Makala

Uhaba wa maji huenda ukatumbukiza dunia kwa machafuko – Ripoti

March 27th, 2024 2 min read

NA MARY WANGARI

UHABA wa maji unaozidi kuongezeka huenda ukachochea uhasama mkubwa baina ya wanajamii na kuvuruga amani barani Afrika na duniani kwa ujumla, ripoti mpya imeonya.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa(UN) iliyochapishwa mnamo Machi 22, 2024, imeelezea wasiwasi kuhusu uwezekano wa amani kuvurugika na ulimwengu kutumbukia kwenye machafuko kutokana na migogoro ya watu kung’ang’ania vyanzo vichache vya maji.

Kwa sasa, watu 3.5 bilioni kote duniani hawawezi kupata maji safi na salama kwa afya.

Aidha takriban watu 2.2 bilioni wanahangaika kupata maji salama jinsi inavyoashiriwa na Ripoti ya UN kuhusu Maendeleo ya Maji Duniani 2024.

Ulimwengu sasa upo kwenye njia panda huku ukikabiliwa na majanga ya mafuriko na maporomoko kwa upande mmoja na kero ya uhaba wa maji inayowaandama nusu ya binadamu duniani kwa upande mwingine.

Ripoti hiyo yenye anwani ‘Kutumia Maji kwa Amani’ inaashiria kuwa karibu nusu ya watu duniani walikabiliwa na uhaba wa maji kwa kipindi kirefu mwaka 2022 huku watu robo nyingine wakihangaishwa na masaibu ya kukosa maji.

Mataifa yaliyoathirika yaligeukia kutumia zaidi ya asilimia 80 ya chemchemi zao za maji kila mwaka, inasema ripoti hiyo.

Watu zaidi ya 1.4 bilioni waliathiriwa na kiangazi kati ya 2002 na 2021, kwa mujibu wa Mwenyekiti wa UN kuhusu Maji, Alvaro Lario.

Makali ya kukosekana kwa maji yameshuhudiwa zaidi katika mataifa maskini hasa barani Afrika ambapo sehemu kubwa ya kazi (asilimia 80) hutegemea maji ikilinganishwa na asilimia 50 katika mataifa tajiri.

Ripoti hiyo imetaja uhamiaji mijini, mabadiliko ya mtindo wa maisha na ulaji, ongezeko la idadi ya watu na maendeleo ya kiuchumi kama baadhi ya masuala ambayo yamechangia kuongezeka kwa ukosefu wa maji barani Afrika.

“Mataifa mengi Afrika yameathiriwa mno na ukosefu wa maji kwa shughuli za kiuchumi, hali inayozoroteshwa zaidi na miundomsingi duni, isiyofaa au hata miundomsingi kukosekana kabisa. Pia tatizo jingine ni kukosa kudhibiti rasilimali za maji na ukosefu wa fedha,” inasema ripoti.

Shirika hilo limetoa wito kwa mataifa kuimarisha mikataba ya mipaka baina ya mataifa na ushirikiano kimataifa likisisitiza kuwa kuwepo maji safi ni muhimu katika kudumisha amani duniani.

“Acha tuseme wazi, hali hii huenda ikazua balaa katika jamii yetu. Ikiwa binadamu watakabwa na kiu, masuala nyeti kama vile elimu, afya na ustawishaji wa maendeleo yatasahaulika na kufunikwa na juhudi za kila siku za kutafuta maji.”

“Kwa sababu hii, kwa miaka mingi mchakato wa kudhibiti maji aghalabu umekuwa chanzo cha ushirikiano badala ya migogoro. Kutambua chemichemi zilizodhibitiwa vyema na kusambazwa kwa njia ya haki kama kiini cha amani.”

“Ripoti yetu ya 2024 inapatia kipaumbele ushirikiano kimataifa miongoni mwa suluhu zilizopendekezwa, kuambatana na kauli mbiu, Maji kwa Ufanisi na Amani.” Inajikita kwenye ukweli wa tangu mwanzo: mito, chemichemi, maziwa na vidimbwi vya maji havijui mipaka yoyote.”

[email protected]