Habari Mseto

Uhaba wa mafuta JKIA wapeleka ndege nchi jirani

March 9th, 2019 2 min read

Na GERALD ANDAE
NDEGE ambazo huhudumu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) Alhamisi zililazimika kwenda katika viwanja vingine katika mataifa jirani kutafuta mafuta, wakati bidhaa hiyo katika uwanja wa JKIA ilipungua na kukaribia kuisha.
Upungufu huo wa mafuta ambao unatarajiwa kuendelea hadi Jumapili, unasemekana ni kutokana na uhaba wa bidhaa hiyo kutoka kwa kampuni ambazo huuzia kampuni za ndege mafuta moja kwa moja.
Mnamo Alhamisi, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Angani Nchini (KCAA) Gilbert Kibe alisema kuwa mafuta yaliyoagizwa yalikuwa yamewasili katika bandari la Mombasa na kuwa yangesafirishwa hadi Nairobi.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa shughuli za kawaida sasa zinatarajiwa kurejelewa kufikia Jumapili, Machi 10, 2019.
“Tumefahamisha kampuni za ndege na zinafahamu kuwa tunakumbana na hali hiyo ya upungufu kwa sasa,” akasema Bw Kibe.
Ndege aina ya MS850 ambayo ilikuwa ikisafiri kuelekea Jijini Cairo, Misri ililazimika kutua uwanja wa kimataifa wa Entebbe, Uganda kupokea mafuta Alhamisi, wakati ilipungukiwa ikiwa hewani.
Ndege hiyo ilikuwa imeondoka Jijini Nairobi saa kumi alfajiri na ilifaa kufika Cairo saa mbili asubuhi, lakini ikachelewa kwa saa tatu kutokana na hali ya kutua Entebbe.
Kampuni ya ndege ya mizigo ya Nairobi Astral Aviation, nayo ilienda Juba-Sudan Kusini, Mogadishu-Somalia na Djibouti kupata mafuta, wakati ndege zingine ambazo zilikuwa zikitoka bara Uropa zililazimika kwenda hadi Tanzania kutafuta bidhaa hiyo.
“Upungufu wa mafuta ya ndege uliopo JKIA sasa umefanya shughuli za ndege kupata mafuta kutafutwa mataifa jirani,” akasema meneja wa mauzo kampuni ya Astral Aviation Mstwafa Murad.
Alisema kuwa upungufu huo umefanya ndege kununua mafuta kwa bei ghali katika viwanja vya ndege vya mataifa jirani, ambapo zinalazimika kuyanunua.
Katika uwanja wa Entebbe, mafuta ya jeti yanauzwa senti 1200 zaidi ya Nairobi, Mogadishu senti 3800 zaidi, Kilimanjaro senti 1400 zaidi na Juba senti 3000 zaidi.
Mwenyekiti wa kampuni ya Kenya Airways (KQ) Michael Joseph, hata hivyo, alisema kampuni hiyo bado haijaathirika na upungufu huo.
“Bado tutakuwa na mafuta ya kutosha hadi Jumapili wakati shughuli za kawaida zitarejelea katika uwanja wa JKIA,” akasema Bw Joseph.
Mafuta katika uwanja wa JKIA yangeisha kabisa Alhamisi, lakini mgomo wa wafanyakazi wa KAA ukasaidia hali.
Lakini shughuli ziliporejelewa kwa hali ya kawaida, mafuta yaliyokuwa yamesalia yalitumiwa.
Kampuni ya Kenya Pipeline (KPC) ambayo husafirisha mafuta ya ndege ilikuwa imeonya kuwa ni lita milioni kumi pekee zilizokuwa zimesalia, ikilinganishwa na lita milioni 2.5 ambazo hutumika kila siku.
Lita milioni 115 za mafuta ziliwasili bandari ya Mombasa Jumanne na yakaanza kusafirishwa jioni yenyewe kuelekea Nairobi.
Upungufu huo aidha umeathiri uwanja wa ndege wa Moi, Jijini Mombasa.