Uholanzi wacharaza Austria na kuingia 16-bora kwenye fainali za Euro

Uholanzi wacharaza Austria na kuingia 16-bora kwenye fainali za Euro

Na MASHIRIKA

UHOLANZI walitinga hatua ya 16-bora kwenye kivumbi cha Euro baada ya kuchabanga Austria 2-0 katika mchuano wa Kundi C uliowakutanisha mnamo Alhamisi usiku mbele ya mashabiki 12,000 katika uwanja wa Johan Cruyff Arena jijini Amsterdam.

Chini ya kocha Frank de Boer, Uholanzi walijibwaga ulingoni kwa ajili ya mchuano huo baada ya kuwakomoa Ukraine 3-2 katika mchuano wa ufunguzi wa mechi za Kundi C mnamo Juni 13, 2021.

Fowadi Memphis Depay aliwaweka Uholanzi kifua mbele kupitia penalti ya dakika ya 11 baada ya beki David Alaba kumwangusha Denzel Dumfries ndani ya kijisanduku. Dumfries alifungia Uholanzi goli la pili katika dakika ya 67.

Uholanzi ambao hawakufuzu kwa fainali za Euro 2016 na Kombe la Dunia mnamo 2018, sasa wametinga hatua ya mwondoano ya Euro kwa mara ya kwanza tangu mwaka wa 2008.

Austria walianza kampeni za Kundi C kwa ushindi dhidi ya Macedonia Kaskazini na matumaini yao ya kusonga mbele kwenye kampeni za kipute hicho yataamuliwa baada ya mchuano wa mwisho wa makundi dhidi ya Ukraine mnamo Juni 20.

De Boer aliwaongoza vijana wake kuvaana na Austria akitumia mfumo wa 5-3-2 uliokashifiwa pakubwa na mashabiki wakati wa mechi za kirafiki zilizopigwa na kikosi chake kabla ya fainali za Euro kung’oa nanga.

Licha ya kukosolewa, mfumo huo uliokumbatiwa na Uholanzi katika mchuano wa ufunguzi wa Kundi C, uliwavunia ushindi wa 3-2 dhidi ya Ukraine mnamo Juni 13.

Uholanzi wamefuzu kwa hatua ya mwondoano kwenye kampeni za soka ya haiba kubwa kwa mara ya kwanza tangu watinge nusu-fainali za Kombe la Dunia mnamo 2014 nchini Brazil.

Kikosi hicho sasa atakutana na timu moja kati zile zitakazokamilisha kampeni za Kundi D, E au F katika nafasi ya tatu kwenye hatua ya 16-bora.

Austria watavaana na Ukraine katika mchuano ujao wa Kundi C mnamo Juni 21 huku Uholanzi wakikamilisha udhia dhidi ya Macedonia Kaskazini.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

‘Plan B’ ya Kenya Shujaa baada ya ziara ya Los...

Gor Mahia yapigiwa chapuo kuendeleza ubabe kwenye kampeni...