Uholanzi wakanyaga Ukraine 3-2 kwenye Euro

Uholanzi wakanyaga Ukraine 3-2 kwenye Euro

Na MASHIRIKA

MWANASOKA Denzel Dumfries alifunga bao katika dakika za mwisho na kusaidia Uholanzi kuwapepeta Ukraine 3-2 katika mechi ya Kundi C kwenye fainali za Euro mnamo Jumapili jijini Amsterdam.

Kocha Frank de Boer anapania kutumia kipute cha Euro kuwasadikisha mashabiki wa Uholanzi kwamba ndiye aliyestahili kutwaa mikoba ya kikosi hicho baada ya mkufunzi Ronald Koeman kuajiriwa na Barcelona mwishoni mwa msimu wa 2019-20.

Georginio Wijnaldum aliyefungia Uholanzi mabao manane kwenye mechi za kufuzu kwa Euro, alifungua ukurasa wa magoli katika dakika ya 52 kabla ya Wout Weghorst kufanya mambo kuwa 2-0 dakika sita baadaye.

Hata hivyo, Ukraine walirejea mchezoni katika dakika ya 75 kupitia kwa Andriy Yarmolenko kabla ya Roman Yaremchuk kusawazisha mambo dakika nne baadaye.

Dumfries ndiye aliyeokoa chombo cha Uholanzi katika dakika ya 85 baada ya kukamilisha krosi ya beki Nathan Benjamin Ake wa Manchester City.

Uholanzi wanarejea kushiriki fainali za Euro mwaka huu baada ya kuwa nje kwa kipindi cha miaka 10. De Boer anaongoza kikosi hicho kushiriki kampeni za Euro baada ya kusimamia mechi 11 ambapo ameshuhudia masogora wake wakishinda michuano mitano, kuambulia sare mara nne na kupoteza mara mbili dhidi ya Mexico na Uturuki.

Ukraine kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Macedonia Kaskazini mnamo Juni 17 jijini Bucharest huku Uholanzi wakialika Austria jijini Amsterdam.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Austria wapepeta North Macedonia na kuvuna ushindi wao wa...

Nafula atinga bao AE Larissa ikishinda shaba kwenye Ligi...