Uhispania wakomoa Ivory Coast na kufuzu kwa nusu-fainali za Olimpiki dhidi ya wenyeji Japan

Uhispania wakomoa Ivory Coast na kufuzu kwa nusu-fainali za Olimpiki dhidi ya wenyeji Japan

Na MASHIRIKA

SUBIRA ya Uhispania kufuzu kwa nusu-fainali ya soka ya Olimpiki kwa mara ya kwanza baada ya miaka 21 iliwavutia heri baada ya kushinda Ivory Coast 5-2 mnamo Julai 31, 2021 na kufuzu kwa nusu-fainali dhidi ya wenyeji Japan.

Japan walishinda New Zealand 4-2 kupitia penalti baada ya kuambulia sare tasa mwishoni mwa muda wa ziada.

Nyota Rafa Mir alitokea benchi katika kipindi cha pili na kufungia Uhispania mabao matatu dhidi ya Ivory Coast. Fowadi Max Gradel alidhani alikuwa amekatia Ivory Coast tiketi ya nne-bora alipofanya mambo kuwa 2-1 mwishoni mwa kipindi cha pili kabla ya Mir kusawazisha mambo sekunde chache baadaye na kulazimisha mshindi kuamuliwa katika muda wa ziada.

Safari ya Ivory Coast kwenye Olimpiki hizo za Tokyo nchini Japan, ilitamatika ghafla baada ya beki Eric Bailly wa Manchester United kusababisha penalti iliyowapa Uhispania bao la tatu kupitia Mikel Oyarzabal wa Real Sociedad. Baily aliyenawa mpira ndani ya kijisanduku ndiye aliwaweka Ivory Coast kifua mbele chini ya dakika 10 za mchezo.

Mir alichuma nafuu kutokana na uchovu wa Ivory Coast mwishoni mwa muda wa ziada na kufungia Uhispania mabao mawili zaidi yaliyozima matumaini finyu ya wapinzani wao.

Ushindi huo uliwarejesha Uhispania kwenye nusu-fainali za Olimpiki kwa mara ya kwanza tangu walipozoa nishani ya fedha mnamo 2000 jijini Sydney, Australia.

Uhispania ndiyo timu ya mwisho ya soka ya wanaume kutoka bara Ulaya kupata tuzo ya dhahabu kwenye Olimpiki mnamo 1992.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Washukiwa watatu wa uhalifu wa kiteknolojia wanaswa Juja

Brazil kuvaana na Mexico katika nusu-fainali za Olimpiki...