Michezo

Uhamisho wa wachezaji KPL ni Desemba

October 16th, 2018 1 min read

Na CECIL ODONGO

Dirisha la uhamisho wa wanasoka mwaka 2018/19 wa ligi ya KPL na ile ya Kitaifa ya Supa (NSL) litafunguliwa rasmi Jumatatu ya Oktoba 29, 2018 kisha lifungwe Ijumaa Januari 4 2019.

Kalenda ya ligi hizo mbili kubwa zimebadilishwa ili ziwiane na ligi nyingine mashuhuri duniani ndiposa msimu huo wa uhamisho pia umebadilika kinyume na zamani ambapo ilifanyika kati ya mwezi Disemba na Januari kila mwaka.

KPL msimu huu itaanza Jumamosi ya Disemba 8 2019 na inatarajiwa kukamilika wikendi ya mwisho ya mwezi Juni mwaka 2019 huku ligi ya Supa ikianza rasmi Jumapili Disemba 2 mwaka 2018.

Ligi ya KPL msimu huu ilitwaliwa na Gor Mahia kwa mara ya 17 nao Western Stima ikijihakikishia marejeo katika KPL kwa mara nyingine baada ya kumaliza kileleni mwa NSL.

Ili kujitayarisha kwa msimu ujao, Gor Mahia tayari wametwaa huduma za aliyekuwa  beki wa kushoto wa mabingwa mara 11 Tusker FC Shafik Batambuze huku Kenneth Muguna akijiunga tena na mabingwa hao. Kutua kwa wawili hao kwenye kambi ya K’Ogalo kutarasmishwa wakati dirisha hilo  la uhamisho litakapofunguliwa.