Habari Mseto

Uhaba wa nyanya waendelea kushuhudiwa bei ikipanda

January 18th, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

UHABA wa nyanya umeshuhudiwa maeneo mbalimbali nchini kufuatia mvua inayoendelea kunyesha.

Kiungo hicho cha mapishi ni miongoni mwa mazao yanayoathirika upesi, hususan kuoza, kiwango cha maji kinapozidi yanayohitajika.

Kwenye uchunguzi wa ‘Taifa Leo’, bei ya nyanya mwezi huu wa Januari imepanda ikilinganishwa na miezi mingine.

Katika soko la Jubilee, lililoko mtaa wa Githurai kiungani mwa jiji la Nairobi, kifungu cha nyanya tatu kinauzwa Sh25.

“Tunazouza Sh25, wakati hakuna uhaba huuza Sh10. Kwa sasa nyanya hazipatikani,” akasema Elizabeth Wanjiku ambaye huuza zao hilo kwenye kibanda-tamba.

Katika kibanda cha mfanyabiashara huyo pia kuna kifungu cha nne Sh20, tatu Sh20 na tatu Sh10 ingawa hali yake si ya kuridhisha.

Soko la Jubilee ni maarufu katika uuzaji wa bidhaa za kula kwa bei nafuu, na mfumuko wa bei ya nyanya unaoshuhudiwa ina maana kuwa zao hilo limeadimika.

Eneo la Roysambu na Zimmerman, bei ya nyanya si tofauti vile na ya mtaa wa Githurai. Kwa mfano, Zimmerman kifungu cha nyanya nne kubwa kinagharimu Sh50.

Nyanya moja ya kadri Zimmerman ni Sh10, ambayo kulingana na Wa Karis zao hilo likiwa kwa wingi huwa Sh5. “Nyanya hazipatikani kwenye mashamba kwa sababu ya mvua kubwa iliyoshuhudiwa mwishoni mwa uliopita, 2019 na inaendelea mwaka huu,” akasema mfanyabiashara huyo.

Aliambia ‘Taifa Leo’ kwamba kreti ya kilo 90 sasa inagharimu kati ya Sh7, 000 – 7, 500. Alisema kipimo hicho, nyanya zikiwa nyingi, hukinunua kati ya Sh2, 000 – 2, 500, kikiwa ghali hakipiti Sh3, 500. “Kwa sasa ninahesabiwa ili nipate angaa faida,” akasema.

Taswira ya mitaa hiyo inawiana na ya eneo la Ruiru, Juja na hata Thika, ambayo ina mashamba yanayokuza nyanya kwa wingi.

Watalaamu wa masuala ya kilimo wanahimiza wakulima kukuza mbegu zinazoweza kustahimili changamoto za wadudu na magonjwa yanayosababishwa na maji.

“Kuna mbegu ambazo hazitatizwi na magonjwa husika ya maji, wakulima wazikumbatie,” ashauri Emmah Wanjiru kutoka kampuni ya HM. Clause na ambayo hutafiti na kuzalisha mbegu za mazao tofauti, nyanya zikiwemo.

Wakulima pia wanashauri kuzingatia muundo wa shamba, wakihimizwa kupanda nyanya eneo lililoinama kiasi ili kuepushia zao hilo athari za maji.

“Eneo lililoinama maji hayatuami mvua kubwa inaposhuhudiwa. Ni muhimu kuandaa mitaro kubadili mikondo ya maji yanayoelekea shambani,” asema Samuel Mwaniki, mkulima mwenye uzoefu wa miaka kadha katika ukuzaji wa nyanya.

Isitoshe, kutokana na ughali wa bidhaa hiyo hasa wakati huu kiwango cha uchumi kinazidi kuwa ghali, watu wanashauriwa kutumia viungo mbadala kama vile pilipili mboga, karoti, matango na giligilani kuongeza mlo ladha.