Habari Mseto

Uhaba wa mahindi magharibi mwa nchi

July 26th, 2019 2 min read

Na WAANDISHI WETU

UHABA mkubwa wa mahindi umeripotiwa katika sehemu kadha za Magharibi mwa Kenya, hali inayoathiri shughuli za kampuni za kusaga nafaka hiyo kupata unga.

Upungufu huo umeripotiwa katika kaunti za Busia, Kisii na Homa Bay ambako maghala ya Bodi Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB) yanauza mahindi kwa vipimo kwa wasagaji unga pekee.

Kampuni ya Western Delux Maize Millers, iliyoko katika kaunti ya Busia, ambayo huzalisha unga wa mahindi chapa Halisi, imesitisha shughuli zake kutokana na uhaba wa mahindi.

Inadaiwa kuwa, baadhi ya wakulima wanahodhi mahindi, wakihofia kuwa uhaba mkubwa wa mahindi utashuhudiwa miezi ijayo kwa sababu ya mvua chache iliyonyesha wakati wa msimu wa upanzi.

Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo John Kariuki aliambia Taifa Leo kwamba, hawajapokea mahindi kwa kipindi cha wiki mbili, ilhali kampuni hiyo ina uwezo wa kusaga magunia 1000 ya mahindi kwa siku.

“Stoo zetu ni tupu kwa sababu hatujapokea mahindi kwa muda wa wiki mbili zilizopita. Hali hii imetulazimu kupunguza shughuli na hata kuwaagiza baadhi ya wafanyakazi wakae nyumbani kwa muda,” akasema.

Akaongeza: “Serikali inafaa ituruhusu kuagiza mahindi kutoka mataifa wanachama wa Muungano wa Soko la Pamoja Kusini na Mashariki mwa Afrika (COMESA) ikiwa haitaagiza mahindi kutoka mataifa ya mbali kama Mexico.”

Bw Kariuki amelalamika kuwa wanaendelea kupata hasara.

Katika kaunti ya Homa Bay, NCPB imesimamisha uuzaji wa mahindi kwa watu binafsi isipokuwa kampuni za usagaji pekee.

Wakati huu kuna magunia 11,926 ya kilo 50 ya mahindi katika ghala la bodi hiyo mjini Homa Bay.

Meneja wa ghala hilo Ben Abongo alisema, walipokea mahindi hayo kati ya Januari na Machi mwaka huu.

“Magunia tuliyo nayo ni machache na hofu yetu ni kwamba, hayawezi kufikisha mwezi ujao kwa sababu ghala la Kendu Bay halina mahindi. Hii ina maana kuwa, kampuni zote za usagaji zinanunua kutoka hapa,” akasema Bw Abongo.

Bei yapanda

Wakati huo huo, bei ya gunia moja la mahindi imepanda hadi Sh3,500 kulingana na wafanyabiashara tuliozungumza nao jana.

“Mnamo Januari mwaka huu gunia hilo moja liliuzwa kwa kati ya Sh1,500 na Sh2,000,” akasema mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara Mjini Homa Bay, Geoffrey Onduso.

Katika kaunti ya Kisii bei ya mahindi makavu imepanda na kupelekea wafanyabiashara kuamua kuagiza bidhaa hiyo kutoka Rift Valley.

Bei ya gunia moja la mahindi imepanda kutoka Sh4,200 hadi Sh4,800 katika kipindi cha miezi miwili iliyopita. Na bei ya mkebe wa kilo mbili imeongezeka kutoka Sh105 hadi Sh120.