Michezo

Uholanzi na Ujerumani zashinda mechi za Euro

October 15th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

MINSK, BELARUS

UHOLANZI na Ujerumani walijizolea alama muhimu za ugenini katika mechi za kufuzu kwa fainali za Euro 2020 mnamo Jumapili na hivyo kudidimiza zaidi matumaini ya Northern Ireland kunogesha kivumbi hicho cha mwakani.

Kiungo matata wa Liverpool, Georginio Wijnaldum alifunga mabao mawili katika kipindi cha kwanza na kusaidia Uholanzi kuwachabanga Belarus 2-1 jijini Minsk.

Kwingineko, Ujerumani waliokamilisha mechi wakiwa na wachezaji tisa uwanjani walihitaji mabao mawili kutoka kwa nyota Ilkay Gundogan wa Manchester City ili kukizamisha chombo cha Estonia kwa mabao 3-0.

N. Ireland kwa sasa wanasalia wa tatu katika Kundi C kwa alama 12, tatu nyuma ya viongozi Uholanzi wanaorodheshwa mbele ya Ujerumani kwa wingi wa mabao.

Chini ya kocha Michael O’Neil, N. Ireland kwa sasa wana ulazima wa kuwabwaga Uholanzi mbele ya mashabiki wao wa nyumbani kisha kuwalaza Ujerumani ugenini katika michuano miwili ijayo ya mwisho.

Uholanzi walikaribia kufuzu kwa fainali za Euro 2020 baada ya Wijnaldum kuwafungulia ukurasa wa mabao katika dakika ya 32 kisha kuongeza la pili dakika tisa baadaye.

Ingawa Stanislav Dragun alipania kuwarejesha Belarus mchezoni katika dakika ya 53, jitihada zake hazikufaulu kuzima makali ya Uholanzi ambao kwa sasa wananolewa na kocha wa zamani wa Everton, Ronald Koeman.

Ujerumani walichelewesha zaidi safari ya kufuzu kwa Uholanzi baada ya kujituma maradufu na kuvuna ushindi jijini Tallinn. Baada ya kuambulia sare tasa mwishoni mwa kipindi cha kwanza, Emre Can alionyeshwa kadi nyekundu. Ingawa hivyo, Ujerumani walitwaa uongozi kupitia kwa mabao mawili ya haraka ya Gundogan.

Werner azititiga nyavu

Bao jingine la Ujerumani lilifungwa na Timo Werner aliyetokea benchi katika dakika ya 72 na kushirikiana vilivyo na Gundogan.

Ubelgiji ambao tayari wamefuzu kwa fainali za Euro 2020, waliendeleza ubabe wao kwa kusajili ushindi wa 2-0 dhidi ya Kazakhstan ambao tayari wamebanduliwa kwenye Kundi I.

Fowadi Michy Batshuayi wa Chelsea alikamilisha krosi ya kiungo Dennis Praet wa Leicester City kwa ustadi mkubwa kabla ya Eden Hazard kumwandalia Thomas Meunier pasi iliyozalisha goli la pili.

Chini ya mkufunzi Roberto Martinez, Ubelgiji kwa sasa wamefunga jumla ya mabao 30 na nyavu zao kutikiswa mara moja pekee katika jumla ya mechi zote nane za hadi kufikia sasa kundini mwao.

Urusi ambao wanashikilia nafasi ya pili huenda wakaungana na Ubelgiji iwapo watasajili sare ya aina yoyote dhidi ya Cyprus ugenini. Scotland na San Marino ambao ni wapinzani wengine katika Kundi I tayari wamebanduliwa.