UGUMU WA MAISHA KUZIDI OKTOBA

UGUMU WA MAISHA KUZIDI OKTOBA

Na PETER MBURU

HALI ngumu ya maisha inawasubiri Wakenya siku chache zijazo, wakati serikali, kwa mara nyingine, itakapopandisha ushuru wa baadhi ya bidhaa muhimu zinazotumiwa kila siku.

Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA) tayari imetangaza kuwa kuanzia Oktoba 1, ushuru wa bidhaa kama mafuta, vinywaji aina ya juisi, maji na pombe za aina tofauti, sukari, pikipiki na bidhaa nyingine utapandishwa.

Kulingana na KRA, hatua hii itachukuliwa kutokana na mfumko wa bei ulioshuhudiwa katika mwaka wa kifedha wa 2020/21, uliopanda kwa asilimia 4.97.

“KRA inaarifu watengenezaji na wanunuzi kutoka nje ya nchi wa bidhaa husika, na Wakenya kuwa Kamishna Jenerali atapandisha ushuru kulingana na hali ya mfumko wa bei mwaka wa fedha 2020/21 wa asilimia 4.97 kulingana na Shirika la Takwimu Nchini (KNBS),” KRA ikasema Agosti 10, kupitia tangazo kwa umma.

Endapo Waziri wa Fedha, Ukur Yatani atapitisha mapendekezo hayo ya KRA, bei za bidhaa 34 zitapanda kwa viwango tofauti, kufuatia kupandishwa kwa ushuru aina ya Excise Duty- ambao hutozwa bidhaa zinapotengenezwa, kupewa leseni na kuuzwa.

Wafanyabiashara wanaonunua sukari kutoka nje ya nchi kuanzia Oktoba 1 watalazimika kulipia ushuru wa Sh1.74 zaidi kwa kila kilo ya sukari, kutoka ushuru wa Sh35 wanazolipa kwa sasa. Hii ni kumaanisha kuwa ushuru wa kilo ya sukari utapanda hadi Sh36.74 kwa kilo.

Kwa sasa, bei ya sukari nchini ni kati ya Sh102 na Sh115 kwa kilo -kwa wastani- na hivyo kupandishwa kwa ushuru wa bidhaa hiyo kunatarajiwa kuongeza bei.

Watumizi wa maji ya kunywa ambayo hupakiwa kwa chupa ama vifaa vingine, aidha watakuwa na wakati mgumu kwani serikali imepanga kupandisha ushuru wa bidhaa hiyo muhimu kwa uhai, kutoka Sh5.74 kwa kila lita ya maji hadi Sh6.03.

Hii ni mbali na vinywaji vyote vya pombe ambavyo pia ushuru wake utapanda kwa kati ya Sh5 na Sh13 kulingana na aina ya kinywaji husika, hali itakayopelekea kupanda kwa bei ya pombe wiki chache tu baada ya baadhi ya wauzaji kupandisha bei.

Baada ya kuongeza bei ya pombe aina tofauti mnamo Juni, Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya EABL, Jane Karuku alisema kuwa alitarajia mauzo yake kushuka, kutokana na ugumu wa maisha ambao unaendelea kuwakumba Wakenya wengi.

Mbali na pombe, mafuta, ambayo bei yake ilipandishwa kwa zaidi ya Sh7 na mamlaka ya kusimamia sekta ya kawi na mafuta nchini (Epra) mnamo Jumanne, na kufikisha bei yake hadi zaidi ya Sh147 katika baadhi ya maeneo nchini, pia yanatarajiwa kuathirika na ushuru mpya unaozinduliwa Oktoba 1.

Ushuru wa Petroli utapanda kwa Sh1.091 kwa kila lita, Mafuta taa – ambayo hutumiwa na familia nyingi maskini nchini kwa upishi na mwangaza – kwa Sh0.565 kwa lita, na Diseli- ambayo mbali na magari makubwa ya kusafirisha bidhaa pia hutumiwa na mashine katika viwanda kuwezesha utengenezaji wa bidhaa – kwa Sh0.2 kwa lita.

Mbali na usafiri, mafuta pia hutumika katika sekta tofauti za kiuchumi kama usafirishaji wa bidhaa, na bei yake inapopanda gharama ya usafiri hupanda, na mwishowe kupandisha bei ya bidhaa.

Watumizi wa vinywaji aina ya juisi na chokoleti pia wanakumbana na wakati mgumu kwani bidhaa hizo ziko kwenye orodha ya zile zitakazoongezewa ushuru. Ushuru wa juisi za matunda utapanda kutoka Sh11.59 kwa lita hadi Sh12.17, huku wa chokoleti ukipanda kutoka Sh209.88 kwa kilo hadi Sh220.31.

Sekta ya bodaboda nchini ambayo imeajiri maelfu ya vijana nayo pia inakabiliwa na ugumu huo kwani ushuru wa pikipiki unatarajiwa kupanda kutoka Sh11,608.23 unaolipwa kwa sasa, hadi Sh12,185.16.

Kupandishwa kwa ushuru huo kunaweza kuwa na matokeo kama vile baadhi ya watu kushindwa kununua pikipiki na hivyo kuzuia uwezekano wa kupanua uchumi kwa kutoa nafasi za ajira. Ikizingatiwa kuwa sekta hiyo pia imeathirika na kupandishwa kwa bei ya mafuta, itakuwa pigo maradufu.

Nao waraibu wa sigara pia wanasubiriwa na balaa hilo kwani ushuru wa bidhaa hiyo utapanda kwa hadi zaidi ya Sh2,000 kwa kilo. Kwa sasa, bei ya wastani ya bidhaa hiyo sokoni ni kati ya Sh200 na Sh280 kwa kilo, kulingana na aina ya sigara husika.

Kwa kawaida, serikali inapopandisha ushuru wa bidhaa tofauti, wafanyabiashara hulipiza kwa kuongeza bei ya bidhaa hizo hata zaidi ya ushuru ulioongezwa, na hivyo hali hii inatarajiwa kujirudia na kuumiza raia wengi.

Wakenya walipaswa kuwasilisha maoni yao kuhusu pendekezo la KRA kupandisha ushuru huo kufikia Septemba 13.

Tayari Wakenya wa ngazi mbalimbali wamekuwa wakilalamika kuhusu gharama ya juu ya maisha, wakati wengi bado wanateseka kutokana na madhara yaliyoletwa na janga la Covid-19.

Baadhi ya mashirika ambayo yamekosoa hatua ya serikali kupandisha ushuru wa mafuta na bidhaa nyingine ni muungano wa watumiaji bidhaa nchini (Cofek), Muungano wa Watengenezaji Bidhaa (KAM), Muungano wa Wafanyabiashara katika Sekta ya Kibinafsi (Kepsa) na Muungano wa Vyama vya Wanyakazi (Cotu).

“Matokeo itakuwa kupanda kwa bei za bidhaa za kawaida ambazo hutumiwa na watu wengi na kupanda kwa gharama ya maisha kijumla,” akasema Bi Carole Kariuki, Afisa Mkuu Mtendaji wa Kepsa baada ya kupandishwa kwa bei ya mafuta

You can share this post!

Muturi atoa ishara anaelekea kwa Ruto

Mtoto aibwa mchana punde baada ya kuzaliwa