Habari Mseto

Ugomvi wa penzi wazua mauti ya mtoto

November 19th, 2018 1 min read

Na MACHARIA MWANGI

MZOZO wa kimapenzi baina ya watu wawili katika eneo la Naivasha, Kaunti ya Nakuru, uliishia katika mauti baada ya mwanaume kumdunga kisu hadi kufa mtoto wa mpenzi wake mwenye umri wa miaka mitano.

Tukio hilo la Jumamosi katika Kijiji cha Karagita liliwaacha wengi katika mshangao, wakati mwanaume huyo alipovamia nyumbani kwa mpenziwe mwendo wa saa moja jioni, mpenziwe huyo pamoja na wanawe wawili walipokuwa wamelala.

Bi Susan Wangari, jirani yao alisema kuwa mwanaume huyo, ambaye anasemekana kuwa na historia ya kufungwa jela, alikuwa amebeba kisu na alijaribu kumvamia mpenzi wake lakini pamoja na mwanawe wa miaka 13 wakafanikiwa kutoroka.

“Walipotoroka, aliangushia ghadhabu zake mtoto mdogo aliyesalia ndani ya nyumba, akamdunga kisu mara tatu wakati mama na mtoto mkubwa kutaka msaada,” akasema Bi Wangari. Baada ya kumdunga, dadake mtoto huyo anadaiwa kuingia ndani ya nyumba na kumbeba kakake hadi hospitalini lakini walipofika, akawa amekufa tayari.

Majirani nao walifika mara moja na kwa hasira wakataka kumuua, lakini alipoona hatari aliyokumbana nayo, mshukiwa akajiua kwa kutumia kisu hicho.

“Alijua kuwa umma ulikuwa unataka kumuua ndipo akaamua kujiangamiza yeye mwenyewe,” akasema jirani huyo.

Taifa Leo ilibaini kuwa mwanaume huyo alikasirishwa na hatua ya mpenzi wake kuamua kumaliza uhusiano baina yao, baada ya mwanamke huyo kumlaumu kuwa alikuwa na tabia za kuzua fujo.

Naibu kamishna wa eneo la Naivasha Janet Mlongo alisema kuwa polisi walishuku mwanaume huyo alichukua hatua hiyo baada ya kuona ameshindwa kupata penzi la mwanamke huyo.

“Alikuwa amelenga kumvamia aliyekuwa mpenzi wake lakini akaelekeza hasira kwa mtoto baada yake kutoroka,” akasema afisa huyo.

Bi Mlongo alisema kuwa mwanaume huyo, ambaye ana jina la utani ‘Nyoka’ alitoka jela miezi miwili iliyopita.

Mili yote miwili ilipelekwa hifadhi ya maiti ya hospitali ya Naivasha.