Uhispania watandikwa nyumbani kwa mara ya kwanza baada ya miaka minne

Uhispania watandikwa nyumbani kwa mara ya kwanza baada ya miaka minne

Na MASHIRIKA

UHISPANIA walishindwa katika uwanja wa nyumbani chini ya takriban miaka minne baada ya Uswisi kuwapokeza kichapo cha 2-1 kilichodidimiza matumaini yao ya kutinga fainali za Nations League mnamo Juni 2023.

Kichapo hicho kilishuhudia masogora hao wa kocha Luis Enrique wakidenguliwa kileleni mwa Kundi A2 baada ya Ureno watakaovaana nao katika pambano la kufa kupona mnamo Septemba 27, 2022.

Bao la Eric Garcia aliyejifunga dakika tatu baada ya Jordi Alba kusawazishia Uhispania, liliamua mshindi wa mechi hiyo kati ya Uhispania na Uswisi waliowekwa kifua mbele na Manuel Akanji katika dakika ya 21 mjini Zaragoza.

Ilikuwa mechi ya kwanza kwa Uhispania kupoteza nyumbani baada ya mapambano 22 katika mashindano yote tangu wapepetwe na Uingereza 3-2 katika Uefa Nations League mnamo Oktoba 2018.

Kichapo hicho wakati huo ndicho cha pekee walichopokezwa baada ya mechi 56 za awali katika uwanja wa nyumbani. Kichapo kutoka kwa Uswisi kilikuwa cha pili kwa Uhispania kupokezwa nyumbani tangu 2003.

Ushindi dhidi ya Uswisi na kichapo kwa Ureno kutoka kwa Jamhuri ya Czech mnamo Jumamosi kingaliwakatia Uhispania tiketi ya kunogesha fainali za Nations League mwakani. Hata hivyo, wanafainali hao wa 2021 sasa watashuka dimbani kwa ajili ya mchuano wa mwisho wa Kundi A2 wakikamata nafasi ya pili kwa alama nane, mbili nyuma ya viongozi Ureno.

Uswisi waliokomoa Ureno 1-0 katika mkondo wa kwanza mnamo Juni 2022, walijiondoa mkiani mwa Kundi A2 na kupisha Jamhuri ya Czech waliopepetwa na Ureno 4-0.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Mahakama yatarajiwa kutoa sababu kamili za kutupilia mbali...

Jentrix Shikangwa na beki Ruth Ingotsi watarajiwa kujiunga...

T L