Ugavana wa Nairobi wazidi kukanganya

Ugavana wa Nairobi wazidi kukanganya

Na RICHARD MUNGUTI

KAUNTI ya Nairobi inaendelea kuzingirwa na mkanganyiko wa kiuongozi, baada ya mahakama kutoa mwanya unaoweza kutoa nafasi ya kuajiriwa kwa naibu gavana aliyekuwa ameteuliwa na gavana aliyebanduliwa, Bw Mike Sonko.

Mahakama Kuu mnamo Alhamisi ilifutilia mbali kesi iliyokuwa inapinga kuhojiwa kwa Bi Anne Kananu Mwenda ili awe naibu gavana.

Hatua hii sasa imezidi kuzua mjadala kuhusu hatima ya uongozi wa kaunti hiyo ambayo kwa sasa inasimamiwa na Spika wa Bunge la Kaunti, Bw Benson Mutura.

Sasa madiwani wako huru kumhoji Bi Mwenda, na akithibitishwa huenda akaapishwa kuwa Gavana wa Kaunti ya Nairobi.

Kesi iliyopinga mchakato huo ilikuwa imewasilishwa mahakamani na Bw Peter Odhiambo Agoro. Jaji Hedwiq Ong’udi alikubalia ombi la Bw Agoro kuondoa kesi.

Wiki iliyopita, mahakama nyingine ilikuwa imekubali ombi la Bw Sonko kutaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kusitisha mipango ya kuandaa uchaguzi mdogo wa ugavana kaunti hiyo.

Bw Mutura anatakikana kikatiba ahudumu kwa muda wa siku 60 pekee.

Katika kesi yake, Bw Agoro alikuwa amesema Bw Sonko hana mamlaka na uwezo kisheria na katiba kumteua naibu wake kwa vile amezuiliwa kutekeleza majukumu yake na Mahakama kuu baada ya kushtakiwa kwa ufisadi wa Sh350 milioni.

Alidai kwa vile Sonko alikuwa amezimwa kutekeleza majukumu yake uteuzi huo wa Bi Mwenda hautambuliki kisheria.

Endapo Bi Kananu atapitishwa, atakuwa Gavana wa nne mwanamke baada ya Charity Kaluki Ngilu (Kitui), Anne Waiguru (Kirinyaga) na aliyekuwa Gavana wa Bomet marehemu Joyce Laboso.

Jaji Ong’udi pia alitupilia mbali ombi la Josephat Kariuki Ng’endo ashirikishwe katika kesi ya Agoro.

“Wanaotaka kumshtaki Sonko wawasilishe kesi zao huru sio kunining’inia katika kesi za watu wengine,” akasema Jaji.

Kwingineko, afisa wa polisi aliyedaiwa kumuua mfanyabiashara ndani ya kituo cha polisi mnamo Desemba 30, mwaka uliopita ameomba mahakama izingatie kuwa hakukusudia kumuua rafiki yake.

Hakimu mkazi Bi Jane Kamau aliamuru Konstebo Edgar Mokamba afikishwe mbele ya Jaji Hedwiq Ong’udi leo kujibu shtaka la kumuua Zachary Makuto Simwa.

Wakili Danstan Omari anayemwakilisha Mokamba alieleza mahakama kuwa mshtakiwa amemsihi aombe msamaha familia ya marehemu kwa niaba yake kwa “vile hakumuua kwa kukusudia rafikiye wa chanda na pete. Ilikuwa bahati mbaya.”

Wawili hao walikuwa wanatafuta miraa ndani ya gari la marehemu la Probox ndani ya kituo cha polisi cha Nyari kilichoko Westlands Nairobi wakati milio ya risasi iliposikika ghafla. Polisi wengine walipofika pale wakampata mshtakiwa akiwa ameshtuka. Alishikwa na kuzuiliwa huku Makuto akifa papo hapo.

You can share this post!

KAMAU: Amerika sasa haina shavu kuzungumzia demokrasia

Trump kwisha!