SHINA LA UHAI: Ugonjwa wa MS hauna tiba lakini waweza kudhibitiwa

SHINA LA UHAI: Ugonjwa wa MS hauna tiba lakini waweza kudhibitiwa

NA PAULINE ONGAJI

NI miaka 11 tangu Caroline Mutinda, 34, mkazi wa jiji la Nairobi agundulike ana Mulitiple Sclerosis-MS, ambapo safari yake katika harakati za kupambana na maradhi haya, haijakuwa rahisi.

Kila siku Bi Mutinda ambaye ni afisa wa ushuru, hupambana na ishara kali zinazotokana na hali hii.

“Mbali na uchovu na maumivu ya sehemu mbalimbali za mwili wakati tofauti, siwezi keti kwa muda mrefu kwani nitahitaji usaidizi kusimama, na nikisimama kwa muda mrefu, pia nitahitaji usaidizi kusonga hatua chache za kwanza kabla ya kutembea mwenyewe,” aeleza.

Aidha, hawezi shika kalamu na yeye pia hupooza kila mara.

“Kupooza kwangu hubadilika kila baada ya kati ya miezi mitatu na sita. Kwa kawaida, sehemu moja hupooza kisha inaacha kabla ya nyingine kuathirika. Kwa sasa mkono wangu wa kulia na miguu yote miwili imepooza,” aeleza.

Ili kudhibiti maradhi haya, kila Ijumaa yeye hutumia Sh15,360 kugharimia dawa.

“Nimebahatika kwamba licha ya matatizo ya kimwili ninayokumbana nayo, bado nina ajira na kupitia bima ya mwajiri naweza mudu matibabu haya,” aeleza.

Bi Mutinda alianza kushuhudia ishara za maradhi haya mwaka wa 2011, lakini ilikuwa changamoto kwa hospitali alizozuru kuanza kumpa matibabu kwani madaktari hawakujua alichokuwa anaugua.

Caroline Mutinda, 34, mkazi wa jiji la Nairobi aligundulika ana Mulitiple Sclerosis-MS. Hapa alikuwa akifanya mahojiano Juni 18, 2022 katika Nation Centre, Nairobi. PICHA | JEFF ANGOTE

Alianza kwa kupooza upande mmoja wa uso, hangeweza konyeza jicho, kisha mdomo wake ukasonga na kwenda kombo.

“Nilifanyiwa uchunguzi wa kila kitu lakini madaktari hawakuweza kutambua nilikuwa naugua maradhi yapi. Mara nyingi madaktari wangemwambia babangu anirejeshe nyumbani, na kupendekeza niwe nikienda hospitalini ili kufanyiwa tibamaungo,” aeleza

Baada ya kujaribu kutafuta matibabu bila mafanikio, mwaka wa 2012 babake aliamua kubadilisha hospitali, na ni hapa ndipo waligundua anachougua.

“Matibabu yalianza mara moja ambapo mwanzoni nilianza kwa kupewa kemikali za steroidi kutoka India, kisha nikalazwa hospitalini. Hata hivyo hali yake ilizorota na madaktari wakalazimika kunibadilishia dawa na hizo ndo natumia hadi sasa,” aeleza.

Dawa hizi anazodungwa kila siku sio tiba ya maradhi haya, bali zinadhibiti ishara kali zinazojitokeza kutokana na ugonjwa huu.

Maradhi ya MS huharibu neva na kusitisha mawasiliano kati ya ubongo na mwili na huwa na ishara kama vile kupoteza uwezo wa kuona, maumivu, uchovu na matatizo ya misuli kupatana.

Takwimu za shirika la Afya Duniani- WHO zaonyesha kwamba takriban watu milioni 2.8 duniani wanaugua MS. Hii ni sawa na watu 35.9 kwa kila idadi ya watu 100,000.

Utafiti uliochapishwa Novemba mwaka wa 2020 katika wavuti wa National Library of Medicine, maktaba makubwa zaidi ya masuala ya kimatibabu nchini Amerika, ulionyesha kwamba idadi ya watu wanaougua MS imeendelea kuongezeka katika mataifa yote wanachama wa Shirika la Afya Duniani, kuanzia 2013 hadi 2020.

Hapa nchini, takwimu rasmi za maradhi haya bado hazijulikani kwani Kenya bado haina vifaa, teknolojia na wataalamu wa kutosha kufanya utambuzi wa mapema.

Dkt Thomas Kwasa, mtaalamu wa nyurolojia na mhadhiri mkuu katika Chuo Kikuu cha Nairobi, asema ishara na ukali wa dalili zake huwa tofauti kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine.

“Kuna wagonjwa ambao wataonyesha ishara ambazo zinafanana na matatizo mengine ya kinyurolojia, na hivyo itamchukua daktari muda kabla ya kuthibitisha kwamba kwa kweli ni maradhi haya,” aeleza.

Hii asema ni mojawapo ya sababu ambazo zatitiza utambuzi wa mapema.

“Huu ni ugonjwa ambao unajumuisha mchanganyiko wa ishara mbalimbali, kumaanisha kwamba itakuwa vigumu kwa daktari kutathmini mara moja, ” asema.

Aidha, anasema tatizo lingine ni kwamba ugonjwa huu ni adimu sana hapa nchini.

“Haya ni maradhi ambayo kwa muda mrefu yalikuwa yamekithiri tu katika mataifa ya Magharibi na wala sio maeneo ya tropiki kama Afrika, Kenya ikiwemo. Kwa mfano, miaka kumi iliyopita, tulikuwa na wagonjwa watano pekee nchini. Lakini miaka inavyozidi kusonga, idadi hii iinaendelea kuongezeka, ingawa hakuna takwimu za kuonyesha idadi kamili ya waathiriwa,” aeleza.

Anasema hii imekuwa changamoto hata zaidi hasa mgonjwa anapoenda kwa wahudumu au madaktari ambao sio wataalamu wa nyurolojia.

“Hii inamaanisha kwamba mgonjwa atafanyiwa chunguzi kadhaa na kutumwa kwa madaktari kadhaa pasipo kiini haswa kutambuliwa, na tena gharama iko juu. Kwa upande mwingine, ukienda kwa mwananyurolojia kwa mara ya kwanza, atafanya chunguzi chache kabla ya tatizo kutambulika,” aeleza.

Dkt Kwasa anasema kuna tiba kadhaa ambazo hutumika kudhibiti ishara zake.

“Hasa sisi hutumia kemikali za steroidi kama mbinu nafuu ya kukabiliana na dalili kali, kisha baada ya kati ya siku tatu na tano, mwathiriwa atakuwa sawa kuendelea na shughuli zake za kawaida. Lakini hii sio tiba,” aeleza.

Kwa upande mwingine, asema, kuna dawa za kisasa kwa jina disease modifying drugs za kukabiliana na maradhi haya ambazo ni ghali lakini ni thabiti.

“Hapa mgonjwa anaweza kutumia kati ya Sh500,000 na Sh1m kwa dozi ya siku tano,” anaongeza.

  • Tags

You can share this post!

Afueni ya bei ya mafuta yanukia Agosti

MUME KIGONGO: ‘Magonjwa ya wanawake’ ambayo...

T L