduma na maendeleo katika ngazi ya mashinani, ilhali ni haki yao kikatiba. Mgao wa fedha kwa serikali za kaunti inapasa kuwa ukiongezeka kila baada ya mwaka sambamba na ungezeko la utajiri wa nchi,” akasema.

“Iweje kwamba serikali za kaunti zilipewa Sh314 bilioni katika mwaka wa kifedha lakini sasa kiasi hicho kipunguzwa hadi Sh310 bilioni kama ambavyo wabunge na maafisa wa Hazina ya Kitaifa wanapendekeza.?” akauliza Bw Nyukuri.