Uhispania wakomesha rekodi ya kutopigwa kwa Italia katika mechi 37 na kufuzu kwa fainali ya UEFA Nations League

Uhispania wakomesha rekodi ya kutopigwa kwa Italia katika mechi 37 na kufuzu kwa fainali ya UEFA Nations League

Na MASHIRIKA

REKODI ya dunia ya Italia ya kutoshindwa katika mechi 37 ilipigwa breki kali na Uhispania waliowatandika 2-1 mnamo Jumatano usiku katika uwanja wa San Siro na kufuzu kwa fainali ya UEFA Nations League.

Kichapo hicho kiliwawezesha Uhispania kulipiza kisasi dhidi ya Italia waliowabandua kwenye nusu-fainali za Euro 2020 kabla ya hatimaye kutawazwa wafalme wa kipute hicho baada ya kuwazamisha Uingereza kwenye mikwaju ya penalti ugani Wembley.

Mabao mawili kutoka kwa fowadi Ferran Torres wa Manchester City aliyeshikiriana vilivyo na Mikel Oyarzabal jijini Milan, yalisaidia kikosi cha Luis Enrique kufuzu kwa fainali itakayowakutanisha sasa ama na Ubelgiji au Ufaransa.

Italia walikuwa tayari wamechapwa 1-0 kabla ya beki Leonardo Bonucci kufurushwa uwanjani baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya manjano kwa utovu wa nidhamu na kumpiga kumbo kiungo Sergio Busquets wa Uhispania.

Italia walifutiwa machozi na Lorenzo Pellegrini katika dakika ya 83 baada ya kupokezwa krosi murua kutoka kwa Federico Chiesa kupitia shambulizi la kushtukiza.

Uhispania walitumia mechi hiyo kama jukwaa maridhawa la kumwajibisha kiungo chipukizi wa Barcelona, Gavi, tukio lililomfanya kuwa mwanasoka mchanga zaidi kuwahi kuchezeshwa na Uhispania, wiki sita baada ya kuvalia jezi za Barcelona kwa mara ya kwanza.

Ushindi wa Uhispania ulifanya Italia kupoteza mechi ya haiba kubwa katika ulingo wa soka kwa mara ya kwanza katika uwanja wao wa nyumbani tangu 1999.

Torres alitumia mechi hiyo kudhihirisha ukali wake katika ulingo wa soka. Kufikia sasa, amefunga mabao 11 katika mechi za kimataifa tangu Septemba 1, 2020. Hakuna mwanasoka mwingine ambaye amepachika wavuni zaidi ya mabao matano ya kimataifa mwaka huu isipokuwa Torres.

Baada ya Italia kusalia na wanasoka 10 uwanjani, kocha Roberto Mancini alileta uwanjani beki veterani Giorgio Chiellini kujaza nafasi ya mshambuliaji Federico Bernardeschi. Hata hivyo, hatua hiyo haikuzima ari ya Uhispania waliovamia na kukita kambi langoni mwa wenyeji wao.

Kipa Gianluigi Donnarumma aliyesaidia Italia kunyanyua taji la Euro 2020 baada ya kupangua penalti kadhaa za Uingereza kwenye fainali alirushiwa cheche za matusi na mashabiki wa Italia kila alipodaka mpira.

Hilo lilichangiwa na maamuzi ya awali ya mlinda-lango huyo kuagana na AC Milan inayoshiriki Ligi Kuu ya Italia (Serie A) na kuyoyomea Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa.

Italia watafahamu wapinzani wao kwenye hatua ya kutafuta mshindi nambari tatu na nne baada ya gozi la nusu-fainali ya pili kati ya Ubelgiji na Ufaransa uwanjani Juventus, Italia mnamo Oktoba 7, 2021.

Fainali ya UEFA Nations Cup imeratibiwa kutandazwa Jumapili ya Oktoba 10, 2021 uwanjani San Siro baada ya mshindi nambari tatu na nne kufahamika ugani Juventus.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

AKILIMALI: Ni fundi stadi pale kwa mjengo; kubeba mawe,...

Gideon Moi awakosha roho mabwanyenye wa Mlima Kenya huku...