Habari Mseto

Uhaba wa maji mitaa kadhaa Thika Road

October 24th, 2020 1 min read

Na SAMMY WAWERU

UHABA wa maji umeendelea kushuhudiwa katika mitaa kadhaa Thika Road licha ya muda wa notisi iliyotolewa na kampuni ya usambazaji maji Nairobi kuhusu usitishaji wa usambazaji wa raslimali hiyo muhimu kukamilika.

Mitaa inayoendelea kuathirika kukosa maji ni pamoja na Kasarani, Mwiki, Roysambu, Zimmerman na Githurai.

Juma lililopita, Oktoba 14, Nairobi Water & Sewerage Company, ilikuwa imetoa notisi ya usitishaji wa usimbazaji maji kati ya Alhamisi, Oktoba 15 hadi Ijumaa, Oktoba 16, 2020.

Mitaa iliyotajwa na kampuni hiyo kuwa ingekosa maji siku zilizoorodheshwa ni pamoja na Mlango Kubwa, South B na C, maeneo ya Viwandani, Huruma, Kariobangi, Pangani, Kayole, Komarockm mitaa iliyoko Thika Road ambayo ni Kasarani, Mwiki, Kahawa Sukari, garden Estate na Thome Estate.

Mitaa mingine iliyotajwa kukosa maji ni Mathare, Muthaiga, Karen, Kawangware, Lang’ata, Kibra, na baadhi ya sehemu Westlands, kati ya maeneo mengine.

“Tunaarifu wateja wetu kuwa tutafunga kituo cha kutibu maji cha Ng’ethu kati ya Alhamisi, Oktoba 15, 2020 kuanzia saa kumi na mbili za asubuhi hadi Ijumaa, Oktoba 16, 2020 saa kumi na mbili za jioni. Hatua hii itasaidia kutuwezesha kukarabati eneo la kutekea maji la Mwagu, Mto Chania, kufuatia msimu wa mvua fupi unaobisha hodi,” ikaeleza notisi ya kampuni hiyo.

Licha ya muda wa notisi ya ukarabati huo kukamilika, wakazi wa Zimmerman, Kasarani, Githurai, na Mwiki wanaendelea kukosa maji.

“Kwa sasa tunalazimika kununua maji, mifereji haina chochote. Mtungi wa lita 20 tunauziwa Sh20 na wachuuzi,” akasema Trizah Wanjiku, mkazi wa Zimmerman.

Wakazi wa maeneo yaliyoathirika, wanaiomba kampuni ya usambazaji maji Nairobi kuangazia changamoto hiyo, hususan kipindi cha virusi vya corona na ambacho kiwango cha usafi kinapaswa kuwa cha hadhi ya juu.