Uholanzi, Croatia zatinga 4-bora

Uholanzi, Croatia zatinga 4-bora

Na MASHIRIKA

CROATIA na Uholanzi ndiyo mataifa ya kwanza kufuzu kwa nusu-fainali za UEFA Nations League baada ya kushinda mechi zao za mwisho katika hatua ya makundi mnamo Jumapili.

Uholanzi walinyamazisha Ubelgiji 1-0 katika pambano la Kundi A4 lililowakutanisha jijini Amsterdam huku Croatia wakipokeza Austria kichapo cha 3-1 katika mechi ya Kundi A1 iliyochezewa Vienna.

Ilikuwa mara ya kwanza baada ya mechi 50 kwa Ubelgiji kukamilisha mchuano bila kufunga bao.

Croatia walikamilisha kampeni za kundi lao kwa alama 13, moja zaidi kuliko nambari mbili Denmark.

Wafalme wa dunia, Ufaransa, waliokung’utwa na Denmark 2-0 jijini Copenhagen, waliambulia nafasi ya tatu kwa pointi tano, moja mbele ya Austria. Hivyo, waliponea chupuchupu kuteremshwa ngazi hadi League B.

Chini ya kocha Louis van Gaal, Uholanzi walidhibiti kilele cha Kundi A4 kwa alama 16, sita kuliko Ubelgiji walioridhika na nafasi ya pili.

Wales walivuta mkia wa kundi hilo kwa alama moja baada ya kupiga sare moja na kupoteza mechi tano kati ya sita. Waliteremshwa ngazi kutoka kwenye kikoa cha vikosi vya haiba kubwa barani Ulaya baada ya kutandikwa 1-0 na Poland waliomaliza wa tatu kwa pointi saba.

Uholanzi sasa wataelekea nchini Qatar kwa ajili ya fainali za Kombe la Dunia mnamo Novemba wakijivunia rekodi nzuri ya kutopigwa katika mechi 15 zilizopita.

Wales kwa upande wao watafungua Kombe la Dunia – wanalolishiriki kwa mara ya kwanza baada ya miaka 64 – dhidi ya Amerika mnamo Novemba 21.

Nusu-fainali za Nations League zitatandazwa mnamo Juni 14-15 mwaka ujao huku mechi ya fainali na ya kutafuta mshindi nambari tatu na nne zikipangwa kusakatwa Juni 18.

Mwenyeji wa michuano hiyo ya hatua ya nne-bora na fainali atafichuliwa Januari 2023. Mataifa yote yanayounga Kundi A4 – Ubelgiji, Poland, Uholanzi na Wales – yamewasilisha maombi ya kuwa waandalizi.

Leo Jumanne itakuwa zamu ya Ureno kualika Uhispania jijini Braga kwa mchuano wa kufa kupona wa Kundi A2 wa kupigania nafasi ya mwisho ndani ya nne-bora.

Ureno watapania kuendeleza ubabe uliowavunia ushindi wa 4-0 dhidi ya Jamhuri ya Czech katika mchuano uliopita huku Uhispania wakilenga kujinyanyua baada ya Uswisi kuwatandika 2-1 mjini Zaragoza wikendi iliyopita na kudidimiza matumaini yao ya kutinga nne-bora kwenye Nations League.

Chini ya kocha Fernando Santos, Ureno walitawazwa mabingwa wa makala ya kwanza ya Nations League mnamo 2018-19 baada ya kupepeta Uholanzi 1-0 katika fainali iliyochezewa jijini Porto.

Sasa wanadhibiti kilele cha Kundi A2 kwa alama 10, mbili zaidi kuliko Uhispania waliopepetwa na Ufaransa 2-1 kwenye fainali ya Nations League 2021 jijini Milan, Italia.

Uswisi wanaokamata nafasi ya tatu kwa pointi sita, watakuwa leo wenyeji wa Czech ugani Kybunpark. Czech wanavuta mkia kwa pointi nne baada ya kushinda mechi moja, kupiga sare mara moja na kupoteza michuano mitatu kundini.

Walipokutana mara ya mwisho katika Nations League mnamo Juni, Uhispania wanaotiwa makali na kocha Luis Enrique, walilazimishia Ureno sare ya 1-1 katika uwanja wa Benito Villamarin jijini Seville.

  • Tags

You can share this post!

Wales wateremshwa ngazi kwenye Nations League baada ya...

Uingereza na Ujerumani waambulia sare ya 3-3 katika Nations...

T L