Habari Mseto

Uhaba wa maua Valentino ikijongea, kisa mbolea

February 8th, 2019 1 min read

Na BONIFACE MWANGI

UUZAJI maua ya Kenya kwa nchi za kigeni utatatizika wakati wa sherehe za siku ya wapendanao ya Valentino mwaka huu kwa sababu ya ukosefu wa mbolea ambayo bado imezuiliwa na serikali bandarini.

Zaidi ya tani 1,000 za mbolea ya Calcium Nitrate ambayo hutumiwa kwa upandaji maua bado imezuiliwa bandarini asasi za serikali zikisubiriwa kuidhinisha itolewe.

Kutokana na hali hii, inahofiwa kutakuwa na uhaba wa maua wakati wa sherehe hizo Alhamisi ijayo. Wakati huo huo, maua chache zitakazokuwepo zitaongezwa bei.

Jopo lililosimamiwa na Naibu Mkuu wa Utumishi wa Umma, Bw Wanyama Musiambo liliundwa ili kuhakikisha bidhaa halali pekee ndizo zinaidhinishwa kuingia kutoka nchi za kigeni kupitia bandarini.

Hii ilikuwa pia katika juhudi za kupambana na ufisadi.

Hata hivyo, shughuli ya kuidhinisha bidhaa kutoka bandarini imekuwa ikifanywa polepole na hivyo basi mbolea ya maua haijaruhusiwa kuingia katika soko mwaka huu.

“Tuna wasiwasi sana kwa jinsi jopo hilo linafanya polepole kuruhusu mizigo iondoke bandarini. Shida hii haidhuru wakulima wa maua pekee bali pia sekta nyinginezo,” akasema Bw Eustace Muriuki ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Mbolea Kenya.

Alisema mbolea imekuwa bandarini kwa zaidi ya miezi minne akaomba serikali ipitishe mikakati mingine ambayo itasaidia kuharakisha shughuli katika bandari.

Kulingana naye, wafanyabiashara wa mbolea hupewa vyeti vya kuthibitisha wanafanya biashara halali na wamefuata sheria kuhusu uagizaji mbolea kutoka nje ya nchi ilhali bado wanahitajika kupitia mfumo mwingine tena kuthibitisha kile ambacho tayari kimeidhinishwa.

Biashara ya maua ni mojawapo ya zile zinazoletea nchi mapato mengi zaidi ya kigeni kila mwaka.