Makala

Ugavi wa pesa kwa mujibu wa idadi ya watu kuumiza Mlima Kenya

January 7th, 2024 3 min read

NA MWANGI MUIRURI

BAADHI ya wanasiasa Mlima Kenya wamekuwa wakivumisha mjadala kwamba iwapo mfumo wa ugavi pesa za kitaifa ungezingatia idadi ya watu, basi wenyeji ndio wangevuna pakubwa.

Wakiongozwa na mbunge wa Githunguri Bi Gathoni wa Muchomba, kauli yao ni kwamba wenyeji wa Eneo la Kati huwa wanatekelezewa udhalimu katika ugavi wa vitita vya rasilimali mashinani.

Hata hivyo, kuna wataalamu wa masuala ya kifedha ambao wameonya eneo hilo kwamba huenda wapoteze pakubwa wakifikiria wanasaka maendeleo kwa wenyeji.

“Kuna ile kasumba inaongoza baadhi ya wanasiasa kwamba wakipiga domo kuhusu suala fulani lililopakiwa katika propaganda ya manufaa, basi watapata umaarufu. Lakini ukweli ni kwamba, iwapo mfumo wa ugavi raslimali utafuata idadi ya watu, basi Mlima Kenya hauko katika manufaa hayo yanayokadiriwa kisiasa,” akasema Bw Wanjumbi Mwangi ambaye ni mkurugenzi wa taasisi ya NewTimes inayotoa huduma za ushauri wa kifedha.

Anasema kwamba “Mlima Kenya hupata kwa kiwango kikuu pesa za miradi kama ujenzi wa barabara, miundombinu kama ya elimu na afya na pia maji kuliko wenzao wa kutoka maeneo ya Kaskazini Mashariki, Pwani na hata kwingineko kwingi”.

Bw Mwangi alisema “kwa mfano, Mlima Kenya wanapokezwa fatalaiza ya bei nafuu huku wengine Kaskazini Mashariki wakikosa afueni hiyo kwa kuwa hawashiriki kilimo. Basi inafaa hata hiyo ya fatalaiza tugawane na jamii za wafugaji na pia wanaoishi katika miji ili tuwe na usawa”.

Mshauri wa Rais William Ruto ambaye hujulikana na ukatili wake wa kunena ukweli kulingana na maoni yake, David Ndii, anasema kwamba mfumo huo wa ugavi pesa za ushuru kwa kuzingatia idadi ya watu hauna mwelekeo.

“Huo mjadala unalenga kuwapa kipau mbele walioendelea kitambo huku waliobaguliwa wakibakia nyuma hivyo basi kuondoa usawazishaji,” anasema Bw Ndii.

Alisema kwamba mjadala huo huongozwa na kasumba kwamba jamii za Mlima Kenya zinafaa kutunzwa kama wababe wa kila safu na katika hali hiyo kuwadhulumu wengine kwa kuwatenga na kuwabagua.

Ukiingia katika takwimu za idadi ya watu, utapata kwamba hata mfumo huo uamrishwe kuanza kutekelezwa sasa bila kuchelea, ni kaunti chache sana za Mlima Kenya zitanufaika huku zingine zikihitajika kupunguziwa mgao unaozifikia kwa sasa ili kusawazisha hali.

Kaunti ambazo zimefikisha idadi ya watu milioni moja na ambazo zinaweza kuibuka na mgao wa juu ni Nairobi ikiwa na watu 4.4 milioni, Kiambu ikifuata ikiwa na watu 2.4 milioni hivyo basi kukupa sababu ya Bi Wamuchomba kupigia debe mfumo huo kwa kuwa ni mbunge katika kaunti hii.

Nakuru inafuata kwa nafasi ya tatu ikiwa na watu 2.2 milioni nayo Kakamega ikifuata kwa watu 1.9 milioni.

Kaunti ya Bungoma ndiyo ya tano ikiwa na watu 1.7 milioni, ile ya Meru ikifuata kwa watu 1.56 milioni nayo ile ya Kilifi ikiwa ya saba kwa watu 1.5 milioni.

Kaunti ya Machakos ndiyo ya nane ikiwa na watu 1.4 milioni, ya Kisii ikiwa ya tisa kwa watu 1.3 milioni nayo Mombasa, Uasin Gishu, Narok na Kisumu zikifuata hadi usajili wa nambari 13 zikiwa na watu 1.2 milioni kila moja, nazo Migori, Murang’a, Homabay, Kitui na Kajiado zikifuata kwa kuwa na watu 1.1 milioni kila moja.

Kati ya kaunti hizo 18 zilizo na watu milioni moja kwenda juu, ni tatu pekee zilizopo Mlima Kenya.

Ina maana kwamba walio eneo hilo kando na kaunti za Murang’a, Kiambu na Meru na wanasukuma mjadala wa ugavi pesa kwa kuzingatia idadi ya watu, basi wanapigia debe kupunguzwa kwa hazina zinazotumwa kwa maeneobunge yaliyoko katika kaunti kama Kirinyaga, Nyeri, Nyandarua, Laikipia, Embu na Tharaka Nithi.

“Tunafaa tumakinike katika suala hili. Iwapo tutasema hazina kama ya maeneobunge izingatie idadi ya watu, maeneo ya Mlima Kenya yatapunguziwa mgao ili ukafae wanaowazidi kwa idadi na hiyo ni njia moja ya kuzua mtafaruku mkuu wa kisiasa na kiuchumi,” anasema Bw Wanjumbi Mwangi, akiongeza kwamba kitaifa, mfumo huo utadhulumu kaunti 29.

Hata Murang’a ambayo husemwa inaweza ikanufaika na mjadala huo, maeneobunge kama ya Kangema na Mathioya hupendekezwa yaunganishwe au yakingwe kisheria yabakie tu kwa kukosa idadi tosha ya watu kwa mujibu wa sheria ya kuwa eneobunge.

Kaunti ya Nyeri ina watu 759, 000, Nyandarua ikiwa na watu 638, 000, Embu 609, 000, Kirinyaga 610, 000, Laikipia nayo ikiwa na watu 519, 000, huku ile ya Tharaka Nithi ikiwa na watu 393, 000.

Seneta wa Nyandarua Bw John Methu aliteta katika runinga ya Inooro kwamba “huu mjadala hauna mashiko kamwe na tunapaswa tuuweke kando kwanza ili tusake mdahalo mbadala ambao utatupa matokeo pasipo kujivuruga na kujikanganya”.

Alisema kwamba “huu mjadala unatuzungusha tu kisiasa, huku wengine wakizingatia manufaa ya vijiji vyao lakini sio utaifa na jinsi ya kutuunganisha na kutusawazisha kama taifa”.

Mwaka wa 2016 Gavana wa sasa Kiambu Bw Kimani Wamatangi wakati huo akiwa Seneta aliwasilisha kesi kortini akitaka mfumo wa kuzingatia watu kwa kugawa pesa uanze kutekelezwa.

“Kesi hiyo ilikuwa nambari 163 ya 2016 mbele ya Jaji Joseph Ongutu lakini sikuwa nimeipamba kama ya kutufaa sisi tu wa Mlima Kenya, lakini kama taifa zima…” akasema.

Hata hivyo, inaibuka sasa msukumo wake hasa ulikuwa wa kufahamu kwamba Kaunti ya Kiambu ingevuna pakubwa na akilenga kuwania ugavana 2022, ajipate guu mbele.

[email protected]