Habari za Kitaifa

Uhalali wa amri ya kutuma jeshi kukabili maandamano watiliwa shaka


MASWALI yameibuliwa kuhusu uhalali wa hatua ya serikali kuwatuma wanajeshi kukabiliana na waandamanaji jijini Nairobi.

Kupitia tangazo katika Gazeti Rasmi la Serikali Jumanne, Waziri wa Ulinzi Aden Duale alisema ameagiza KDF kusaidia polisi wa kawaida katika shughuli ya ulinzi wa ndani.

Ni hatua iliyoibua hisia kali moja kwa moja, wachanganuzi wakisema jeshi haliwezi kutumwa kwa kazi za polisi bila kupitishwa na Bunge.

Serikali ikaonekana kujibu shutuma hizo Jumatano adhuhuri kwa kutuma ombi hilo Bungeni lililoidhinishwa chini ya dakika 30.

Lakini wachanganuzi wanashikilia kwamba uamuzi huo ungali na dosari.

Waziri wa zamani wa Ulinzi Eugene Wamalwa anapinga agizo hilo akisema ni kinyume cha Katiba akisema lilitolewa bila idhini ya bunge kwanza.

“Hatua hii ikakiuka Katiba kwa sababu utaratibu hitajika haukufuatwa kabla ya kuwahusisha wanajeshi katika maandamano ya raia. Nafahamu hili kwa sababu nilihudumu kama Waziri wa Ulinzi katika serikali iliyopita,” Bw Wamalwa akawaambia wanahabari katika makao makuu ya Chama chake cha Democratic Action Party of Kenya (DAP-K), Nairobi.

Kulingana na kipengele cha 241 (b) cha Katiba, wanajeshi wa Jeshi la Ulinzi Nchini (KDF) wanaweza kusaidia au kushirikiana na vikosi vingine katika kukabiliana na hali ya dharura endapo tu ripoti inawasilishwa katika Bunge la Kitaifa iwapo wanajeshi watatumika katika hali kama hiyo.

Ripoti hiyo inafaa kujadiliwa kwa kina huku wabunge wakitathmini ufaafu, sehemu maalum ambapo wanatumwa na muda kamili wa operesheni yao.

Hata kabla ya Waziri wa Ulinzi Aden Duale kutoa agizo hilo kupitia notisi kwenye toleo maalum la gazeti rasmi la serikali mwendo wa saa moja za usiku Jumanne, wanajeshi walikuwa wamefika kulinda majengo ya bunge yaliyovamiwa na waandamanaji.

Mengine yalionekana yakizunguka katika barabara kadhaa za jiji la Nairobi wanajeshi wakifuatilia kwa makini hali ya usalama.

Kwenye toleo hilo la gazeti rasmi la serikali, Bw Duale alisema maafisa wa KDF walitumwa katikati jijini baada ya fujo hizo kusababisha uharibifu wa mali na uvamizi wa majengo muhimu ya serikali kama Bunge.

“Kwa mujibu wa Kipengele cha 241 (3) (b) ya Katiba ya Kenya ikisomwa pamoja na sehemu za 31 (1) (a), 31 (1), 34 (1) na 34 (2) za Sheria ya Jeshi la Ulinzi la Kenya, maafisa wa KDF wametumwa Juni 25, 2024 kusaidia maafisa wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi kushughulikia dharura ya kiusalama iliyotokana na maandamana yanayoshuhudiwa sehemu mbalimbali nchini. Maandamano hayo yamesababisha uharibu na uvamizi wa majengo muhimu ya serikali,” Bw Duale akasema kwenye notisi hiyo.

Hii sio mara ya kwanza kwa wanajeshi kutumika kupiga jeki maafisa wa polisi kudumisha usalama wa ndani.

Mapema mwaka jana, serikali ya Rais William Ruto iliwahusishwa maafisa wa KDF katika operesheni ya kukabiliana na kero la majangili katika eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa.

Hata hivyo, maafisa hao walihudumu chini ya uelekezi wa wakuu wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS), hali ambayo iliibua maswali mengi.

Aidha, mnamo 2008 serikali ya Hayati Rais Mwai Kibaki ilitumia wanajeshi katika operesheni dhidi ya kundi la wapiganaji la Sabaot Land Defence Forces (SLDF) katika eneo la Mlima Elgon.

Wanajeshi hayo walifaulu kuzima kundi hilo ambalo lilihusishwa na mauaji ya zaidi ya watu 600 kando na kutekeleza maovu mengine kama vile ubakaji.