Habari Mseto

UHALIFU: Watu wawili wauawa Samburu

August 15th, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ONDIEKI

WATU wawili wameuawa na wengine wawili kuachwa na majeraha mabaya ya risasi kwenye shambulio linaloaminika kutekelezwa na wezi wa mifugo katika eneo la Nachola, Kaunti ya Samburu.

Wahanga na majeruhi walifyatuliwa risasi Ijumaa na wahalifu hao walipokuwa wakichunga mifugo yao kwenye kijiji cha Ayanae.

Majeruhi wamekimbizwa katika hospitali ya rufaa ya Samburu mjini Maralal.

Kamanda wa polisi katika kaunti ndogo ya Samburu Kaskazini Tom Makori ameambia Taifa Leo kuwa wawili hao walifariki papo hapo.

Kulingana na afisa huyo, waliopata majeraha wanapokea matibabu katika hospitali ya rufaa ya Samburu, huku miili ya walifariki ikiwa imesafirishwa hadi mjini Maralal ili kuhifadhiwa.

“Wahalifu ambao wanaaminika kutoka jamii ya Pokot walivuka mpaka kwa lengo la kuiba mifugo na hapo wakaanza kufyatuliana risasi,” Bw Makori alisema.

Afisa huyo wa polisi alifichua kwamba jaribio la wezi hao kuiba mbuzi zaidi ya 5,000 lilitibuliwa na maafisa wa polisi ambao walifika kwa wakati na kukabiliana nao.

Kufuatia shambulio hilo, polisi wameshika doria katika eneo hilo ili kuzuia uwezekano wa kulipiza kisasi kwa jamii hizo mbili hasimu.

Bw Makori alihimiza wakazi wa eneo hilo kuishi kwa amani ili kuzuia machafuko zaidi.

“Kwa sasa polisi wanafuata wezi hao hadi mafichoni. Tunaendea na uchunguzi kuhakikisha kwamba wanakamatwa na kufunguliwa mashataka kisheria,” aliongeza.

Kiongozi huyo wa polisi alihimiza viongozi wa kisiasa kuwa katika mstari wa mbele katika vita dhidi ya wizi wa mifugo ambao umekithiri eneo hilo.