Uhispania wazamisha Uswisi kupitia penalti na kufuzu kwa nusu-fainali za Euro

Uhispania wazamisha Uswisi kupitia penalti na kufuzu kwa nusu-fainali za Euro

Na MASHIRIKA

MABINGWA mara tatu wa Euro, Uhispania, waliwaondoa Uswisi kwenye robo-fainali za Euro mnamo Julai 2, 2021 kwa kuwapokeza kichapo cha 3-1 kupitia penalti.

Uswisi walikamilisha mchuano huo wakiwa na wachezaji 10 pekee uwanjani baada ya Remo Freuler kuonyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 77.

Ruben Vargas aliyetokea benchi katika kipindi cha pili kwa upande wa Uswisi alibubujikwa na machozi baada ya kupulizwa kwa kipenga cha kuashiria mwisho wa mechi.

Nyota huyo alipaisha mkwaju wake wa penalti kabla ya Mikel Oyarzabal kufungia Uhispania mkwaju wa ushindi.

Uhispania ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya sita kimataifa kwenye orodha ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), pia walihitaji muda wa ziada kuwaondoa Croatia kwenye hatua ya 16-bora licha ya kujivunia uongozi wa 3-1 hadi dakika ya 85.

Walianza mechi yao dhidi ya Uswisi kwa matao ya juu jijini St Petersburg, Urusi huku kiungo Denis Zakaria wa Uswisi akijifunga katika dakika ya nane baada ya kuzidiwa na presha kutoka kwa beki Jordi Alba.

Nahodha wa Uswisi, Xherdan Shaqiri alisawazisha katika dakika ya 68, tisa kabla ya Freuler kufurushwa uwanjani kwa kadi nyekundu baada ya kumkabili visivyo Gerard Moreno.

Uhispania watakutana sasa na Italia kwenye nusu-fainali mnamo Julai 6, 2021 uwanjani Wembley, Uingereza. Hii ni baada ya Italia ya kocha Roberto Mancini kubandua Ubelgiji kwa kichapo cha 2-1.

Uhispania wanaotiwa makali na kocha Luis Enrique walipoteza nafasi nyingi za kufunga mabao kupitia kwa Alba, Cesar Azpilicueta na Pau Torres ambaye masihara yake na Aymeric Laporte yalisaidia Uswisi kusawazisha na kurejea mchezoni.

Mechi dhidi ya Italia inatarajiwa kuwa kipimo halisi cha uthabiti wa Uhispania ikizingatiwa kwamba masogora wa Mancini walidengua kikosi kinachoshikilia nafasi ya kwanza duniani.

Uhispania walitawazwa mabingwa wa Euro mnamo 1964, 2008 na 2012; na wakaibuka wafalme wa Kombe la Dunia mnamo 2010 nchini Afrika Kusini. Walicharaza Slovakia 5-0 katika mchuano wa mwisho wa Kundi E baada ya kulazimishiwa sare tasa na ya 1-1 dhidi ya Uswidi na Poland kwenye mechi mbili za ufunguzi.

Kikosi hicho kilijikatia tiketi ya robo-fainali baada ya kubandua wanafainali za Kombe la Dunia mnamo 2018, Croatia, kwa kichapo cha 5-3.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

AU yalaani ghasia Eswatini maandamano yakichacha

Warembo na ganda la chungwa