Michezo

Uhispania yazamisha chombo cha Uswisi katika Nations League na kudhibiti kilele cha Kundi A4

October 11th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

UHISPANIA walisalia kileleni mwa kundi lao kwenye mechi za Uefa Nations League baada ya kusajili ushindi mwembamba wa 1-0 dhidi ya Uswisi mnamo Oktoba 10, 2020 jijini Madrid.

Fowadi matata wa Real Sociedad, Mikel Oyarzabal alifunga bao la upekee na la ushindi kwa upande wa Uhispania kunako dakika ya 14.

Mechi ilikuwa ya kwanza kwa kiungo mvamizi wa Wolves, Adama Traore kuchezea timu ya taifa ya Uhispania. Naye kiungo wa Liverpool, Xherdan Shaqiri alisakatia Uswisi baada ya kupona ugonjwa wa Covid-19.

Kipa David De Gea aliyeaminiwa kujaza pengo la mlinda-lango wa Chelsea, Kepa Arrizabalaga, alilazimika kufanya kazi ya ziada kuwanyima mafowadi wa Uswisi nafasi kadhaa za kufunga mabao.

Kati ya wanasoka waliomtatiza pakubwa De Gea mwishoni mwa kipindi cha pili ni Loris Benito anasakatia kikosi cha Bordeaux cha Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1).

Bao la Uhispania lilikuwa zao la masihara makubwa ya kipa Yann Sommer ambaye alijaribu kutoa pasi dhaifu iliyofikiwa na Mikel Merino aliyeshirikiana vilivyo na Oyarzabal.

Baada ya kosa hilo, Sommer alijitahidi maradufu langoni na akafaulu kupangua makombora mazito aliyoelekezea na sajili mpya wa Manchester City, Ferran Torres aliyetua uwanjani Etihad msimu huu baada ya kushawishiwa kuagana na Valencia ya Uhispania kwa kiasi cha Sh2.8 bilioni.

Oyarzabal alikosa nafasi kadhaa za wazi za kufungia Uhispania mabao zaidi mwishoni mwa kipindi cha kwanza.

Chipukizi wa Barcelona, Ansu Fati aliridhisha sana katika mchuano huo kwa upande wa Uhispania kabla ya kuondolewa uwanjani katika kipindi cha pili na nafasi yake kutwaliwa na Traore, 24.

Katika mechi nyingine ya Kundi A4, Ujerumani waliwatandika Ukraine 2-1 na kupunguza pengo la alama kati yao na viongozi Uhispania hadi pointi mbili baada ya kila mmoja kupiga jumla ya michuano mitatu.