Michezo

Uholanzi kukosa difenda nguli inapokabili Estonia

November 19th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

AMSTERDAM, UHOLANZI

BEKI Virgil van Dijk hatakuwa sehemu ya kikosi cha Uholanzi kitakachochuana leo Jumanne na Estonia jijini Amsterdam katika mchuano wa mwisho wa kufuzu kwa fainali za Euro 2020.

Sogora huyo wa zamani wa Liverpool aliyetokea Southampton alitegemewa zaidi na Uholanzi katika sare tasa waliyosajili dhidi ya Northern Ireland mnamo Jumamosi.

Matokeo hayo yaliwapa tiketi ya kushiriki fainali zijazo.

Kulingana na Shirikisho la Soka la Uholanzi (KNVB), Van Dijk ambaye ni nahodha wa timu yake ya taifa, atakosa mechi dhidi ya Estonia kwa sababu za kibinafsi na tayari ameondoka kambini kurejea Uingereza.

Van Dijk, 28, hajakosa hata dakika moja katika michuano yote ambayo imepigwa na Liverpool hadi kufikia sasa katika kipute cha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL). Ushawishi wake kila awapo ugani ni kiini cha Liverpool kutawala kampeni za EPL hadi kufikia sasa msimu huu ambapo wanaselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 34, nane zaidi kuliko Leicester City wanaoshikilia nafasi ya pili.

Manchester City ambao ni mabingwa watetezi wa kivumbi hicho, wanafunga mduara wa nne-bora kwa alama 25, moja nyuma ya Chelsea ambao wapo nyuma ya Leicester kutokana na uchache wa mabao yao.

Mchuano ujao wa Liverpool ligini ni kivumbi kitakachowakutanisha na Crystal Palace uwanjani Selhurst Park mwishoni mwa wiki hii.

Van Dijk aliwagharimu Liverpool kima cha Sh9.8 bilioni aliposhawishiwa kuagana na Southampton mnamo Januari 2018. Tangu wakati huo, amewajibishwa na Liverpool katika mechi 64 kati ya 66 katika EPL.

Wakati uo huo, Ufaransa ambao ni mabingwa wa dunia, walikamilisha kibarua chao cha kufuzu kwa fainali za Euro 2020 kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya Albania na hivyo kuibuka kileleni mwa Kundi H.

Ufaransa walihitaji ushindi ili kuwapiga kumbo Uturuki waliokuwa wapinzani wao wakuu kundini. Corentin Tolisso aliwaweka Ufaransa kifua mbele kunako dakika ya nane kabla ya Antoine Griezmann wa Barcelona kuongeza bao la pili katika dakika ya 31.

Nusura Olivier Giroud wa Chelsea awafungie Ufaransa bao la tatu mwishoni mwa kipindi cha kwanza ila akashuhudia kombora lake likibusu mwamba wa goli.

Ufaransa ambao walisajili ushindi mara nane kutokana na mechi 10 za Kundi H, kwa sasa wanajivunia alama 25, mbili nyuma ya Uturuki waliowalazimishia sare katika mchuano wa kwanza kisha kuwalaza wakati wa marudiano jijini Istanbul.

Ufaransa, Uhispania na Ujerumani huenda zikawa timu sita kati ya 10 zitakazounga matapo makuu wakati wa droo ya Euro 2020.

Uhispania walichuana na Romania hapo jana huku Ujerumani wakijiandaa kupimana ubabe na Northern Ireland hii leo Jumanne.

Kwa upande wao, Uingereza walikamilisha kampeni zao za kufuzu kwa ushindi wa 4-0 dhidi ya Kosovo mnamo Jumaapili. Mabao ya Uingereza yalifumwa wavuni kupitia kwa Harry Winks, Harry Kane, Marcus Rashford na Mason Mount. Vibarua vijavyo kwa Uingereza ni mechi mbili za kirafiki zitakazopigwa kati ya Machi 23-31, 2020.