Uhaba wa mboga dukani ulimpa kichocheo cha kujitosa katika kilimo-biashara

Uhaba wa mboga dukani ulimpa kichocheo cha kujitosa katika kilimo-biashara

Na SAMMY WAWERU

FEBRUARI 2020 Edward Kagwamba alizuru duka moja lililoko Karen, jijini Nairobi kununulia familia yake chakula na bidhaa nyinginezo kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.

Kagwamba anasema familia yake inapenda sana mboga na mazao ya kutoka shambani.

“Mke wangu anapenda mboga, na ni yeye huhakikisha mboga ni kati ya chakula kiamsha kinywa,” asema Kagwamba ambaye ni baba wa watoto watatu.

Baada ya kukagua rafu zote, alipigwa na butwaa kwa sababu hakuona sukumawiki, spinachi wala mboga za kienyeji.

“Niliulizia mboga ya saladi (lettuce) nayo pia haikuwepo. Mmoja wa wahudumu aliniambia shelfu zilikuwa zimesalia wazi kwa muda wa siku kadhaa,” aelezea.

Aliona mwanya wa biashara, akaamua kuandama msimamizi wa duka hilo kuona ikiwa angeingia katika maafikiano ya kibiashara awe akisambaza kilichokosekana.

“Alinielekeza kwa wasimamizi wa duka, tukaagana nikiwa tayari nitajiunga na kikosi cha wanaoisambazia,” asema.

Alirejea nyumbani akiwa mkwasi wa mawazo, kuwekeza katika kilimo-biashara cha mboga.

Kwa bahati mbaya ugonjwa wa Covid-19 ukabisha hodi mwezi Machi.

Safari yake ya miaka 25 katika sekta ya utalii ikafikia kikomo. Kagwamba, 48, anafichua alikuwa miongoni mwa wafanyakazi waliopoteza ajira, kufuatia sheria na mikakati iliyowekwa kusaidia kudhibiti msambao.

“Lilikuwa pigo na sikuwa na budi ila kutafuta njia mbadala kutafutia familia riziki,” Kagwamba ambaye ana Stashahada ya Masuala ya Utalii na Shahada ya Uzamili kuhusu Uratibu wa Mikakati na Usimamizi asema.

Aliamua kuingilia shughuli ya uuzaji mashamba na ujenzi, kazi ambayo anaienzi.

“Mwezi Desemba nilinunua kipande cha shamba chenye ukubwa wa thumni ekari Sh5 milioni,” afichua.

Kibarua kilikuwa chaguo la ujenzi wa nyumba za kukodi au kufanya kilimo, kwa mujibu wa mwasisi huyu wa Green Gardens Ltd.

Kikiwa katika mtaa wa Thogoto Greens Estate, Kikuyu, Kaunti ya Kiambu, alikinunua kupitia mkopo.

Mapema mwaka huu, alikigeuza kuwa bustani ya mazao ya matumizi nyumbani.

Alipanda mboga kama vile sukuma wiki, spinachi, kabichi na za kienyeji; mnavu almaarufu managu na pia mchicha.

Vilevile katika orodha ya utangulizi uliomgharimu Sh20,500 alilima bitiruti, pilipili mboga, matango, vitunguu, minji, nyanya na mahindi.

Edward Kagwamba akipalilia vitunguu shambani mwake eneo la Kikuyu, kiungani mwa jiji la Nairobi. PICHA | SAMMY WAWERU

Huku changamoto kuu ikiwa maji, mkulima huyu hutegemea maji ya mradi Kikuyu na ya mvua.

Anasema bustani yake imegeuka kutoka mazao ya matumizi nyumbani na kuwa kitega uchumi.

“Tulipoanza kufanya mavuno, majirani walikuwa wanafurika kununua,” asema.

Anasema taswira ya yalivyonawiri, ilikuwa mvuto kwa kila mpita njia akitaka kujua yalivyozalishwa.

“Kupitia tafiti, nimegundua ukikuza mimea kwa kutumia mfumohai na asilia, soko litakutafuta. Huwa situmii dawa zozote kukabili magonjwa na wadudu,” asisitiza.

Kilimo chake kikiwa hai, anasema hutumia mbolea itokanayo na samadi ya mifugo kama vile ng’ombe, mbuzi na kuku.

Badala ya dawa, hutumia jivu kwa kuimwagilia kwenye majani na mashina ya mimea kukabili wadudu na magonjwa.

Mkulima huyu amegawanyama shamba lake kwa vipande, kusitiri kila mmea.

Majuzi, alijumuisha saladi, karoti na giligilani (dhania).

Wataalamu wanahimiza wakulima kukumbatia mfumo wa ukuzaji mseto wa mimea.

“Ukiwa na mimea mbalimbali, utaweza kusalia sokoni na kuwa na mapato kila wakati kinyume na mkulima anayetegemea zao moja pekee,” asema Geoffrey Kavita, kutoka Amiran Kenya Ltd.

Mdau huyu pia anasema mseto wa mimea huwezesha mkulima kufanikisha kigezo cha mzunguko wa mimea, crop rotation.

Huku shamba la Kagwamba likiwa uga wa mafunzo kuhusu kilimohai bora, amekumbatia matumizi ya mifereji ya sehemu za haja (iliyosalia baada ya ujenzi) na magurudumu ya gari yaliyotumika, kukuza mboga.

Ameunganisha paipu kuunda mfano wa ngazi, na magurudumu kukatwa mara kadha.

Ameweka udongo na mbolea kwenye mifereji aliyotoboa mashimo na magurudumu, na kupanda mboga.

“Teknolojia ya mifereji ni bora kuendeleza kilimo, hasa kwa maeneo ya mijini na ambayo yana upungufu wa ardhi,” Kagwamba akaambia Taifa Leo wakati wa mahojiano.

Kwa sasa, anaendelea kufanya mavuno, kifungu kimoja cha sukuma wiki na kabichi akikiuza kuanzia Sh10 bei ya lango la shamba.

Saladi na dhania, kifungu kimoja ni Sh20 na Sh5 mtawalia.

“Mazao ninayopata ni ya chini mno kukidhi kiwango cha oda ninazopata,” akasema.

“Nimeanza harakati za kuandaa ekari mbili zaidi, niweze kukimu mahitaji ya wateja na pia kusambazia maduka ya kijumla,” akaongeza.

Ana mfanyakazi mmoja. Mbali na uhaba wa maji, ndege pia ni kero kwa mimea na mazao.

You can share this post!

Mshindi wa kwanza wa shindano la Mozzart la Omoka na Moti...

Mwanamke amwagia mpango wa kando Petroli

T L